Monday, December 23, 2024
spot_img

MOYO WANGU USILIE TENA

NA JOSEPH SHALUWA

Email: joeshaluwa@gmail.com

Simu: 0718-400146

Facebook @Joseph Shaluwa

Instagram @joeshaluwa

HANA haraka anapotembea, ukimtazama anaonekana kujiamini sana. Tabasamu mwanana linaupamba uso wake lakini mavazi yake yanaonesha asivyo mtu wa dhiki!

Hata kama siyo sana lakini uwezo wa kubadilisha mboga ulikuwa mikononi mwake! Anatoka kwenye duka hili maalumu kwa kuuza kadi na zawadi mbalimbali lililopo ghorofa ya saba, katika Jengo la KPC Towers, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Anatembea taratibu kuifuata lifti iliyokuwa mita chache mbele yake.

Anatabasamu! Ni kweli anatabasamu!

Tena basi alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, maana zilibaki wiki tatu tu kabla ya ndoa yake na mpenzi wake wa siku nyingi, Joanitha.

Mkononi mwake ana bahasha ya kaki ambayo ndani yake kuna zawadi kwa ajili ya Joanitha wake. Alijua anachotakiwa kumfanyia Joanitha!

Siku zote alikuwa akinunua apple tu, mambo yanakuwa sawa! Huo ulikuwa ugonjwa mkubwa zaidi kwa Joanitha. Alipoifikia lifti, alibonyeza kitufe mlangoni, mlango ukafunguka. Akaingia na kusimama, punde mlango ukajifunga, akabonyeza kwenye herufi G akimaanisha kwamba anataka kushuka chini.

Ni kijana mtanashati sana, anayevutia kwa kila mwanamke aliyekamilika. Anaitwa Deogratius Mgana. Mfanyakazi wa shirika moja lisilo la kiserikali jijini Dar es Salaam.

Ana furaha moyoni mwake, maana anakwenda kufunga ndoa na chaguo la moyo wake. Kwa nini asitabasamu? Hakika ana haki ya kutabasamu!

“Ni kweli lazima nitabasamu, kwanza nusu ya ndoto zangu tayari zipo kwenye mstari. Lazima nijisikie vizuri,” akawaza mwenyewe akiwa kwenye lifti.

Akabaki ametulia kimya akiwa amesimama kwenye lifti ile, ikaanza kushuka taratibu kwenda chini. Ghorofa ya sita, ghorofa ya tano, ghorofa ya nne…alipofika ghorofa ya tatu, lifti ikasimama. Hapo akajua kuna mtu mwingine aliyekuwa akitaka kushuka chini. Mlango ulipofunguka, wakaingia wanaume watatu, wote wamevaa miwani za jua. “Mambo bro?” mmoja akamsalimia. “Poa,” akaitikia Deo.

Lifti ikaanza kushuka taratibu, walipofika ghorofa ya pili, ikasimama. Mlango ulipofunguka tu, ghafla wale vijana watatu wakamsukuma hadi nje. Mara mlango ukafunga. “Paaaaaa!” mlio wa risasi ukasikika. Deo akaanguka chini, akianza kuvuja damu!

**

Alisikia vizuri sana mlio wa simu yake lakini aliamua kupuuzia! Si kwamba hakutaka kwenda kupokea, lakini alikuwa na kazi muhimu aliyokuwa akiifanya, zaidi ya kwenda kupokea simu!

Joanitha alikuwa anapika! Chakula kizuri ambacho mpenzi wake alikuwa anakipenda sana. Alikuwa anapika viazi vya kukausha, maarufu kama maparage ambayo Deo alikuwa akipenda sana. Siku hiyo Deo alipanga kwenda nyumbani kwa kina Joanitha, Mikocheni.

Ilikuwa zimebaki wiki tatu tu ndoa yake na Deo ifungwe. Siku ambayo alikuwa akiitamani sana na kuomba ifike haraka. Mlio wa simu yake ukakatika ghafla. Akaendelea na mapishi yake jikoni lakini baada ya muda mfupi simu ikaita tena kwa mara nyingine…

“Nani huyo aaah!” Joanitha akasema kwa hasira kidogo. “Mimi nampikia Deo wangu bwana alaaah!” akatamka tena, akifunika kile chakula jikoni na kufunga kanga vizuri.

Yap! Kama ungekuwepo, ungeamini kweli Joanitha alikuwa mwanamke mrembo. Pamoja na kwamba alikuwa amevaa kanga, lakini umbo lake lenye namba nane liliweza kuonekana vyema kabisa. Joanitha alijaaliwa umbo zuri la kuvutia. Ona anavyotembea… Kama anaonea huruma ardhi!

