Thursday, March 13, 2025
spot_img

DPP AFUATILIA FAILI LA MTUHUMIWA WA ULANGUZI WA UMEME

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema anafuatilia faili la shauri la mfanyabiashara, Ugur Gurses ambalo ndani yake kuna tuhuma za kufanya biashara ya umeme kinyume cha sheria bila kuwa na leseni ya EWURA na kuuuza kwa bei ya juu.

DPP Mwakitalu amesema faili hilo halijafika mezani kwake na inawezekana liliwasilishwa katika ofisi ya kanda lakini aliahidi kuwa analifuatilia.

Alisema Tanzania PANORAMA Blog inaweza pia kuwasiliana na Ofisi ya Kanda ya Mkurugenzi wa Mashtaka kujua kama faili hilo lilipokelewa huko na namna lilivyofanyiwa kazi.

“Faili la shauri hilo halijafika ofisini kwangu, inawezekana EWURA waliwasilisha katika ofisi za kanda, haya mambo mengine yafanyika huko ofisi za kanda lakini nakushukuru umeniambia, nalifuatilia,” alisema DPP Mwakitalu

Mfanyabiashara Ugur Gurses anayetuhumiwa kulangua umeme na kukaidi maelekezo ya EWURA

 

Kauli hii ya DPP Mwakitalu imekuja baada ta Meneja Mwasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo kueleza kuwa mamlaka yake imewasilisha kwa DPP tuhuma zinazomuhusu mfanyabiashara Gurses za kufanya biashara ya umeme kinyume cha sheria akiwa hana leseni ya mamlaka hiyo na kuuuza kwa bei ya juu.

Kaguo aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumzia hatua zilizochukuliwa na mamlaka yake dhidi ya Gurses anayedaiwa kukiuka sheria za nchi na kukaidi maelekezo ya EWURA.

Gurses, raia wa Uturuki ambaye ni mmiliki Kampuni ya Adamas Group yenye ofisi zake Karioakoo, Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya nyumba anadaiwa kufanya biashara ya kuuza umeme wa Tanesco kwa bei ya ulanguzi tangu mwaka 2016.

Mfanyabiashara Akif Kara anayetuhumiwa kulangua umeme

 

Pamoja naye, mfanyabiashara mwenzake, Akif Kara ambaye ni mmiliki mwenza wa jengo hilo naye anatuhumiwa kutenda makosa hayo lakini mwanasheria na msemaji wake, Albert Kimaro, juzi aliiambia Tanzania PANORAMA kuwa ni kweli Kara alikuwa akijihusisha na vitendo hivyo lakini amemshauri afuate sheria na maelekezo ya EWURA.

Kwa mujibu wa Kimaro, Kara ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Mar Kim Chemicals amekubali kufuata maelekezo ya EWURA na kwamba bei ya umeme watakayokuwa wanalipa wakazi wanaoishi katika jengo lake itakuwa sh. 292 ambayo ndiyo bei elekezi ya EWURA.

Awali Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa wapangaji na walionua nyumba za Gurses na Kara wanawauzua kimabavu umeme kwa kutumia mita za Bahdela kwa bei la ulanguzi.

Kwamba Gurses anauza uniti moja ya umeme kutoka kwenye mita za Bahdela kwa shilingi 650 na mkazi anayekataa kununua kwa bei hiyo humkatia umeme.

Tanzania PANORAMA inaripoti kwa uhakika kuwa Gurses ambaye alifikiwa na EWURA na kutakiwa kuacha kulangua umeme kwa sababu kitendo hicho ni kukiuka sheria, alikataa maelekezo hayo na inadaiwa kuwa sasa anajigamba kuwa EWURA ameikamata mkononi ndiyo maana aliwafukuza maafisa wadogo wa mamlaka hiyo waliokwenda kumtaka aache ulanguzi wa umeme na amekuwa akienda mbali zaidi kwa kudai kuwa yeye ni mwekezaji na ‘mama’ amekwishaagiza wawekezaji wasiguswe kwa lolote kwa sababu anawahitaji sana.

Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo

 

Akizungumzia tuhuma hizo, Kaguo alisema Gurses ana makosa mawili, la kwanza ni kuuza umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kosa la pili ni kuuza umeme kwa bei ya juu.

Alisema EWURA baada ya kubaini makosa hayo kwa Gurses ilimpelekea karipio la kisheria lakini alikataa kulipokea hivyo imelifikisha shauri hilo kwa DPP ambaye ana nguvu za kisheria na pia ana vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

“Huyu mtu ana makosa yafuatayo, 1) kuuza umeme wakati hana leseni ya EWURA, 2) kuuza umeme kwa bei ya juu. Tulimpelekea ‘complaince order’ karipio la kisheria na alikataa kupokea.

“Katika hali kama hii, sheria inatutaka tumpelekee DPP ambaye ana vyombo vya dola kama polisi ili ampeleke mahakamani. DPP analifanyia kazi na tumeishakaa na DPP juu ya hili shauri.

“Tunasubiri hatua za DPP. DPP ana taratibu zake na anaweza kufanya uchunguzi kabla ya kuchukua hatua. Sasa fuatilia kwa DPP ‘unless’ DPP aamue kuwa hana nia ‘but’ itakuwa fundisho,” alisema Kaguo.

Gurses amemkatia umeme Salem Balleith ambaye amenunua ghorofa moja katika jengo lake hilo baada ya kutaka kuanza kununua umeme wa Tanesco na kukataa kutumia mita za Bahdela pamoja na kupinga kutozwa Dola za Marekani 100 kila mwezi kama kodi ya huduma wakati hakuna haduma inayotolewa.

Balleith mwenyewe ambaye alizungumza na Tanzania PANORAMA akiwa nje ya nchi alithibitisha kukatiwa umeme na kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa sehemu aliyonunua imekaa kama gofu kwa sababu hawezi kuishi yeye mwenyewe wala kuipangisha kutokana na kutokuwa na umeme.

Uchunguzi wa nyaraka za mgogoro huo umeonyesha kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa EWURA imekuwa ikihangaika kuutatua pasipo mafanikio.

Jengo linalomilikiwa na Ugur Gurses na Akif Kara ambalo wakazi wake wanamalalamika kulanguliwa umeme

 

Moja ya nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA imeziona ikiwa imesainiwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki wa EWURA, Mhandisi Nyirabu Musira ya Septemba 2, 2020 na yenye kumbukumbu namba SN. 71/135/95/2 ikiwa na kichwa cha habari, malalamiko dhidi ya Ugur Gurses na Tanesco inasomeka;

‘Rejea kichwa cha habari hapo juu na malalamiko yako ya terehe 31, Agosti 2020. Mamlaka inakiri kupokea malalamiko yako ya tarehe 31, Agosti 2020 na ya kwamba tunayafanyia kazi. Tutakupatia taarifa katika kila hatua inayofuata katika shauri lako.’

Nyaraka nyingine ambayo ni fomu ya malalamiko iliyotolewa na EWURA iliyojazwa na Haykal Hassan na kupokelewa na kugongwa muhuri katika Ofisi ya Kanda ya Mashariki Machi 2, 2020, mlalamikaji ameandika.

‘Tuna majonzi tele kwa ufanyaji kazi wa EWURA katika kutekelezsa kero yetu. Tulilalamika kuhusu kuuziwa umeme kwa unit 650 shilingi.

‘Tuna miaka kama mitano tunalipa umeme kwa kwa bei ya unit kwa 650 na sasa tumepunguziwa kwa unit moja kwa bei ya shilingi 500 ambayo bado ni kubwa. Kila tukifuatilia kwa EWURA tukufu hatusaidiwi sijui tatizo liko wapi kwani ni tatizo rahisi ambalo EWURA wanaweza kulimaliza haraka na sisi kupata haki sawa kwani sisi ni watanzania.’

Kwa mujibu wa EWURA, iliruhusu watu wenye nyumba kubwa zilizopangishwa watu wengi kutumia mita ndogo (sub meters) na mita kubwa ya Tanesco inawekwa mahali unapoingilia umeme.

“EWURA iliruhusu watu wenye majumba makubwa ambao wamepanga na wapangaji au wakazi wengi kutumia sub meters kwa maana kwamba mita ya Tanesco kuwekwa pale unapoingilia umeme ambao kimsingi mara nyingi unakuwa umenunuliwa in bulk (kwa jumla).

“Lakini gharama ya umeme haitakiwi kuzidi shilingi 292 kwa unit kwa T1 ambao unatumika majumbani. ‘Therefore, Bahdela anatakiwa kutoza sh 292 kwa unit ambayo ilipitishwa na EWURA kwa matumizi ya majumbani.

“Kama sivyo watu wanatakiwa kuleta malalamiko katika ofisi zetu za kanda ya mashariki. Kijitonyama PSSSF ghorofa ya saba,’ alisema Kaguo.

Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kufuatilia sakata hili.    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya