![]() |
Laizer Marko na mkewe Pamela Kayira siku ya ndoa yao |
*Ni Laizer Marko anayehofia usalama wa maisha yake ndani ya ndoa, bosi Mamlaka ya Chakula na Lishe aficha siri
*Aomba huruma ya mkware anayevuruga familia yake, azungumzia uraia wa mkewe na shemeji yake
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
SAKATA la wivu na usaliti wa mapenzi ndani ya ndoa linatishia uhai wa ndoa ya wanandoa Laizer Marko na Pamela Kayira na linawanyima watoto wao haki ya malezi bora.
Tanzania PANORAMA Blog katika sehemu yake ya kwanza ya makala maalumu ya sakata hili, iliripoti kuwa tuhuma za usaliti wa mapenzi ndani ndoa hiyo zimeibua hofu na wasiwasi katika familia ya Marko na Pamela ambao ni wakazi wa Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam.
Marko, mume wa Pamela ndiye anayefichua kuwepo kwa hali ya hofu na wasiwasi ndani familia yake katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine anamtuhumu mkewe kuwa chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo kutokana na vitendo vyake vya kusaliti penzi lao na kuwatelekeza watoto wake.
Katika mahojiano hayo, Marko anamtuhumu Pamela kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanamume mwingine, kuipa kisogo familia yake, (mumewe Marko na watoto wao watatu), kuwa na kiburi na jeuri, kuondoka nyumbani asubuhi kwenda kazini na kurudi asubuhi ya siku inayofuata akiwa hajulikana alikolala huku akijua kuwa uraia wake pamoja na wa dada yake ni wa mashaka pamoja na kuhama nyumbani kwake kwa muda wa miezi sita kwenda kuishi mahali kusikojulikana.
Marko anasema amemgundua mkware mwenye uhusiano wa kimapenzi na mkewe na anamuomba amuonee huruma kwa sababu kitendo anachokifanya kina athari mbaya katika maisha ya watoto wake na kinaiharibu familia yake. Pia anamuomba mwajiri wa mkewe asaidie kuokoa ndoa yake na watoto kupata mapenzi na malezi ya mama yao.
Kwa upande wake Pamela, anazipuuza tuhuma hizo. Katika mahojiano aliyofanya na Tanzania PANORAMA Blog, Pamela anakataa kutoa ushirikiano na anaikana ofisi anayofanyia kazi.
Wakati Pamela anapuuza tuhuma na kilio cha mumewe, bosi wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk. Germana Henry Leyna naye anakataa kuthibitisha kama Pamela ni mfanyakazi wa taasisi anayoiongoza au lah na anajiweka mbali na ombi la Marko la kumkalisha kitako Pamela kumsihi kuijali familia yake na hasa kulea watoto wake.
Tanzania PANORANA Blog ambayo imefuatilia mkasa huu kwa kina imeandaa makala maalumu ikianza na mahoajino iliyoyafanya na Marko anayeeleza kinaga ubaga historia ya maisha baina yake na mkewe, mateso anayoyapata ndani ya ndoa, hofu aliyonayo kuhusu maisha yake na watoto na wasiwasi wa nyendo na uraia wa mkewe pamoja na dada yake. Hii ni sehemu ya pili ya makala hiyo.
Marko anasema hivi karibuni, mwezi wa saba au wa nane ndipo mkewe Pamela amerudi nyumbani kutoka alikokuwa amekwenda na kuiacha familia yake.
Anasema, “Mwezi wa saba au wa nane akawa amerudi, akawa amekuja na mabegi yake, akanikuta nimekaa sebuleni lakini yale mabegi akawa ameyaficha kwenye maua ili asifahamike kuwa amerudi. Kwa hiyo hatuna mazungumzo naye. Tunaishi kihatari hatari tu, hatari mno.
“Tuna mfanyakazi ambaye huwa anatusaidia siku za jumatatu mpaka ijumaa. Ni mke wa mtu. Anatusaidia mpaka saa 10 hivi au saa 11 hivi jioni, anarudi nyumbani.
“Siku za jumamosi na jumapili huwa haji. Siku za jumamosi na jumapili mimi ndiyo napika, siku zote. Mke wangu Pamela hafanyi lolote, hagusi chochote na alishawaambia mpaka na watoto kwamba hatanunua chochote nyumbani wala hatafanya chochote.”
Alipulizwa kuhusu maendeleo ya watoto wake katika masomo na hisia wanazoonekana kuwa nazo mama yao anapokuwa hayupo nyumbani, Marko anasema, “Tumezaa naye watoto watatu, mmoja yuko form three, mwingine ndiyo kamaliza darasa la saba na mwingine ndiyo huyu mdogo.
“Tena huyu mdogo alishawahi kumsafirisha kama kifurushi, kutoka huko anakokaa akamleta. Akampakia kwenye bajaji kama kifurushi, akamleta. Yaani badala ya kuja naye akampakia tu kwenye bajaji kama mzigo akaletwa.
“Kwa hiyo tuna watoto watatu. Huyo mtoto mdogo ndiyo anaumia sana, hawa wengine wakubwa wameishazoea hizi hulka za mama yao. Wanaumia ndiyo lakini wamezoea kwa sababu labda ni wazima kidogo.
“Lakini huyo mdogo kuna saa analia mama hayupo zaidi ya miezi sita. Amemtekeleza ameniachia nateseka naye yeye ameenda huko kwenye vituko vyake.”
Kuhusu kuripoti mwenendo huo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama au Serikali ya Mtaa anasema, “Taarifa hii niliipeleka kwa wazazi wa pande zote. Kwa upande wa kwangu na upande wa kwake na wasimamizi wa ndoa. Huko ndiko nilikopeleka. Niliona mambo mengine ya kwenda polisi pengine ni kama udhalilishaji.”
Marko anasema analo ombi kuwa, kama kuna sheria yoyote au mamlaka yoyote au chombo chochote kinachoweza kurekebisha mwenendo wa mambo katika ndoa yake, kichukue hatua.
Anasema chombo hicho kichukue jukumu la kumlazimisha mkewe kufuata sheria za ndoa ambazo aliapa kuzifuata lakini vile vile sheria za utumishi wa umma nazo kama zina nafasi ya kuokoa ndoa za wafanyakazi wake na kusaidia watoto kupata haki ya malezi ya mama nazo zichukue mkondo wake.
“Kwa haya yanayonikuta, haya magumu wanayopitia watoto wangu, watu wataogopa kuoa watumishi wa umma kwa sababu watajua wakishawapeleka watumishi wa umma nyumbani wanakuwaga hivi na hivi na hivi.
“Hivyo serikali labda kwa upande wake, kama inaweza ifanyie kazi mateso yangu haya na wanangu. Lakini kwa mamlaka zinazohusika na sheria nazo zifanyie kazi jambo hili ili walau liwe fundisho kwa watu wengine.
“Mke wangu Pamela anafanya kazi Ocean Road, kwenye Taasisi ya Chakula na Lishe. Sasa nimuombe bosi wake, namjua, anayajua mateso yangu ndani ya ndoa kwa sababu nilishayafikisha kwake, anayajua mateso ya watoto malaika hawa. Na yeye ni mwanamke, ana mume na watoto naamini hivyo, asaidie hasa hawa watoto.
“Maana hawa watoto wanateseka sana. Pamela ni mwanamke mwenzie, ni kiongozi wake, anaweza kumkalisha chini akamuasa arejee kwenye maadili mema, akae nyumbani alee watoto kwa sababu wanamuhitaji sana na wanaumia sana anapokuwa hayupo.
“Lakini pia huyu bwana anayemchukua mke wangu. Yeye ni mwanamume kama mimi na anajua kuwa anayemlaza nje na kumzurulisha huko usiku kucha ni mke wa mtu na ana watoto wadogo wanaohitaji malezi ya mama yao.
“Namuomba kwanza awaonee huruma watoto hawa, ni malaika, naamini yeye alilelewa vizuri na wazazi wake wote wawili, baba na mama ndiyo maana kapata kazi hadi kumrubuni mke wangu ambaye sasa pesa zake haleti nyumbani kusaidia watoto wetu anazipeeka kwake kustarehe. Hawa watoto wanapata shida sana anapokuwa anamchukua mama yao na kumlaza nje huko anamrudisha asubuhi anapishana nao wanakwenda shule na wakati mwingine anamchukua kabisa siku nyingi tu hamrudishi.
