Thursday, June 26, 2025
spot_img

RAIS SAMIA KURA YA TURUFU YA CCM CHAGUZI NDOGO ZA BUHIGWE, MUHAMBWE

 

Rais Samia Suluhu Hassan 

CHARLES MULLINDA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ni kura ya turufu ya CCM katika chaguzi ndogo za ubunge wa majimbo ya Buhigwe na Muhambwe zinazotarajiwa kufanyika kesho, Mei 16, 2021.

Uturufu wa Rais Samia ni uchapakazi wake, jinsia yake, haiba yenye mvuto kwa watu wa rika, dini na itikadi tofauti, ucha Mungu, uzalendo kwa nchi yake, ujasiri, uthubutu na mapenzi aliyonayo kwa Watanzania ambavyo vimebebwa na kuwekwa kibindoni na CCM kinachoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Buhigwe na Muhambwe; kama kura yake turufu ya kukipa ushindi.

Wananchi wa Buhigwe na Muhambwe, kesho wanatarajiwa kupiga kura za ‘mapenzi’ kwa CCM kama ishara ya shukrani, furaha na pongezi; na imani waliyonayo kwa Rais Samia, achilia mbali kura zilizosakwa na makada wa chama hicho wakiwemo vigogo, katika kipindi cha kampeni za uchaguzi, ambazo nazo zina kivuli cha Rais Samia.

Tayari CCM kimekwishakiri hilo kupitia kwa mpiga propaganda wake mkuu, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, aliyeueleza umma wa Watanzania kuwa pamoja na sababu nyingine zitakazokipa ushindi CCM kwenye chaguzi hizo, mojawapo ya muhimu ni shukrani za wananchi wa majimbo hayo kwa Rais Samia kwa kumteua Dk. Philip Isdor Mpango, kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanawake wa Buhigwe wanaotarajiwa kupiga kura kesho


Aidha, tathimini ya jumla ya kampeni katika majimbo ya Buhigwe na Muhambwe imeonyesha kuwa wanawake wengi watakipigia kura CCM kwa sababu ya kumuunga mkono mwanamke mwenzao, Rais Samia na kukishukuru CCM kwa kutomuwekea mizengwe kwenye kushika hatamu ya kuliongoza taifa bila kujali jinsia yake, kama yalivyo matakwa ya Katiba.

Sambamba na wanawake, wapigakura wanaume nao wanatarajiwa kuegemea katika kukipigia kura CCM kama ishara ya kumuunga mkono Makamu wa Rais, Dk. Mpango ambaye ni zao la Rais Samia kwenye wadhfa alionao sasa na pia imani waliyonayo kwa Rais Samia kuwa ndiye kiongozi mwenye sifa zote za kurithi mikoba ya Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyeiachia dunia soma la uongozi bora, ucha Mungu, uzalendo, ujasiri, uthubutu na mapenzi ya dhati kwa taifa na watu wake.

CCM, chama chenye macho matatu katika siasa za kimkakati na zile za majukwaani, kikiwa kimekwishang’amua Rais Samia ni kura yake ya turufu katika chaguzi hizo, kimemtuma Makamu wa Rais wa Tanzania na pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk. Mpango ambaye bado ananukia u Samia Samia kwenda kufunga kampeni katika majimbo yote mawili.

Uamuzi huu wa CCM wa kumtumia Dk. Mpango ambaye angali amefunikwa na kivuli cha maualidi cha Rais Samia kwenda kufunga kazi katika kampeni hizo ni wa kimkakati zaidi na unalenga kuminya pumzi ya mwisho ya vyama vya upinzani vilivyojitosa kwa kuweka wagombea wao ambao kuna kila dalili kwamba wataambulia patupu katika uchaguzi huu ulioalika walimwengu kuushuhudia kuanzia kampeni zake hadi upigaji kura jinsi ulivyotakasika.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka


Kutokana na mwenendo huo, haina shaka hata kidogo kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka, katika tamko la tathimini ya mwenendo wa kampeni za uchaguzi mdogo wa majimbo ya Buhigwe na Muhambwe; kwa kujiamini aliandika; 

“Uzinduzi wa kampeni za ubunge katika Jimbo la Muhambwe ulifanyika Mei 4, 2021 na Jimbo la Buhigwe Mei 5, 2021 ukiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa.

“Chaguzi hizi ni kutokana na kufariki kwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Atashasta Nditiye na Mbunge wa Buhigwe, Dk. Philip Isdor Mpango kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tulipoteza Mbunge wa CCM kwa kifo kule Muhambwe, hivyo wananchi wanachokitaka ni kuifariji CCM. Kwa Jimbo la Buhigwe wananchi wenyewe wanataka kumpa ahsante Rais Samia kwa kumteua kuwa Makamu wa Rais aliyekuwa mbunge wao, Dk. Philip Isdor Mpango.”

