Mganyabiashara Ugur Gurses anayetuhumiwa kuuza umeme bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), imelirejesha kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) faili la mfanyabiashara Ugur Gurses anayetuhumiwa kulangua umeme, kufanya biashara ya umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kukataa kupokea karipio la kisheria la EWURA la kutojihusisha na vitendo vya uvunjivu wa sheria.
Hayo yameelezwa mapema wiki hii na Mkuu wa Mashtaka, Mkoa wa Dar es Salaam (PRO), Pius Hilla alipokuwa akizungumzia hatua zilizofikiwa na ofisi ya DPP kushughulikia shauri hilo.
PRO Hilla alisema baada ya DPP kulipitia faili hilo aliamua kulirejesha EWURA akiwa ameielekeza kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi zaidi kuhusu shauri hilo.
“Faili la mtuhumiwa huyo limetoka ofisini kwa DPP, amelirejesha EWURA akiwa ameelekeza ishirikiane na DCI kufanya uchunguzi zaidi wa shauri hilo kisha mambo mengine ndiyo yataendelea,” alisema PRO Hilla.
Gurses anatuhumiwa kulangua umeme, kufanya biashara ya umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kukataa kupokea karipio la kisheria la mamlaka hiyo la kutojihusisha na vitendo vya uvunjivu wa sheria,
EWURA ndiyo inayomtuhumu Gurses, raia wa Uturuki na mmiliki wa Kampuni ya Adamas Group yenye ofisi zake Karioakoo, Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya nyumba.
Awali, Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo aliiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa Gurses ana makosa mawili, la kwanza ni kuuza umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kosa la pili ni kuuza umeme kwa bei ya juu.
Alisema EWURA baada ya kubaini makosa hayo kwa Gurses ilimpelekea karipio la kisheria lakini alikataa kulipokea hivyo ililifikisha shauri hilo kwa DPP ambaye ana nguvu za kisheria na pia ana vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
“Huyu mtu ana makosa yafuatayo, moja kuuza umeme wakati hana leseni ya EWURA, mbili kuuza umeme kwa bei ya juu. Tulimpelekea ‘complaince order’ karipio la kisheria na alikataa kupokea.
“Katika hali kama hii, sheria inatutaka tumpelekee DPP ambaye ana vyombo vya dola kama polisi ili ampeleke mahakamani. DPP analifanyia kazi na tumeishakaa na DPP juu ya hili shauri.
“Tunasubiri hatua za DPP. DPP ana taratibu zake na anaweza kufanya uchunguzi kabla ya kuchukua hatua. Sasa fuatilia kwa DPP ‘unless’ DPP aamue kuwa hana nia ‘but’ itakuwa fundisho,” alisema Kaguo.