Ana hips pana zinazozidisha uzuri wake, ana macho mazuri yenye uwezo wa kumchanganya mwanaume yeyote aliyekamilika. Labda niseme kwamba Joanitha alikuwa mwanamke mrembo sana.

Alivyofika sebuleni simu ikaacha kuita. Akachukia sana lakini akiwa anainua ili aweze kujua aliyekuwa akimpigia ili aweze kumpigia tena, akashangaa simu yake ikianza kuita tena. Kwenye kioo cha simu yake likaonekana jina ‘My Darling’. “Jamani, kumbe ni sweetie,” akasema akipokea ili kumsikiliza.

Ilikuwa ni namba ya Deo ikionekana kwenye kioo cha simu yake…

“Yes baby, najua hujasahau kuninunulia apple na napenda kukujulisha kwamba, maparage yako yanakaribia kuiva ila sijui ungependa nikuandalie juice ya nini? Machungwa, maparachichi, maembe au mananasi? Maana kila kitu kipo kwenye friji,” Joanitha akasema kwa sauti iliyojaa mahaba mazito.

Ni vile hakujua tu! Laiti angejua!

Joanitha alihisi kumkosa sana mpenzi wake Deo. Kitu pekee ambacho alihitaji kwa muda huo ni kuisikia sauti nzuri ya mpenzi wake ambayo imetulia. Hakutaka kitu kingine chochote zaidi.

Simu ilikuwa sikioni, uso ukiwa umemjaa tabasamu mwanana, akisubiri kusikia sauti ya Deo wake. Hilo tu. Kilipita kimya cha sekunde kadhaa, kisha akasikia sauti ya upande wa pili… “Samahani dada, mimi siyo mwenye simu!” sauti hii ya kiume, tulivu yenye mikwaruzo kwa mbali ilisikika kwenye simu ya Joanitha. Hakuwa Deo!

“Sasa kama wewe si mwenye simu, kwa nini umepiga? Kwa nini unakosa ustaarabu?” Joanitha akamwuliza yule mtu akiwa na hasira. “Samahani sana dada’ngu, lakini nadhani ni vyema ukawa mtulivu na kuuliza kilichotokea. Si kawaida mtu kupiga simu isiyo yake kwa watu ambao wamehifadhiwa kwenye simu hiyo. Hiyo ingetosha kabisa kukufaya ugundue kwamba kuna tatizo!” mtu huyo akasema akizidi kuonesha kwamba anahitaji utulivu wa Joanitha.

“Ndiyo…enhee kuna nini? Hebu niambie, maana tayari nahisi nimeanza kuchanganyikiwa!”“Sina shaka wewe ndiye Joanitha!”

“Ndiyo!”

“Ni nani wako?”

“Ni mchumba’ngu, kwani vipi?”

“Usijali, tuliza moyo dada yangu. Mimi ni Dk. Palangyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Huyu ndugu mwenye simu, ameletwa hapa na wasamaria wema, baada ya kupitishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay!”

“Anaumwa na nini dokta?” Joanitha akauliza akianza kulia kwa huzuni.

“Amepigwa risasi na watu wasiojulikana katika Jengo la KPC Towers. Hata hivyo, hana hali mbaya sana, matibabu yanaendelea lakini nimeona ni vyema kukujulisha ili uwafahamishe na ndugu wengine!”

“Ahsante dokta kwa taarifa, baada ya nusu saa nitakuwa hapo,” Joanitha akajibu akizidisha kilio chake.

Akatoka mbio hadi chumbani kwake. Hakukumbuka kwenda kuipua chakula jikoni. Akavaa haraka na kutoka hadi getini! Ghafla kumbukumbu zake zikarudi!

“Mama yangu, nimeacha chakula jikoni na jiko linawaka,” akawaza akirudi ndani mbio. Ilikuwa ni hatari sana, maana alikuwa anapikia jiko la umeme. Mara moja akarudi ndani na kuzima jiko, akaipua kile chakula na kutoka kwa kasi sana.

“Wewe vipi mwenzetu, mbona hivyo?” mama yake akamwuliza baada ya kumuona mwanaye anaonekana kuwa na haraka ambayo hakujua ni ya nini.

“Nitakupigia simu mama!”

“Unakwenda wapi?”

“Mama nitakupigia!”

“Joan, mwenzako si anakuja au haji tena?”

“Mama Deo amepigwa risasi, yupo hospitalini,” akasema Joanitha akiwa tayari ameshaingia kwenye gari.

Akapiga honi kwa nguvu, mlinzi akafungua haraka. Joanitha akaondoa gari kwa kasi sana. Alikuwa anakwenda Muhimbili, huku nyuma akiwa amemuacha mama yake mwenye mawazo sana.

