Wednesday, June 25, 2025
spot_img

KAMPUNI YA PARAMOUNT YAHAHA KUFICHA UKWELI WA TUHUMA ZAKE

 

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Paramount Commodities Limited ya mkoani Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya mazao mbalimbali, sasa imeanza kuhaha kuficha ukweli wa tuhuma zake huku baadhi ya iliowatambulisha kuwa ni wasemaji wake wakikataa kuzungumza chochote.

Paramount inadaiwa kufanya shughuli zake za kununua na kuuza mazao nje ya nchi kinyemela ikiwa imejificha ndani ya kampuni nyingine na pia inadaiwa kukwepa kulipa kodi, kukiuka sheria za ajira, kuajiri wafanyakazi wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini pamoja na kunyanyasa wafanyakazi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Paramount, Dhaval Patel katika mazungumzo yake na waandishi wa habari kuhusu tuhuma inazoelekezewa kampuni yake, alisema kampuni ina msemaji na alitoa namba zake za simu ili apigiwe atoe majibu.

Msemaji huyo ambaye awali alificha jina lake lakini uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog umeonyesha kuwa anaitwa Evans Kisavio, kwanza alisema hayuko kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza hivyo atafutwe baadaye lakini jitihada za kumtafuta tena jana hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, alipotafutwa leo mapema asubuhi saa 2.30 alipokea simu lakini alikataa kuzungumza lolote kwa madai kuwa yupo harusini lakini alipoulizwa ni harusi gani inayofungwa mapema asubuhi alisema anaomba kukutana na mwandishi kwa mazungumzo.

Mwandishi aliposisitiza kuwa maswali yake yanaweza kujibiwa kwenye simu, Kisavio alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sababu yeye siyo msemaji wa kampuni hiyo bali atafutwe Dhaval amalize matatizo yake mwenyewe.

Taarifa zaidi zilizopatikana zimeeleza kuwa uongozi wa Kampuni ya Paramount amemuita ofisini kwake haraka mmoja wa wafanyakazi aliyefukuzwa ili akalipwe stahiki zake na ameombwa asiongee tena na waandishi wa habari.

Imeelezwa kuwa mfanyakazi huyo (jina tunalihifadhi) ndiye anayedhaniwa na uongozi wa Kampuni ya Paramount kutoa siri za kampuni hiyo kwa waandishi wa habari

Jana Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa; Kampuni ya Paramount inaendesha shughuli zake za biashara ndani ya jengo linalomilikiwa na kampuni nyingine ambayo jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

Inadaiwa Paramount imekuwa ikinunua mazao na kuuza nje ya nchi, kuajiri raia wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kuishi wala kufanya kazi nchini na imefunga mitambo ya kusafishia mazao bila ya kuwa na ofisi.

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo aliyezungumza na waandishi wa habari (jina tunalihifadhi) alisema shughuli zote za kibiashara za kampuni hiyo zinafanywa ndani ya eneo la kampuni nyingine.

“Hawa wahindi ni watu wa ajabu sana. Huyu sisi ametuajiri lakini kwanza hatuna mikataba ya kazi, hatuna pensheni ya aina yoyote ile yaani kiufupi hafuati taratibu zote za ajira za hapa nchini.

“Hapa ndani, hizi siyo ofisi zake, hii kampuni haina ofisi ujue, hizi ni ofisi za kampuni nyingine lakini jamaa huyu wa Paranount amejificha humu, anafanya biashara lakini halipi kodi wala nini kwa sababu hizi siyo ofisi zake.

“Sasa humu amefunga mashine za kusafishia ufuta, ufuta una vumbi sana kuusafisha hivyo wafanyakazi wanatakiwa kuwa na vifaa vya kujikinga na hilo vumbi kwa ajili ya afya zao lakini hawa hawana kifaa chochote, vumbi lote linawaingia wanaishia kuumwa vifua na hana huruma, ukiugua anakufukuza kazi.

“Hakuna mamlaka za Serikali zinazojua ofisi za hii kampuni zilipo kwa hiyo siyo rahisi kuzifuatilia, hizo mashine hata TRA hawajui kama zimefungwa humu na zinafanya kazi ya kusafisha ufuta.

“Jamaa wa hii kampuni wanajifanya wawekezaji lakini wana madudu mengi sana na wanafanya wanavyotaka kwa sababu Serikali haijui lolote kuhusu ofisi zao zilipo maana wamejificha kwenye kampuni nyingine,” alisema mtoa taarifa.

Jitihada za kuutafuta uongozi wa kampuni ambayo imeikaribisha kampuni ya Paramount kufanya shughuli zake za biashara ndani ya ofisi zake kwa kificho bado zinaendelea.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya