Tuesday, August 26, 2025
spot_img

WAIRAQW WATIKISA DAR ES SALAAM

 

 

Balozi Dk. Willbrod Slaa akizungumza na jamii ya Wairaqw waishio Dar es Salaama na waliotoka Mkoa wa Manyara kwenye tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam

MWANDISHI MAALUMU

JAMII ya Wairaqw waishio Dar es Salaam (UMBLUCHA) wamefanya tamasha kubwa Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha jamii ya kabila hilo inayoishi mijini kuziishi mila na desturi zao.

Tamasha hilo lililofanyika hivi karibuni pia lililenga kuwarithisha watoto hasa wanaozaliwa na kuishi mijini mila na desturi pamoja na kuibua mawazo ya utalii wa mazao ya utamaduni.

Akizungumza na wanajumuia ya kabila hilo, mgeni rasmi katika tamasha hilo, Balozi Dk. Willibrod Slaa amewaasa watanzania hasa wazazi kuwarithisha watoto utamaduni wao ili waendelee kukua katika maadili mema.

Dk. Slaa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwenye uhifadhi wa utamaduni wa mtanzania hasa kwa serikali anayoingoza kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha Kijiji cha Makumbusho kilichopo chini ya Makumbusho ya Taifa nchini.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk. Noel Lwoga, Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Mawazo Ramadhani Jamvi amesema taasisi hiyo imeweka utaratibu wa kushirikiana na makabila mbalimbali kufanya matamasha ya kiutamaduni yenye lengo la uhifadhi na urithishaji wa urithi wa utamaduni.

Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Mawazo Ramadhani Jamvi akizungumza na jamii ya Wairaqw waishio Dar es Salaama na waliotoka Manyara kwenye tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.

 

Licha ya kuwapongeza jumuiya ya Wairaq waishio Dar es Salaam kwa kuamua kuratibu tamasha hilo, alisema Makumbusho ya Taifa itaendela  kuwa karibu nao na hata kuhakikisha ujenzi wa nyumba ya kabila hilo unafanyika kwenye kijiji hicho ili kutangaza na kuhifadhi urithi wa kabila hilo.

Mmoja wa washiriki wa tamasha hilo, Dk. Leonia Hambati ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema amejisikia fahari kuendelea kudumisha utamaduni wake awapo mjini na anafanya hivyo kwa watoto wake bila kuangalia elimu yake wala mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayochochea kasi ya uytandawazi unaoharibu mitazamo ya vijana kuhusu utamaduni wao.

Naye Dk. Baltazary Awe aliyeongea kwa niaba ya Jamii ya Wairaqw (UMBLUCHA) waishio Dar es Salaam, amesema jumuiya yao imeona umuhimu wa kufanya tamasha hilo ili kujikumbushia mambo yanayohusu utamaduni wao, kuhakikisha watoto wao wanajifunza kutoka kwa wazee waishio vijijini na kuowaonesha wengine utajiri uliopo kwenye utamaduni huo.

Mwenyekiti wa jamii ya Wairaqw, Dk. Baltazary Awe akiburudika na wanajamii wa Kiiraqw kwa kunywa pombe aina ya Magure kwenye tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam.

 

 

Tamasha hilo lililochukuwa siku mbili na kufurahiwa na wageni wa ndani na nje ya nchi, lilipambwa na ngoma za asili za kabila hilo, vyakula vya asili, majigambo, masimulizi ya wazee nyakati ya usiku, mapishi ya pombe maarufu ya kabila hilo ijulikanayo kama magure, michezo ya jadi na dua kutoka kwa wazee wa mila walioi ombea nchi, Rais Samia na Serikali ya Tanzania pamoja na muungano.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya