Thursday, March 13, 2025
spot_img

NANI MHUJUMU SEKTA YA UTALII TANZANIA? (1)

 

Jaji Frederick Werema

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

NANI anaihujumu Sekta ya Utalii Tanzana? Hili ni swali ambalo Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza kiongozi mwandamizi wa serikali, wanasheria nguli na wafanyabiashara wakubwa waliopewa dhamana ya kuendesha hotel za kitalii zenye hadhi ya nyota tano pasipo kupatiwa majibu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Kiongozi mwandamizi wa serikali aliyeulizwa swali hili amefumba mdomo na hata alipoandikiwa maswali kwa maandishi, ni kama aliweka kalamu yake chini asiandike chochote kujibu.

Wanasheria walioulizwa wamekuwa wakirushiana mpira na kuwa na ndimu zinazopishana. Kwanza wakiahidi kulizungumzia, baadaye kidogo wakikataa kwamba wao siyo wazungumzaji, wengine walikanusha kata kata kujua lolote lakini baadaye wakakiri kuwa wanajua ila hawawezi kusema kwa sababu wamefungwa midomo.

Lakini cha kushangaza zaidi wapo wanaohakikisha kuwa wanaodaiwa kuhusika na uhujumu wa sekta ya utalii hapa nchini hawafikiwi kwa namna yoyote ile kuzungumza.

Wanatoa sababu tofauti tofauti; mosi, wanadai watuhumiwa hao wapo nje ya nchi hivyo hawapatikanai kabisa, pili, watuhumiwa hao hawataki kabisa kuzungumzia jambo hilo; tatu, jambo hilo lipo serikalini hivyo wenye dhamana ya kulizungumzia ni viongiozi wa serikali; na nne, anayewatafuta akapekue taarifa zao Brela.

Tanzania PANORAMA Blog iliuliza swali hili baada ya kuvuja kwa taarifa zilizodai kuwa Kampuni ya Hotel and Lodgers, inayojihusisha na biashara ya uendeshaji wa hotel za kitalii kwa miaka mingi imeshindwa kuziendesha kwa kiwango cha kimataifa hotel nne za kitalii zenye hadhi ya nyota tano zilizopo hapa nchini.

Hotel hizo zinatajwa kuwa ni Manyara, Lobo, Soronera na Ngorongoro zilizoko ndani ya hifadhi za taifa.

Kwa mujibu wa taarifa, hotel hizo ziligunduliwa kuwa kwenye hali mbaya kutokana na kutofanyiwa ukarabati na mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tano ambaye alizitembelea na kukuta baadhi zinavuja kwenye paa na baadhi ya vyumba vya wateja, maji ya kuoga na kunawa uso yalikuwa yanachotwa nje kwenye ndoo na kupelekwa vyumbani.

Taarifa zilieleza kuwa kiongozi huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa alisikitishwa na hali mbaya ya hoteli hizo na aliwasilisha serikalini taarifa ya jinsi zilivyochakaa kiasi cha kuvuja kwenye paa na maji ya kuoga na kunawa uso kuchotwa nje kwa ndoo kisha kupelekwa vyumbani.

Taarifa ya kiongozi huyo iliishtua serikali ambayo iliunda tume ya kwenda kuzikagua ili baadaye ishauri hatua za kuchukua lengo likiwa kuzinusuru na uchakavu zilizokuwa nao.

Hoteli ya kitalii ya Lobo yenye hadhi ya nyota tano
 

Kwamba uamuzi huo pia ulilenga kuzinusuru kukosa wateja (watalii) na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na biashara ya utalii.

Inadaiwa kuwa tume iliyoundwa ilikuwa chini ya mhifadhi anayetajwa kwa jina moja la Banga lakini kabla haijaanza kazi, mmoja wa viongozi waandamizi wa serikali alikutana kwa faragha na mwakilishi wa hoteli hizo aliyekuwa ameteuliwa kuwemo kwenye tume hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa tume baada ya kufanya ukaguzi na kubaini hali ya uchakavu wa hoteli hizo, pia ilibaini kuwa menejimenti inayoziendesha iko nchi jirani ya Kenya ambayo ni washindani wakubwa wa biashara ya utalii wa Tanzania.

Kwamba tume iliandaa ripoti yake na kuikabidhi serikalini ikiwa imependekeza Kampuni ya Hotel and Lodgers kunyang’anywa uendeshaji wa hoteli hizo.