CCM, kikijua kuwa nyota ya Rais Samia inang’ara kwa uchapakazi wake sambamba na kusimamia bila lelemama Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo imeleta mageuzi chanya katika nyanja zote za kiuchumi, kimeutumia vema muda wa kampeni kutangaza Sera na Ilani yake ya uchaguzi ambayo imebeba mzigo wa kuwaletea wananchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wagombea wa chama hicho, Dk. Frolence George Samizi wa Jimbo la Muhambwe na Mwalimu Eliadory Felix Kavejuru wa Jimbo la Buhigwe wamekuwa na wakati mzuri wa kampeni kwa kukumbatiwa muda wote na vigogo na makada maarufu na mashuhuri wa CCM waliopita nao kwa wapiga kura wakiwaomba wawachague ili neema ya uchumi wa kati waliyoionja katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, iendelee kuwashukia.

Haya nayo yanathibitishwa na Shaka ambaye katika taarifa ya CCM ya tathimini ya kampeni za uchaguzi Muhambwe na Buhigwe, anazungumza kwa majigambo yenye kuwatisha kisiasa wagombea wa vyama vya upinzani huku pia akiwaaminisha wapiga kura na umma wote kuwa hakuna mahali palipoachwa bila kukanyangwa na CCM, anasema; “majimbo ya Buhigwe na Muhambwe ni ya CCM.

“CCM imedhihirisha kivitendo uwezo wake mkubwa wa kuwatumikia wananchi katika awamu zote za uongozi. Kazi kubwa ya kisera na utekelezaji wa miradi, kuondoa kero kwa wananchi wakiwemo wa Buhigwe na  Muhambwe imefanyika chini ya CCM hivyo ushindi wa CCM ni jambo lisilo na shaka wala wasiwasi.

“Mfumo wa kampeni kwa wagombea wetu ulijielekeza katika kufanya zaidi mikutano midogo, kukutana na kuzungumza na makundi ya kijamii katika maeneo yao, makazi na vijiji vyao.

“Dk. Florence George Samizi amefika katika kata zote 19 na amefanya mikutano midogo ya kampeni na kukutana na makundi maalumu ya vijana, wanawake, wazee, wafanyabiashara na makundi mengine ya kijamii. 

Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,. Kassim Majaliwa


“Wakati wote wa kampeni wananchi wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano yetu ya kampeni jimboni humo na kuonyesha matarajio yao kwa mgombea wa CCM Dk. Samizi.

“Mwalimu Eliadory Felix Kavejuru amefanya kampeni katika kata zote 20 na kukutana na wananchi katika vijiji 44, sawa na asilimia 100 ya vijiji vyote na anaendelea kumalizia kampeni katika vitongoji vinane vilivyobaki kati ya 192.

“Mikutano mikubwa imefanywa kimkakati katika viwanja vya Shule ya Msingi Buhigwe, Munanila na Muyama maeneo hayo yana wakazi wengi  waliojiandikisha kupiga  kura. 

“Mikutano midogo 62 aliyoifanya mgombea wa CCM, Kavejuru pamoja na mazungumzo mahususi na makundi ya kijamii yamemkutanisha na kumpa uhakika zaidi wa kupata ushindi.”

Katika kampeni hizi za chaguzi ndogo kwenye majimbo ya Buhigwe na Muhambwe, pia CCM kimenufaika sana na mtandao wake wa jumuiya za ndani ya chama kilizozishirikisha kikamilifu kuwafikia ‘wafia chama,’ wanachama, wapenzi na mashabiki ambao wamelegezwa mioyo yao kwa kuwaona makada na vigogo wa chama hicho wanaowika kwa sasa wakiwa mguu kwa mguu na wagombea kusaka kura za ushindi.

Kote walikopita, Muhambwe na Buhigwe kelele zilikuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM inayonunulika kwa sasa; kwa manufaa kwa Watanzania wote.

Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Dk. Philip Isdor Mpango


Ndiyo maana haitia shaka kumsikia Shaka akisema, “Kampeni za CCM katika majimbo yote mawili zitafungwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Philip Isdor Mpango Mei 14 na Mei 15, 2021 katika uwanja wa Taifa kwa Jimbo la Muhambwe na Uwanja wa Shule ya Mayama kwa Jimbo la Buhigwe

“Tathmini ya awali imeonesha katika majimbo hayo  CCM itashinda si chini ya asilimia 80 na ikumbukwe ushindi huu hautakuwa mgeni kwetu kwani CCM ni kinara na baba wa mageuzi ya demokrasia nchini, Afrika na duniani kwa ujumla.

“Nilisema siku ya uzinduzi na ninaendelea kusisitiza, CCM itashinda Buhigwe na Muhambwe kwa haki, amani na utulivu mkubwa na sababu za ushindi ni nyingi lakini kubwa ni imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi.

“Chini ya uenyekiti wa CCM wa Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaendelea kuvilea vyama vya siasa nchini ili viweze kufanya siasa safi na zenye tija kwa Taifa badala ya kufanya siasa za danadana. Sote tunajenga nyumba moja hakuna sababu ya kugombea fito.”


Mwenyekiti, Rais Samia, akiyajua yote haya ameamua kwenda kupumzika shinani alikotokea kusubiri muda uzungumze ndiyo arejee Dodoma kuwazingua watakaomzingua kwa sababu ameapa, iwe jua au mvua, jahazi analoliongoza lazima lifike bustanini 2025 kuchuma maualidi yaliyochipua.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya