![]() |
Nyama zinazouzwa machinjio ya Vingunguti |
NA MWANDISHI WETU
MWAKILISHI wa Kampuni ya Farmer’s Choice ya Kenya, Coroline Manka aliyeletwa nchini kusimamia bidhaa za nyama zinazozalishwa na kampuni hiyo amekiri kuwa Kampuni ya Bright Choice inanunua nyama katika machinjio ya Vingunguti.
Akizungumza leo na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu tuhuma inazoelekezewa Kampuni ya Bright Choice Limited kuwa imekuwa ikighushi nembo za Kampuni ya Farmer’s Choice Limited na kuziweka katika bidhaa zake, alisema anachofahamu yeye, nyama inayonunuliwa Vingunguti ndiyo inayotengenezwa na kuuzwa na Kampuni ya Bright Choice.
Alizitaja bidhaa za nyama zinazotengenezwa na Bright Choice kuwa ni ‘beef fillet na beef mince,’ na kwamba soko lake kubwa liko mkoani Arusha.
Akizungumza kuhusu majukumu yake ndani ya kampuni hiyo alisema ni kweli kwamba aliletwa hapa nchini na Kampuni ya Farmer’s Choice kama mwakilishi wake na pia alikiri kuwa alipofika hapa nchini aliajiriwa na Kampuni ya Bright Choice kwa majukumu tofauti na aliyopewa na Farmer’s Choice ya Kenya.
Hata hivyo, Manka alikataa kuzungumzia tuhuma za Kampuni ya Bright Choice kutengeneza bidhaa bandia za Farmer’s Choice na kutaka atafutwe Mkurugenzi wa Bright Choice kuzungumzia suala hilo.
Baadaye, mmoja wa wakugenzi wa Kampuni ya Bright Choice, Jacob Mlingi, aliipigia simu Tanzania PANORAMA Blog akiomba miadi ya kukutana na mwandishi kwa mazungumzo lakini alipoambiwa atoe ufafanuzi wa kile anachokifahamu kuhusu tuhuma inazoelekezewa Bright Choice alikataa kusema chochote.
Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kufuatilia sakata hili.