Hata hivyo uamuzi uliofikiwa ni kuipa muda wa siku 90 Kampuni ya Hotel and Lodgers kuzifanyia matengenezo na menejimenti inayoziendesha ihamishiwe mkoani Arusha kutoka Nairobi Kenya iliko sasa.

Tanzania PANORAMA Blog imeelezwa kuwa kampuni hiyo ilishindwa kufanya ukarabati uliotakuwa ndani ya muda hivyo iliomba muda zaidi, ikaongezewa mwaka mmoja ambao nao uliisha huku ukarabati huo ukiwa haujakamilika kama ilivyotakiwa na pia menejimenti inayoziendesha ikiwa haijahamishwa kutoka Nairobi Kenya kuja Arusha kama ilivyoelekezwa.

Kwa kutambua unyeti wa suala hilo, hasa jitihada za serikali kukuza sekta ya utalii ili iweze kuchangia ipasavyo uchumi wa taifa. Na pia Tanzania PANORAMA Blog ikitambua kuwa menejimenti inayoendesha hoteli hizo haipo hapa nchini, iliharakisha kumtafuta mwnasheria wsa Kampuni ya Hotel and Lodgers ambaye alitajwa pia kama msemaji, Ahmad El Maamry ili kulizungumzia hilo.

Katika majibu yeke alisema ni kweli hapo awali alikuwa mwanasheria na msemaji wa Kampuni ya Hotel and Lodgers lakini nafasi hiyo alikwishanyang’anywa na kupewa Jaji Frederick Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani.

“Brother nimekusikia, nimekusikia sana na umenitisha sana maana inaonekana umechimba sana, yaani umejiandaa. Lakini nataka nikwambie tu mimi kwa sasa siyo msemaji tena wala siyo mwanasheria wa kampuni hiyo, kwa sasa matajiri wamempa majukumu hayo Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali, Jaji Frederick Werema. Sasa kama unamuweza huyo, ndiyo kamuulize sasa, eeeeh, Jaji Werema. Mimi nimebaki kama company secretarytu.

“Ila mimi sifahamu chochote kabisa kuhusu hiyo tume wala kama walipewa muda wa kuzikarabati maana ninavyojua zilikuwa zinafanya kazi vizuri tu. Muda wote niliokuwa nao karibu sikuwahi kukanyaga kwenye hizo hoteli ila najua kweli ni zao na hiyo tume unayosema mimi nilikuwa mmoja wa wajumbe, hivi mimi naingiaje kwenye hiyo tume na nani ananiteua, sijawahi kuwa mjumbe wa tume nikaenda kwenye hoteli hizo,” alisema El Maamry.

Tanzania PANORAMA Blog ilifunga safari hadi zilipo ofisi za Jaji Werema katika jengo la Haidery Plaza, eneo la posta mpya, Dar es Salaam ambapo awali ilikataliwa kuonana naye kwa maelezo kuwa wageni wake huomba miadi ya kukutana naye mapema na huwekwa kwenye rejista kupangiwa siku na muda wa kuonana naye.

Lakini baada ya utambulisho na kueleza sababu ya kumfuata haraka ofisini kwake, wafanyakazi wa mapokezi walikubali kuikaribisha Tanzania PANORAMA Blog kwenye viti kisha wakawasiliana naye kwa simu.

Baada ya mawasiliano walisema Jaji Werema ameagiza Tanzania PANORAMA Blog iache namba zake za simu na yeye ataipigia baadaye, jambo ambalo hakulitekeleza licha ya kuachiwa namba za simu kama alivyotaka. Alikaa kimya.

Baada ya ukimya huo, Oktoba 8, 2021 Tanzania PANORAMA Blog ilimwandikia Jaji Werema maswali haya.

Jaji Frederick Werema

 

Mosi; Kampuni ya Hotel and Lodgers pamoja na kufanya biashara nyingine imekabidhiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuendesha hotel zake tatu ambazo ni Manyara, Lobo na Soronera pamoja na Ngorongoro Wild Life inayomilikiwa na NCAA. Imeelezwa kuwa mwanasheria wa kampuni hii ni wewe Jaji Werema, naomba kufahamu kutoka kwako mwenyewe kama kweli wewe ni mwanasheria wa kampuni hii? B) Umeanza lini kuisimamia kisheria?