Joan aliendesha gari kwa kasi sana, hakujali ajali barabarani, alikuwa tayari kwa lolote litakalotokea! Kutokea nyumbani kwao Mikocheni hadi Muhimbili, alitumia dakika ishirini!

Hakukubali kukaa kwenye foleni, aliendesha kama daladala, kwani alipenyeza pembeni, sehemu zilizokuwa na foleni kubwa. Alipofika hospitalini, akaegesha gari lake kisha akapiga simu ya Deo na kuzungumza na yule daktari.

“Nimeshafika dokta!”

“Ok! Uko wapi?”

“Kwenye maegesho!”

“Tukutane Kibasila!”

“Sawa dokta.”

Bila kupoteza muda Joan akachanganya miguu hadi liilipo Jengo la Kibasila. Akiwa kwenye lango kuu la kuingilia, akamwona mwanaume mmoja mrefu aliyevaa koti jeupe na miwani, akahisi angekuwa ndiye daktari aliyekuwa akimfuata.

“Sorry, ni Dk. Pallangyo?” Joanitha akauliza akimkazia macho.

“Yes, karibu!”

“Ahsante!”

“Nifuate!”

Dk. Pallangyo akatangulia na Joanitha akimfuata nyuma. Safari yao ikaishia ofisini kwa daktari yule iliyokuwa nje ya Jengo la Kibasila.

“Karibu sana dada yangu!”

“Ahsante!” Joanitha akajibu na kuketi kwenye kiti, kwa mtindo wa kutazamana na daktari.

“Ulisema mgonjwa ni nani wako?”

“Mchumba wangu!”

“Oh! pole sana…kilichotokea ni kwamba, mwenzio amepigwa risasi ya begani, lakini inaonekana kutokana na mshtuko alioupata, umesababisha apoteze fahamu. Tunashukuru kwamba risasi haijatokeza upande wa pili, kwa hiyo tumefanikiwa kuitoa, lakini bado hajazinduka!”

“Mungu wangu, atapona kweli?”

“Uwezekano huo ni mkubwa sana lakini yafaa tuombe Mungu naamini atakuwa sawa.”

“Naweza kwenda kumuona tafadhali?”

“Bila shaka!” dokta akamjibu na kusimama.

Akaonesha ishara kwamba Joanitha amfuate. Akasimama na kumfuata nyuma yake.

***

Deogratias alikuwa amelala kimya kitandani, Joanitha akimwangalia kwa jicho la huruma, simanzi tele ikiwa imemjaa moyoni mwake. Moyo wake unashindwa kuvumilia, macho yake yanazingirwa na unyevunyevu. Chozi linadondoka!

Chozi la huzuni!

Deo ametulia kitandani, mwili wake ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe, isipokuwa kuanzia kifuani, bandeji inaonekana mkononi mwake. Mapigo ya moyo wake yanakwenda taratibu kabisa!

“Deo wangu…Deo…Deo jamani…amka mpenzi wangu. Naomba usife mpenzi wangu jamani. Hebu amka baby, tufunge ndoa…bado nakupenda…” akasema Joanitha akilia kwa uchungu.

Deo hakusikia kitu, alikuwa katika usingizi mzito, hajui chochote kinachoendelea. Alikuwa amepoteza fahamu na hakuwa na uwezo wa kusikia chochote.

Wasiwasi wa Joanitha ulikuwa mmoja tu; kwamba Deo akifa asingeweza tena kufunga naye ndoa, tendo ambalo alikuwa akilisubiria kwa muda mrefu sana. Joanitha akazidi kulia. Alitamani sana kuliona tabasamu la Deo.

Alitaka kuona akiongea, akimbusu, akimkumbatia na kumwambia maneno matamu ambayo amekuwa akimwambia kila wakati.

Hilo tu!

Lakini Deo hakuweza kufanya chochote kati ya hivyo. Alikuwa amelala kitandani kama mzigo, hana taarifa kama mpenzi wake Joanitha alikuwa kitandani mwake akilia.

“Basi dada yangu, mwache apumzike, usijali, huna sababu ya kulia. Atapona tu!”

“Lakini inaniuma dokta, bado wiki tatu tufunge ndoa. Tayari ndoa imeshatangazwa mara ya kwanza kanisani, bado mara mbili ili nifunge ndoa na Deo wangu, sasa itawezekanaje tena? Si ndiyo nimeshampoteza? Si tayari nimeshapoteza ndoa?” Joanitha akasema akionekana kuwa na uchungu sana.

“Hapana, hana hali mbaya, wiki tatu ni nyingi sana, kabla ya muda huo atakuwa amesharejea katika hali yake ya kawaida, bila shaka atapanda madhabahuni kufunga ndoa na wewe!”

ITAENDELEA…

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya