Sunday, May 11, 2025
spot_img

KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA SGR DAR – MORO

 

MWANDISHI MAALUMU

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga jana alifanya ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Katika ziara hiyo, Balozi Katanga aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Gabriel Migire, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Prof. John Kondoro pamoja na Menejimenti ya Shirika la Reli Tanzania.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Katibu Mkuu Migire alisema lengo la ziara lilikuwa kumfahamisha Katibu Mkuu Kiongozi Katanga mwenendo mzima wa kazi  na kumpitisha katika eneo la mradi.

Alisema Balozi Katanga kama mtendaji mkuu wa Serikali amekuwa akifikishiwa taarifa za mwenendo wa mradi huo lakini pia ni muhimu kwake kufika eneo la mradi kujiridhisha na taarifa ambazo amekuwa akipatiwa.

“Katibu Mkuu Kiongozi ameridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika, ameona kwa mara ya kwanza nchi imefanya uwekezaji mkubwa na ametutaka tuhakikishe tunafikia matarajio ya nchi na tunaweka mazingira mazuri ya kutafuta bidhaa na masoko katika reli hii ya kisasa”

“Tumetokea Pugu hadi Morogoro kwa treni, tumeshafanya manunuzi ya vichwa na mabehewa kwa ajili ya kuanza majaribio, lakini watengenezaji wana changamoto ya UVIKO19 kwa hiyo tulishindwa kupata vichwa na mabehewa.

“Tulitarajia kufanya majaribio mwezi Disemba lakini kutokana na changamoto ya UVIKO19 vichwa na mabehewa vitapokelewa kuanzia mwezi Machi 2022,” alisema Katibu Mkuu Migire.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC, Prof. Kondoro yeye alisema ni mara ya kwanza kwa Katibu Mkuu Kiongozi kutembelea mradi wa SGR na ilikuwa fursa kwa shirika kuelezea mafanikio, changamoto pamoja na mipango yake ikiwemo uendelezaji wa mradi wa SGR kutoka Mtwara hadi Bamba Bay, Tanga hadi Musoma, Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma na nchi za jirani.

Aidha, Prof. Kondoro alisema Balozi Katanga alipata ufafanuzi kuhusu mafanikio ya shirika katika utoaji huduma na namna linavyoshirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuimarisha huduma za usafirishaji wa mizigo.


 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema Katibu Mkuu Kiongozi alipata taarifa ya shirika hususani katika mradi wa ujenzi SGR na aliridhishwa na mwenendo wa kazi.

Kadogosa alisema Balozi Katanga alitoa maagizo kwa uongozi wa TRC kuboresha zaidi utendaji wake.


 



Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya