Wednesday, June 25, 2025
spot_img

MAZINGAOMBWE YA KAMPUNI YA PARAMOUNT

 

Ufuta


NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Paramount Limited ya mkoani Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya mazao mbalimbali inadaiwa kuendesha shughuli zake kinyemela ndani ya eneo la mamlaka ya maeneo maalumu ya uzalishaji kwa mazao ya nje (EPZ)

Sambamba na hilo kampuni hiyo inadaiwa kuajiri raia wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini, kukwepa kulipa kodi na pia kutotekeleza matakwa ya sheria za ajira.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya ofisi hizo zimedai kuwa, kampuni hiyo inaendesha shughuli zake za biashara ndani ya jengo linalomilikiwa na kampuni nyingine ambayo jina lake tunalihifadhi kwa sasa

Inadaiwa Paramount imekuwa ikinunua mazao na kuuza nje ya nchi, kuajiri raia wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kuishi wala kufanya kazi nchini na kufunga mitambo ya kusafishia mazao bila ya kuwa na ofisi.

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo aliyezungumza na waandishi wa habari (jina tunalihifadhi) amesema kuwa shughuli zote za kibiashara za kampuni hiyo zinafanywa ndani ya eneo la kampuni nyingine.

“Hawa wahindi ni watu wa ajabu sana. Huyu sisi ametuajiri lakini kwanza hatuna mikataba ya kazi, hatuna pensheni ya aina yoyote ile yaani kiufupi hafuati taratibu zote za ajira za hapa nchini.

“Hapa ndani, hizi siyo ofisi zake, hii kampuni haina ofisi ujue, hizi ni ofisi za kampuni nyingine lakini jamaa huyu wa Paranount amejificha humu, anafanya biashara lakini halipi kodi wala nini kwa sababu hizi siyo ofisi zake.


“Sasa humu amefunga mashine za kusafishia ufuta, ufuta una vumbi sana kuusafisha hivyo wafanyakazi wanatakiwa kuwa na vifaa vya kujikinga na hilo vumbi kwa ajili ya afya zao lakini hawa hawana kifaa chochote, vumbi lote linawaingia wanaishia kuumwa vifua na hana huruma, ukiugua anakufukuza kazi.

“Hakuna mamlaka za Serikali zinazojua ofisi za hii kampuni zilipo kwa hiyo siyo rahisi kuzifuatilia, hizo mashine hata TRA hawajui kama zimefungwa humu na zinafanya kazi ya kusafisha ufuta.

“Jamaa wa hii kampuni wanajifanya wawekezaji lakini wana madudu mengi sana na wanafanya wanavyotaka kwa sababu Serikali haijui lolote kuhusu ofisi zao zilipo maana wamejificha kwenye kampuni nyingine,” alisema mtoa taarifa.

Alipoulizwa mkurugenzi wa Kampuni ya Paramount aliyetambulika kwa jina moja la Dawal, kuhusu madai hayo alisema anayeweza kuyazungumzia ni msemaji wake ambaye alitoa namba zake za simu ili atafutwe.

Alipotafutwa msemaji huyo ambaye hata hivyo imebainika ni mmoja wa wamiliki wa jengo ambalo Paramount inaendesha shughuli zake kwa uficho, alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kuzungumza hivyo atafutwe baadaye na alipotafutwa baadaye kama alivyoomba alisema aulizwe Dawal mwenyewe azungumzie matatizo yake.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya