![]() |
Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewasilisha kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) tuhuma za kufanya biashara ya umeme kinyume cha sheria na kuuuza kwa bei ya juu zinazomkabili mfanyabishara Ugur Gurses
Hayo yamesemwa jana na Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo alipokuwa akizungumzia hatua zilizochukuliwa na mamlaka hiyo dhidi ya Gurses ambaye anadaiwa kukiuka sheria za nchi na kukaidi maelekezo ya EWURA.
Gurses, raia wa Uturuki ambaye ni mmiliki Kampuni ya Adamas Group yenye ofisi zake Karioakoo, Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya nyumba anadaiwa kufanya biashara ya kuuza umeme wa Tanesco kwa bei ya ulanguzi tangu mwaka 2016.
Walalamikaji, Haykal Hassan na Salem Balleith, wanadai kuwa Gurses ambaye ni mmoja wa wamiliki wa jengo lenye ghorofa 13 lililopo mtaa wa Livingstone, aliwauzia ghorofa moja kila mmoja katika jengo hilo lakini amewazui kimabavu kutumia umeme unaosambazwa na Tanesco na badala yake anawauzia umeme kwa kutumia mita za Bahdela kwa bei la juu .
Kwamba Gurses anauza unit moja ya umeme kutoka kwenye mita za Bahdela kwa shilingi 650 na mkazi anayekataa kununua kwa bei hiyo humkatia umeme. Pia wanamlalamikia kuwatoza Dola za Marekani 100 kama kodi ya huduma kila mwezi wakati hakuna huduma anayotoa iliyolingana na kiasi hicho na kwamba jenerata lililopo kwenye jengo limeharibika kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Tanzania PANORAMA inaripoti kwa uhakika kuwa Gurses ambaye alifikiwa na EWURA na kutakiwa kuacha kulangua umeme kwa sababu kitendo hicho ni kukiuka sheria, alikataa maelekezo hayo na inadaiwa kuwa sasa anajigamba kuwa EWURA ameikamata mkononi ndiyo maana aliwafukuza maafisa wadogo wa mamlaka hiyo waliokwenda kumtaka aache ulanguzi wa umeme na amekuwa akienda mbali zaidi kwa kudai kuwa yeye ni mwekezaji na ‘mama’ amekwishaagiza wawekezaji wasiguswe kwa lolote kwa sababu anawahitaji sana.
Akizungumzia tuhuma hizo, Kaguo alisema Gurses ana makosa mawili, la kwanza ni kuuza umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kosa la pili ni kuuza umeme kwa bei ya juu.
![]() |
Jengo la Ugur Gurses ambalo wakazi wake wanalanguliwa umeme |
Alisema EWURA baada ya kubaini makosa hayo kwa Gurses ilimpelekea karipio la kisheria lakini alikataa kulipokea hivyo imelifikisha shauri hilo kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali ambaye ana nguvu za kisheria na pia ana vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
“Huyu mtu ana makosa yafuatayo, 1) kuuza umeme wakati hana leseni ya EWURA, 2) kuuza umeme kwa bei ya juu. Tulimpelekea ‘complaince order’ karipio la kisheria na alikataa kupokea.
“Katika hali kama hii, sheria inatutaka tumpelekee DPP ambaye ana vyombo vya dola kama polisi ili ampeleke mahakamani. DPP analifanyia kazi na tumeishakaa na DPP juu ya hili shauri.
“Tunasubiri hatua za DPP. DPP ana taratibu zake na anaweza kufanya uchunguzi kabla ya kuchukua hatua. Sasa fuatilia kwa DPP ‘unless’ DPP aamue kuwa hana nia ‘but’ itakuwa fundisho,” alisema Kaguo.
Hata hivyo, mlalamikaji Haykal Hassan Alwan anasema kuwa malalamiko yao ni ya muda mrefu lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa huku wakizidi kuumia kwa kukamuliwa pesa nyingi na kwamba mgogoro huo sasa unaelekea kwenye hatua mbaya kutokana na vitendo vya kibabe vya Gurses.
Anasema Gurses amemkatia umeme Salem Balleith ambaye amenunua ghorofa moja katika jengo lake hilo baada ya kutaka kuanza kununua umeme wa Tanesco na kukataa kutumia mita za Bahdela pamoja na kupinga kutozwa Dola za Marekani 100 kila mwezi kama kodi ya huduma wakati hakuna haduma inayotolewa.
Balleith mwenyewe ambaye alizungumza na Tanzania PANORAMA akiwa nje ya nchi alithibitisha kukatiwa umeme na kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa sehemu aliyonunua imekaa kama gofu kwa sababu hawezi kuishi yeye mwenyewe wala kuipangisha kutokana na kutokuwa na umeme.
Uchunguzi wa nyaraka za mgogoro huo umeonyesha kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa EWURA imekuwa ikihangaika kuutatua pasipo mafanikio.
Moja ya nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA imeziona ikiwa imesainiwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki wa EWURA, Mhandisi Nyirabu Musira ya Septemba 2, 2020 na yenye kumbukumbu namba SN. 71/135/95/2 ikiwa na kichwa cha habari, malalamiko dhidi ya Ugur Gurses na Tanesco inasomeka;
‘Rejea kichwa cha habari hapo juu na malalamiko yako ya terehe 31, Agosti 2020. Mamlaka inakiri kupokea malalamiko yako ya tarehe 31, Agosti 2020 na ya kwamba tunayafanyia kazi. Tutakupatia taarifa katika kila hatua inayofuata katika shauri lako.’
Nyaraka nyingine ambayo ni fomu ya malalamiko iliyotolewa na EWURA iliyojazwa na Haykal Hassan na kupokelewa na kugongwa muhuri katika Ofisi ya Kanda ya Mashariki Machi 2, 2020, mlalamikaji ameandika.
‘Tuna majonzi tele kwa ufanyaji kazi wa EWURA katika kutekelezsa kero yetu. Tulilalamika kuhusu kuuziwa umeme kwa unit 650 shilingi.
‘Tuna miaka kama mitano tunalipa umeme kwa kwa bei ya unit kwa 650 na sasa tumepunguziwa kwa unit moja kwa kwa bei ya shilingi 500 ambayo bado ni kubwa. Kila tukifuatilia kwa EWURA tukufu hatusaidiwi sijui tatizo liko wapi kwani ni tatizo rahisi ambalo EWURA wanaweza kulimaliza haraka na sisi kupata haki sawa kwani sisi ni watanzania.’
Kwa mujibu wa EWURA, iliruhusu watu wenye nyumba kubwa zilizopangishwa watu wengi kutumia mita ndogo (sub meters) na mita kubwa ya Tanesco inawekwa mahali unapoingilia umeme.
“EWURA iliruhusu watu wa majumba makubwa ambao wamepanga wengi kutumia sub meters kwa maana kwamba mita ya Tanesco inawekwa pale unapoingilia umeme ambao kimsingi mara nyingi unakuwa umenunuliwa in bulk (kwa jumla).
“Lakini gharama ya umeme haitakiwi kuzidi shilingi 292 kwa unit kwa T1 ambao unatumika majumbani. ‘Therefore, Bahdela anatakiwa kutoza sh 292 kwa unit ambayo ilipitishwa na EWURA kwa matumizi ya majumbani.
“Kama sivyo watu wanatakiwa kuleta malalamiko katika ofisi zetu za Kanda ya Mashariki. Kijitonyama PSSSF ghorofa ya saba,’ alisema Kaguo.
Kwa upande wao Bagdela ambao wametoa kauli kuhusiana na mgogoro huo ambao wanahusishwa kwa mita zao kuuza umeme kwa bei kubwa wamefanya mahojiano na Tanzania PANORAMA blog ambayo yatariporiwa kesho.
Jitihaza za kumtafuta DPP kuzungumzia kadhia hii hazikuzaa matunda lakini Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kumtafuta na aidha, Waziri wa Nishati, Januari Makamba na Waziri wa Uwekezaji, Kitila Mkumbo ambao wizara zao zinasimamia sekta za nishati na uwekezaji nao hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hili.