![]() |
Rais Samia Suluhu Hassan |
NA CHARLES MULLINDA
KAZI ya kujenga uchumi na kupambana na umaskini inaendelea chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo kabla ya kutimiza siku 100 madarakani imekwishakanyaga kila unyayo wa Serikali ya Awamu ya Tano na sasa imeanza kuacha nyayo zake katika sekta za maji, umeme, biashara na uwekezaji, elimu, ujenzi na uchukuzi.
Hayo yameelezwa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa hali ya Taifa na utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa umma, uliofanyika mkoani Dodoma,
Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) alisema pamoja na dunia kutikiswa na ugonjwa wa Corona na hivyo uzalishaji katika maeneo mengi kushuka kwa kiwango kikubwa, watanzania wanaendelea kuchapa mwendo kimaendeleo na Serikali inawahimiza kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali kwa juhudi na maarifa huku wakichukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Alisema kutokana na mwenendo huo, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekwishaeleza msimamo wake wa uongozi wa kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na watangulizi wake, tayari amekwishakanyaga nyayo zote zilizoachwa na awamu zilizotangulia, hususan awamu ya tano ambayo yeye mwenyewe alikuwa msimamizi pacha wa kiongozi mkuu wa utekeleza wa ilani ya uchaguzi, ambayo alishiriki kikamilifu kuinadi kwa watanzania.
Msigwa alisema, Serikali inaendelea kutekeleza kwa mafanikio ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendo kasi ambayo kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, chenye urefu wa kilomita 300 sasa umefikia asilimia 91 na kipande cha Marogoro hadi Makutopora chenye urefu wa kilomita 422, umefikia asilimia 61.
“Ujenzi wa reli kutoka Mwanza hadi Isaka umeanza na tayari Serikali imetoa Shilingi Bilioni 372.34 kwa ajili ya ujenzi huo ambao reli yake ina urefu wa kilomita 341.
![]() |
Daraja la Kigongo – Busisi |
“Kazi kwenye ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, huko Mto Rufiji inaendelea na sasa umefikia asilimia 52 kutoka asilimia 45 za awali na ujenzi wa Bwawa la Kigongo hadi Busisi mkoani Mwanza sasa umefikia asimilia 27. Mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 721 hadi utakapokamilika mwaka 2024,” alisema Msigwa.
![]() |
Ndege ya Air Tanznania |
Kuhusu usafiri wa anga alisema ndege tatu mpya zinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa na hivyo pamoja na nane zilizopo, zitafanya idadi yake kuwa 11.
Aidha, Msigwa alisema ujenzi wa miondombinu ya Jiji Dar es Salaam, kazi inaendelea ambapo sasa ujenzi wa Daraja la Tanzanite umefikia asilimia 77.19. Maeneo mengine aliyoyataja ambako kazi inaendelea usiku na mchana ni ujenzi wa barabara ya juu Chang’ombe na Kurasini, barabara za mabasi ya mwendo kazi katika Barabara ya Kilwa na upanuzi wa Barabara ya Morogoro.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa meli ya Mv Mwanza – Hapa Kazi tu ambao umefikia asilimia 74. 19 na kwamba mwaka huu kuna mikataba tisa ya ujenzi wa meli itakayotekelezwa ambayo ni pamoja na ujenzi wa meli mpya tatu katika maziwa makuu, meli mpya moja Bahari ya Hindi pia ukarabati wa meli tano Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.