RIPOTA WA PANORAMA
0711 46 49 84
MFANYABIASHARA Remoy Kibombe amepoteza mali zake na pesa zaidi ya shilingi bilioni moja baada ya kuhadaiwa na mganga wa kienyeji anayefahamika kwa jina la Salim Kanyani kuwa atapata utajiri wa ghafla kwa msaada wa majini.
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu tukio la kufilisika kwa mfanyabiashara huyo anayejihusisha na biashara ya vyuma chakavu Jijini Mwanza, sambamba na kutajirika haraka haraka kwa mganga wa kienyeji Kanyani, imeonyesha kuwa wawili hao walifahamiana baada ya kukutanishwa na aliyekuwa dalali maarufu katika jiji hilo, marehemu Hashim Shimweta
Kwa mujibu wa uchunguzi, marehenu dalali Shimweta alikuwa akifahamiana na mfanyabiasha Kibombe na alimtambulisha kwa mganga wa kienyeji Kanyani kwa ajili ya kumpatia tiba ya matatizo yake ya kiafya.
Hata hivyo, uchunguzi umeibaini kuwa merehemu dalali Shimweta alifariki dunia mwaka jana baada ya kupondwa na mawe yaliyokuwa yakimwagwa na roli eneo la Nyamanoro jijini Mwanza.
Watu wa karibu na mfanyabiashara Kibombe wameieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa, Kibombe akiwa katika matibabu ya afya yake, mganga Kanyani alimwambia anayo majini ambayo yamemwambia mteja wake huyo ana nyota ya biashara na ana mali na ukwasi mwingi lakini mali na ukwasi alionao havitulii kwake kwa sababu havijaoshwa na kwamba yupo hatarini kupoteza utajiri wake huo asipochukua hatua za kuulinda kwa kusafisha nyota yake na kuosha fedha zake kwa kutumia nguvu za giza.
Imeelezwa kuwa mganga wa kienyeji Kanyani alimwambia mteja wake kuwa majini yake yana uwezo wa kusafisha nyota za kibiashara, kusafisha fedha na kuziongeza kwa kiasi chochote mtu atakacho iwapo atatimiza masharti atakayopewa na majini hayo.
Taarifa zimeeleza kuwa mganga Kanyani alimtaka mteja wake Kibombe, ampatie kiasi kidogo cha Dola za Marekani ili ayape majini yake yaweze kuziosha na kuzizalisha, jambo ambalo alilitimiza na baada ya mganga huyo kuzungumza na majini yake kama alivyodai alirudi kwa mfanyabiashara Kibombe akiwa na mabosi sita makubwa yaliyokuwa yamejaa Dola za Marekani.
Watu wa karibu na mganga Kanyani wameeleza kuwa Dola za Marekani alizoonyeshwa mfanyabiasha Kibombe hazikuwa halisi na hakupewa muda wa kuzishika bali alifunguliwa tu maboksi hayo na kuonyeshwa zikiwa zimepangwa kwa ustadi kisha akaambiwa zinarudishwa kwa majini hayo na iwapo anataka kuzichukua anapaswa kwanza kutekeleza matakwa ya majini hayo.
Imeelezwa zaidi kuwa mganga Kanyani baada ya kuzirudisha Dola za Marekani kwa majini alirudi kwa Kibombe na kumwambia majini yametoa masharti kuwa kila boksi moja lililojaa Dola za Marekani alizoonyeshwa linapaswa kulipiwa Dola za Marekani za kibinadamu 150,000 (laki moja na nusu) kama tambiko kwa majini ili yaweze kuziachia Dola za Marekani za majini zilizojaa kwenye maboksi sita ziwe zake na kwamba zitakuwa zikiongezeka haraka haraka kwa kadri atakavyokuwa akizifanyia biashara.
Kwa mujibu wa masharti aliyopewa Kibombe, alipaswa kutoa Dola za Marekani 900,000 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 1.4 za Tanzania, pesa ambazo hakuwa nazo katika akaunti zake za benki.
Taarifa zilizokusanywa na Tanzania PANORAMA Blog zimeonyesha zaidi kuwa Kibombe alizitamani Dola Marekani alizokuwa ameonyeshwa na mganga Kanyani na alimtaka ampe muda ili akusanye kiasi cha fedha kilichokuwa kinatakiwa na majini kama sharti la kumpatia maboksi sita yaliyojaa Dola za Marekani..
Uchunguzi wa namna Kibombe alivyoanza kutafuta fedha za kulipia masharti ya majini umeoyesha kuwa alianza kuuza mali zake ambazo ni pamoja na magari matano ya kihafari, moja likiwa la mke wake, nyumba, viwanja na ghala lake la kuhifadhia vyuma chakavu.
Imeelezwa zaidi kuwa Kibombe aliwasilisha mkupuo wa kwanza wa malipo ya fedha za kibinadamu kwa majini kupitia kwa mganga Kanyani, shilingi milioni 600.
Hata hivyo mganga Kanyani alimtaka Kibombe akasajili laini ya sinu kwa jina lake amletee ili awe anamtumia fedha kupitia kwenye laini hiyo hadi atakapokamilisha malipo yote. Sharti ambalo alilitekeleza.
INAENDELEA KESHO.