![]() |
Kaizer Chiefs |
DUKULE INJENI
WAPINZANI wa Simba katika mechi ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, Kaizer Chiefs, watashuka katika Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg, Afrika Kusini Jumatano Mei 12, mwaka huu kuwavaa Moroka Swallows.
Mchezo huu wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini itatumiwa na kocha wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt, kama sehemu ya maandalizi kuelekea mechi yao dhidi ya Simba itakayopigwa Jumamosi Mei 15 mwaka huu jijini Johannesburg.
Tofauti na Simba ambao wanaongoza jedwali la msimamo wa Ligi Kuu Bara, hali ni mbaya kwa Kaizer Chiefs ambapo katika mchezo wa mwisho wa ligi ya kwao walichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa timu ya Tshakhuma Tsha Madzivhandila (TTM) inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr.
Mara ya mwisho Kaizer Chiefs kushinda mchezo wa Ligi Kuu Afrika Kusini ilikuwa Aprili 25 walipowafunga vinara Mamelodi Sundowns mabao 2-1 na tangu mechi hiyo, wamecheza michezo mitatu wakipoteza miwili na kutoka sare moja.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini, vijana wa Hunt wanashika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 29 baada ya kucheza michezo 26. Kwa kifupi wamewazidi kwa pointi tano Chippa United iliyo kwenye mstari wa kushuka daraja.
Nafasi ya tisa sio nafasi nzuri kwa Kaizer Chiefs, moja ya klabu kongwe Afrika Kusini ambayo imebakiza mechi nne ngumu dhidi ya Swallows, Black Leopards, Golden Arrows na TS Galaxy kabla ya kumaliza msimu.
Katika hizi mechi nne zilizobakia, Kaizer Chiefs wanahitaji angalau pointi nane kati ya 12 zitakazowafanya wafikishe pointi 37, la sivyo wanaweza wakajikuta wapo nafasi ya 15 itakayowafanya kushuka daraja.
Hali inaweza ikawa mbaya zaidi kwa Hunt na vijana wake endapo timu kama Bloemfontein Celtic, Baroka, Stellenbosch, Maritzburg United, Tshakhuma na Chippa United zitashinda mechi zao zote zilizobaki.
Kwa mantiki hiyo, Kaizer Chiefs wapo katika vita vitatu navyo ni kuepuka kushuka daraja, kupigania kumaliza nafasi nane za juu ili kucheza ligi ndogo maarufu MTN8 na kutinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
![]() |
Simba Sports Club |
Simba waliondoka nchini alfajili ya Jumanne Mei 11 mwaka huu kuelekea Afrika Kusini na jambo jema ni kwamba benchi lao la ufundi chini ya kocha mkuu Didier Gomes itapata fursa kuwatazama wapinzani wao watakapoikabili Moroka Swallows Jumatano Mei 12.
Kocha Hunt yupo katika mtihani mgumu ni namna gani anavyoweza kupanga kikosi chake kuelekea mechi dhidi ya Swallows na kuhakikisha bado kinakuwa imara kuwavaa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Wakati Kaizer Chiefs watatumia mechi dhidi ya Swallows kama kipimo cha mchezo wao wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, wapinzani wao Simba walishuhudia mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya watani zao Yanga ikitibuka mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mechi hiyo ambayo awali ilikuwa ianze saa 11 jioni, iliahirishwa hadi saa 1 usiku kitendo ambacho Yanga walikipinga wakisisitiza ni kinyume cha kanuni wakisisitiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitakiwa kutoa taarifa ya mabadiliko saa 24 kabla ya mchezo.
Yanga iliingia Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam saa 11 jioni na walipoona wapinzani wao hawapo, wakaondoka huku Simba ikiingia uwanjani saa 1 usiku na wao pia wakawakosa wapinzani wao.
Kocha Gomes ambaye amekuwa na wakati mzuri tangu kuchukua mikoba ya Sven Vandenbroeck alitamani kucheza dhidi ya Yanga ili kukipima kikosi chake kuelekea mtanange dhidi ya Kaizer Chiefs.
“Wachezaji walikuwa tayari kwa mchezo huu na maandalizi yalikuwa yamekamilika. Tulihitaji kucheza ili kuongeza morali ya wachezaji lakini imeshindikana hivyo tunajiandaa kwa mchezo unaofuata (dhidi ya Kaizer Chiefs),” alisema Gomes na kuongeza.
“Sote tulipata taarifa ya mchezo kusogezwa mbele, nawaomba radhi mashabiki wa Simba na wadau wa soka nchini kwa utata uliojitokeza, binafsi nimeshutushwa na hilo lakini naamini litamalizika salama.”