“Lakini pia na mimi hanitendei haki kabisa, anaiua ndoa yangu. Wakubwa zake kazini kama bado ni kijana mdogo nawaomba wakae naye wamwambie hiki anachokifanya siyo kitu kizuri kwa sababu kunaweza kuhatarisha maisha ya mtu.
“Lakini kingine, kuna dada yake ndiye anayemchochea. Kuna dada yake ambaye anafanya kazi taasisi ya (anaitaja jina). Anaitwa (anaitaja jina).
“Huyu dada yake anajua kabisa hapa kuna watoto ambao wanahitaji malezi ya mama yao lakini ndiyo anamchochea waende kuzurura. Yaani huyo ndiye kiongozi wake katika haya mambo yasiyofaa.
“Anajua kabisa kuwa hii dunia imeharibika na wao hawana ndugu wa damu hapa isipokuwa hawa ndugu wa hiari tu kwa sababu ni watu kutoka nje, wapo wawili tu huyu mke wangu na huyo dada yake na siyo raia wa hapa. Sasa likitokea la kutoka huko anakokwenda Pamela usiku mimi nitafanya nini jamani.
“Kiukweli naomba msaada ili kunusuru ndoa yangu na maisha ya watoto wangu yasije yakatokea maafa,” anasema.
![]() |
Pamela Kayira |
Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Pamela na kumuuliza kuhusu malalamiko na tuhuma anazoelekezewa na mumewe wake. Naye kwa maneno yake mwenyewe anasema.
“Hivi mnanifuata fuata kwa nini nyie watu. Nawapeleka polisi nawaambia. Mtaoza huko. Achaneni na huyo mpuuzi na huo upuuzi wake.”
Tanzania PANORAMA Blog ilimsihi Pamela atulie kwanza kwa sababu tuhuma na malalamiko dhidi yake hayana afya katika ndoa yake na kwa malezi ya watoto wake na kama kuna tatizo kwenye ndoa yake ayaeleze kwa sababu anaweza kupata msaada yakifahamika na pia anao uhuru na haki kwenda polisi au mahakamani iwapo ataona hajatendewa haki kwenye mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog.
Akijibu, alisema. “Upuuzi mtupu, mimi siyo mtumishi wa Taasisi ya Chakula na Lishe aliyowaambia na wala siijui na sifundishwi na mtu maisha. Ole wenu nisikie habari zangu hata punje kwenye hiyo media yenu nawaambia, wote mnaozea jela dakika moja. Achaneni na mimi,” alijibu Pamela kisha akakata simu.
![]() |
Dk. Germana Henry Leyna |
Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi ya Chakula na Lishe, Dk. Germana Henry Leyna naye alitafutwa na kuulizwa kama Pamela ni mtumishi wa taasisi anayoingoza na iwapo, kwa nafasi yake kama kiongozi wa taasisi ya umma na mama anaweza kusaidia kuinusuru ndoa ya Pamela na pia watoto kupata malezi wanayostahili kutoka kwa mama yao alisema yeye hahusiki na mambo binafsi ya watu na wala hawezi kuthibitisha au kukataa kama Pamela ni mfanyakazi wa taasisi ya chakula na lishe.
Tanzania PANORAMA Blog ilimweleza Dk. Leyna kuwa ingawa masuala ya ndoa yanaweza kuchukuliwa kuwa ya binafsi lakini hama sababu ya kuficha siri iwapo Pamela ni mtumishi wa katika taasisi ya Chakula na Lishe kwa sababu suala la malezi ya watoto lina uzito wa kipekee katika jamii na yeye kama kiongozi wa umma na pia mama anao wajibu wa kusaidia walau kwa kutoa ushauri, alisisitiza kuwa hayo ni mambo binafsi ambayo hawezi kuyaingilia hivyo anapaswa kuficha siri.
ITAENDELEA.