Pili; Kampuni ya Hotel and Lodgers imetajwa kuwa moja kati ya makampuni yanayojihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi kwa kuikosesha serikali mapato ya fedha za kigeni baada ya kubainika kuziua kibiashara kwa kutozifanyia matengenezo na kutoa huduma zisizokidhi viwango vya biashara kwa hotel za kitalii ilizokabidhiwa kuziendesha na TANAPA na NCAA. Jambo hili unalizungumzije?

Tatu; Kampuni ya Hotel and Lodgers imeajiri menejimenti ya kigeni kutoka taifa jirani la Kenya ambalo ni washindani wakubwa wa biashara ya utalii na Tanzania na zipo taarifa kuwa menejimenti hiyo ya kigeni ni mhusika mkuu wa kuhujumu hotel hizo. A) wewe kama mwanasheria wa kampuni hiyo unafahamu kuwa menejimenti ya hotel hizo ni ya kigeni? B) Je, imekuwa ikitekeleza wajibu wake sawasawa? C) Ni nini mtizamo wako  kuhusu jambo hili kisheria na kwa sekta ya utalii Tanzania?

Nne; Ofisi za menejimenti inayoendesha hoteli hizi ipo Kenya na si Tanzania. Kwa faida ya wasomaji wa magazine ya PANORAMA na Blog ya PANORAMA na watanzania wote, naomba kujua ni kwanini ofisi za menejimenti inayoendesha hoteli hizi ipo nchini Kenya.

Tano; Mwezi Mei, mwaka jana iliundwa tume ya kuchunguza matatizo ya hoteli hizo baada ya kubainika kuwa zipo kwenye hali mbaya na watalii wanazikimbia. Tume hiyo ilibaini upungufu mwingi kwenye hotel hizo na baada ya kuwasilisha katika mamlaka za serikali, Kampuni ya Hotel ya Lodgers iliagizwa kuzifanyia ukarabati ndani ya siku 90, A) Jambo hili unalifahamu? B) Maelekezo hayo mahususi ya serikali yalitekelezwa kwa kiwango gani?

Sita; Serikali ilitoa muda zaidi hadi kuwa mwaka mmoja kwa Kampuni ya Hotel and Lodgers kukarabati hotel hizo. Jambo hili unalifahamu na maelekezo hayo ya serikali yalitekelezwa kwa kiwango gani?

Sita; PANORAMA Magazine na Tanzania PANORAMA Blog zina taarifa kuwa hadi sasa Kampuni ya Hotel and Lodgers imekaidi maelekezo ya serikali ya kuzikarabati hoteli hizo kwa kiwango cha kuzirejesha kwenye ubora wake wa awali wa kuhudumia watalii. Je ni kwanini imekaidi?

Nane; Septemba 22, 2021, Kampuni ya Hotel and Lodgers imenyang’anywa Hotel ya Ngorongoro Wild Life inayomilikiwa na NCAA kwa kukaidi maelekezo ya serikali ya kuikarabati hotel hiyo. Hili unalifahamu? Na unalizungumziaje?

Kenda; Kampuni hii pia imenyang’anywa hotel mbili za kitalii zilizoko Zanzibar baada ya kubainika kushindwa kuziendesha pamoja na kubainika kujihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi wa Zanzibar. Hili unalifahamu? Na unalizungumziaje?

Kumi; Watanzania wengi wamekosa ajira katika hoteli hizo kutokana na kuwa chini ya menejimenti ya kigeni na inayoendesha hoteli hizo kutoka nje ya nchi. Wewe ukiwa mmoja wa viongozin wanaoheshimika hapa nchini uliyepata kuwa na jukumu zito la uanasheria mkuu wa serikali, una kauli gani kuhusu hili?

Naomba ushurikiano wako.

Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia maswali hayo Jaji Werema kwa whatsapp na aliyasoma lakini alibaki kimya hivyo iliendelea kumtafuta kwa simu yake ya kiganjani hadi ilipofanikiwa kumpata.

Alipoelezwa kuwa kuna maswali alitumiwa na yanaonyesha aliyapata na kuyasoma lakini hajajibu alisema ni kweli aliyapata lakini ndiyo kwanza anashuka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, hivyo apewe muda afike nyumbani kwake apumzike, ndiyo ayajibu.

RIPOTI HII INAENDELEA     

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya