DUKULE INJENI
Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, wanarudi nchini wakihitaji hesabu kali ya kuhakikisha wanapindua matokeo katika mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Simba chini ya ukufunzi wa kocha Mfaransa, Didier Gomes waliruhusu mabao manne katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumamosi Mei 15, Uwanja wa FNB jijini Johannesburg na kuwafanya wapinzani wao kuweka mguu moja hatua ya nusu fainali.
Iliwachukua dakika sita wenyeji kupata bao la kwanza lililofungwa na Eric Matholo na kisha Samir Nurkovic, Raia wa Serbia akatupia bao la pili dakika ya 34 na lingine dakika ya 57, huku Leonardo Castro, raia wa Colombia akihitimisha ushindi mnono kwa Kaizer Chiefs dakika ya 63.
Kuruhusu mabao manne ugenini ni mlima mrefu kwa Simba lakini bado hiyo haijazima ndoto yao ya kutinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo msimu huu wamekuwa gumzo barani Afrika.
Kocha Gomes anazo takribani siku sita, yeye pamoja na jopo lake la benchi la ufundi kurudi mezani na kupanga mikakati ya kupindua meza kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam, Jumamosi Mei 22.
Moja ya maeneo ambayo Simba inapaswa kuyafanyia kazi ni kutumia nafasi wanazopata kwani katika takwimu za mechi dhidi ya Kaizer Chiefs zinaonyesha, licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 65, walishindwa kupata hata shuti moja lililolenga goli.
Hata hivyo, ni dhahiri Gomes ameshawasoma wapinzani wao na kwa kuzingatia Simba wamekuwa na matokeo mazuri wanapocheza uwanja wa nyumbani msimu huu katika michuano ya kimataifa, watahitaji ushindi wa zaidi ya mabao manne.
Simba inajivunia safu nzuri ya ushambuliaji ambapo imetoa wachezaji wanne kati ya 10 bora hadi sasa wanaowania Kiatu cha Dhahabu msimu huu huku kwa ujumla wao wakiwa wamefunga mabao 36.
Wachezaji hao wanne wa Simba kati ya 10 bora wanaowania Kiatu cha Dhahabu na idadi ya mabao waliyofunga katika mabano hadi sasa ni Meddie Kagere (11), John Bocco (10), Chris Mugalu (8) na Luis Miquissone (7).
Mechi ya kwanza dhidi ya Kaizer Chiefs imewapa benchi la ufundi fursa ya kujua ni wachezaji gani hatari ambao wanahitaji kupewa ulinzi mkali ili wasiwe na madhara kiasi cha kuzima kabisa ndoto ya Simba kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Matokeo ambayo Simba wamepata ni dalili tosha ya kuwakumbusha kwamba wapinzani wao Kaizer Chiefs wana sura mbili tofauti; ile inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini na ile inayocheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hali ya Kaizer Chiefs kwenye ligi ya nyumbani sio ya kuridhisha ambapo wameshindwa kupata ushindi katika mechi zao nne za mwisho kiasi cha mashabiki kuanza kushinikiza uongozi kumtimua kocha wao. Gavin Hunt.
Hata hivyo, katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Amakhosi kama wanavyofahamika na mashabiki wao wamekuwa wa moto wakimaliza nafasi ya pili kwenye kundi lao na ushindi dhidi ya Simba unawapa matumaini ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.