Wednesday, June 25, 2025
spot_img

MFANYABIASHARA FIDA HUSSEIN AKIRI KUUZA VIATU 'VIBOVU

Viatu vibovu vinavyouzwa kwenye duka la mfanyabiashara Abbas Fida Hussein, lililopo Mtaa India, Dar es Salaam

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

MFANYABIASHA wa vifaa vya ujenzi, mavazi na viatu vinayotumika migodini na kwenye shughuli za ujenzi, Abbas Fida Hussein wa Dar es Salaam amekiri kuwa anauza viatu vibovu vinavyoingizwa nchini kutoka China

Fida Hussein alikiri hayo jana dukani kwake, Mtaa wa India katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog kwa kueleza kuwa viatu hivyo vilivyoisha muda wake wa matumizi tangu mwaka 2006, anaviuza kwa bei ya chini na hamlazimishi mtu kuvinunua.

Sambamba na hilo, Fida Hussein alikiri kufanya mauzo hayo pasipo kutoa risiti ya aina yoyote kwa kile alichodai kuwa bei anayouza ni ndogo sana ambayo haina haja ya kutoa risiti.

Alisema vifaa vibovu anavyoviuza katika duka lake ni vile vilivyokuwa vimezuiliwa katika kituo cha Polisi Chang’ombe kama ushahidi katika kesi iliyokuwa ikimkabili kwa miaka mingi na baada ya kushinda na kurejeshewa bidhaa zake aliamua kuziuza kwa bei ya chini.

Mahali lilipo duka la  mfanyabiashara Abbas Fida Hussein, Mtaa wa India Dar es Salaam

 


“Mzee ni kweli hivi viatu ni vibovu na vimekwisha muda wake miaka mingi sana. Lakini unajua kwanini mimi naviuza, hivi vimetoka polisi na polisi wanavijua. Vilikuwa polisi Chang’ombe kwa miaka mingi na huko ndiko viliharibika.

“Unajua nini, mimi nilikuwa na kesi kwa miaka mingi sana na bidhaa zangu zilikamatwa na polisi wakaziweka Chang’ombe kama ushahidi. Sasa kesi imekwenda mimi nikashinda lakini vitu vyangu hawakunipa kwa muda, walikaa navyo sana mpaka badaaye ndiyo wakanirudishia. 

“Nilipata hasara sana lakini baada ya polisi kunirudishia, huyu kijana wangu akasena basi aviuze apate shilingi elfu mbili mbili kidogo na elfu mbili bwana pesa kidogo sana huwezi kutoa risiti,” alisema Fida Hussain.

Alipoulizwa haoni ni kosa kuuza vitu vilivyoharibika na vinavyotumika sehemu nyeti kama kwenye kazi za ujenzi na migodini na kwamba kitendo chake hicho kinahatarisha usalama wa watumiaji, alisema yeye hamlazimishi mtu kununua na anajua sheria vizuri ndiyo maana anaviuza kwa sababu hakiuki sheria yoyote

Viatu vibovu vilivyonunuliwa dukani kwa mfanyabiashara Abbas Fida Hussein

 



“Najua sana sheria mimi na ninao mawakili, wanasheria wa kutosha sana na nawalipa vizuri, wananisimamia mimi. Hakuna kosa kuuza mali yako hata kama imeharibika kwa sababu mimi simlazimishi mtu kununua bali wanakuja wenyewe kununua, wanavipenda sana mimi nawafanyia bei ndogo, nawasaidia.” alisema.

Awali watu walionunua viatu katika duka hilo waliieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa mfanyabiashara huyo anauza viatu vibovu kwa kuwahaa wananunuzi wanaonunua dukani kwake ambao wakishalipa pesa huwafungia viatu vibovu badala ya vipya na wanaporudi kulalamika huwatisha kuwa atawaitia polisi. 

“Huyu muhindi ni hatari sana, anauza vitu vibovu dukani kwake tena hadharani hapo lakini hakamatwi. Mtu akienda pale kununua hukuta viatu vizima vilivyo ubaoni lakini akishalipa pesa na kupewa bidhaa yake, akifika nyumbani akifungua anakutana na viatu vilivyooza kabisa na ukirudi kulalamika anakutishia polisi, nadhani kuna polisi anafahamana nao wanaomlinda.

“Hayo ndiyo yaliyonikuta hata mini lakini inakuwa vigumu kulalamika zaidi kwa sababu hatoi risiti na tunakubali kutoa hela bila kupewa risiti kwa sababu anauza bei rahisi ssna,” alisena mmoja wa watu walionunua viatu hivyo.

Jitahada za kumtafuta wakala wa viatu hivyo hapa nchini ili kuzungumzia athari anazozipata katika soko kutokana na kuuzwa kwa bidhaa mbovu na kwa bei ya chini hazikufanikiwa mara moja lakini Tanzania PANORAMA Blog inaendalea kumtafuta.

 

 

 

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya