Uongozi wa TIRTEC ukiwa katika pamoja na viongozi wa Shirika wa Reli (TRC) na viongozi wa Serikali wa Wilaya ya Tabora wakati wa mahafali ya kwanza ya chuo hicho. (Picha kwa hisani ya TRC) |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
SHIRIKA la Reli (TRC) linakusudia kukijengea uwezo zaidi wa utoaji taalamu Chuo cha Teknolojia ya Reli Tanzania (TIRTEC) ili kiweze kutoa wahitimu waliobobea katika fani ya uendeshaji wa reli.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo cha TIRTEC, Damas Mwajanga alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Reli Tabora, Disemba 18, 2021.
Mwajanga alisema TRC ina mpango wa kuboresha miundombinu ya chuo hicho ili kiweze kuzalisha wataalamu wengi zaidi na kuanzisha kozi mpya ili kukidhi mahitaji ya sasa, hususani katika shughuli za uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR sambamba na kuwawezesha wahitimu kujiajiri.
Alisema hatua iliyofikiwa na chuo anachokiongoza ya kutoa wahitimu wa kwanza wa taaluma mbalimbali kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada imetoa taswira njema inayoonyesha kuwa kinaweza kinazalisha wataalamu wengi zaidi ili kuendana na mahitaji ya watalaamu katika sekta ya usafirishaji wa reli.
Wahitimu wa Astashahada na Stashahada kwa kada za usafirishaji, teknolojia ya matengenezo ya njia ya reli |
ukaguzi na matengenezo ya behewa wakielekea katika viwanja vya Chuo cha Reli Tabora kwa ajili ya mahafali yao. (Picha kwa hisani ya TRC)
Mwajanga alisema licha ya changamoto za hapa na pale zinazokikabili chuo hicho, kimeweza kuunda bodi ya ushauri ya chuo, kuboresha taaluma, kujenga uzio, kuimarisha nidhamu ya wanafunzi, kushiriki katika makongamano ya kitaaluma, kusajili chuo na kupewa ithibati pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk. Yahaya Nawanda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo aliahidi kuendelea kushirikiana na chuo pamoja na kukilinda muda wote.
Nawanda alilitaka TRC kushughulikia changamoto zinazopo chuoni hapo ili kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na watumishi.
Naye Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TRC, Amina Lumuli aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika mahafali hayo alisema, TRC imepokea changamoto zilizopo chuoni hapo na itazitatua kulingana na uwezo uliopo ili kuboresha mazingira yake.
Lumuli alisema TRC imeshaanza kushughulikia baadhi ya changamoto hizo ikiwemo usafiri na ujenzi wa miundombinu ya chuo.
Alisema changamoto hizo zinashughulikiwa kupitia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa, kipande cha Makutupora hadi Tabora.
Pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk. Nawanda na Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TRC, Lumuli, wengine waliohudhuria mahafali hayo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Washauri ya TIRTEC, Mhandisi Alfred Ng’hwani, wajumbe wa bodi ya ushauri ya chuo, wafanyakazi, wahitimu na wanafunzi.
Chuo cha Teknolojia ya Reli kilianzishwa mwaka 1947 na wakoloni ili kukidhi mahitaji ya wakati huo na baadaye kiliendelea kusimamiwa na TRC kabla ya hivi karibuni kuanza kujengewa uwezo zaidi wa utoaji taaluma katika fani ya usafirishaji wa reli .
TIRTEC kina jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa TRC na kuandaa wataalamu wa kada mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa huduma za Shirika la Reli.
Kinatoa kozi mbalimbali katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kada za usafirishaji, teknolojia ya matengenezo ya njia ya reli, ukaguzi na matengenezo ya behewa pamoja na kozi za muda mfupi kwa ajili ya watumishi wa TRC.
Aidha, TIRTEC kinatoa mafunzo kwa watumishi wa taasisi nyingine zinazohusika na usafiri wa reli ikiwemo Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia – TAZARA na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi kavu – LATRA.