MWANDISHI WA PANORAMA
MMILIKI wa Kampuni ya Canghui Traders Limited ya jijini Dar es Salaam, inayojihusisha na uagizaji na uuzaji wa vifaa vya ujenzi na samani za ndani, Baosheng Ge, maarufu zaidi kwa jina la Dennis jana alifanya vitendo vya kisanii wakati akihojiwa na Tanzania PANORAMA Blog.
Baosheng Ge ambaye ni raia wa China, alipopigiwa simu kutoa ufanunuzi wa tuhuma anazoelekezewa yeye binafsi pamoja na kampuni yake, kwanza alipokea na kusalimiana na mwandishi kwa furaha kwa lugha ya kiswahili lakini baada ya mwandishi kujitambulisha na kuanza kumuuliza maswali alitoa majibu ambayo hayahusiana hata kidogo na maswali aliyoulizwa.
Katika hatua ya kushangaza, Baosheng Ge ambaye anaongea Kiswahili fasaha alisema haelewi Kiswahili huku akimtaka mwandishi kuachana na wafanyakazi na kwamba yeye anatimiza wajibu wake vizuri kwa vyombo vya habari, vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi za serikali anazohusiana nazo.
Alipotakiwa kueleza namna anavyotekeleza wajibu wake huo, alijifanya hasikii na kuanza kuita kwa sauti kubwa jina la mwandishi kama mtu ambaye hasikii anachoulizwa au kuelezwa na aliendelea kuita jina hilo kwa muda usiopungua dakika mbili kisha alikata simu na alipopigiwa tena hakujibu bali alituma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani.
Ujumbe huo ulisomeka, “hakuna mfanyakazi hadi moja kufukuzwa kazini from CANGHUI bosi ….. 2021,” na alipoelezwa kuwa mwandishi alifika mwenyewe ofisini kwake kufanya uchunguzi dhidi ya malalamiko ya wafanyakazi pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa hajafukuza mfanyakazi yoyote.
Akitumia lugha ya kimombo, aliandika; “in this year 2021, we do not have any worker has been stopped contract? You are talking about ‘mfanyakazi fukuzwa’ shocked me,” kwa tafasili isiyokuwa rasmi ‘mwaka huu 2021 hatuna mfanyakazi aliyesimamishiwa mkataba wake, unazungumzia mfanyakazi kufukuzwa, umenishtusha.’
Alipoulizwa ni mwaka gani alikuwa akiwafukuza wafanyakazi, amefukuza wangapi na kwa makosa gani, alijibu tena kwa kimombo, “That is why I fail to understand, if 5 years ago I can not remember, kwa tafasili isiyokuwa rasmi ‘ndiyo maana nashindwa kuelewa, kama ni miaka mitano nyuma siwezi kukumbuka.’
Baosheng alikanusha kuuza vigae vibovu na kupokea fedha za mauzo bila kutoa risiti na alipoelezwa kuwa mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog alifika ofisini kwake ambako kuna kamera zinazoweza kuonyesha matukio yaliyotokea ambapo ilimshuhudia mmoja wa watu aliyejitambulisha kuwa ni fundi ujenzi na kuomba auziwe vigae vibovu kwa bei ya chini na yeye alimpunguzia bei, alisisitiza kuwa jambo kama halipo.
Kampuni ya Canghui Tredars Limited inatuhumiwa kukiuka masharti ya leseni yake ya biashara, sheria za kazi na kuwakandamiza wafanyakazi wake na kwamba imekuwa ikikwepa kulipa kodi stahiki za serikali kwa kufanya kazi zilizo nje ya masharti ya leseni yake ya biashara.
Inadaiwa kuwa kampuni hiyo ambayo ipo Wilaya ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam leseni yake ni ya kutengeneza, kuagiza na kuuza vifaa vya ujenzi na samani za ndani lakini imekuwa ikichukua tenda za ukandarasi mdogo ikiwemo kufunga madirisha, milango na kuweka vigae katika majengo mbalimbali.
Hayo yote yameelezwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo (majina yao yamehifadhiwa) waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog na kudai zaidi kuwa mwajiri wao huyo anakiuka sheria za kazi kwa kutowapa wafanyakazi mikataba ya ajira, kutowasilisha makato ya fedha za pensheni za wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wafanyakazi hawapimwi afya zao licha ya kufanyakazi katika mazingira yenye vumbi hasa wanapopelekwa kwenye shughuli za ujenzi.
Alipoulizwa awali kuhusu tuhuma hizo, Baosheng Ge alimuomba mwandishi asubiri kidogo amuite msemaji wake lakini aliiacha simu hewani kwa muda mrefu hadi ilipokatika na alipopigiwa tena na tena hakupokea.