![]() |
Aifang Zhong – Ivan |
MWANDISHI WA PANORAMA
AIFANG ZHONG, maarufu zaidi kwa jina la Ivan anayemiliki kiwanda cha kuyeyusha chupa za plastiki kilichopo eneo la viwanda, Mbezi Makonde amekimbilia polisi.
Zhong alikimbilia polisi jana baada ya kupigiwa simu kuulizwa kuhusu tuhuma mbalimbali alizoelekezewa na wafanyakazi wake zikiwemo za unyanyasaji wafanyakazi na kutotoa mikataba ya ajira.
Tanzania PANORAMA Blog ilimpigia simu Zhong kuomba ufafanuzi wa ziada kuhusu idadi ya wafanyakazi alionao katika kiwanda chake na wangapi wenye mikataba na wasiokuwa na mikataba ya ajira na yeye alijibu kuwa anakwenda polisi akifika hapo atapiga simu ili polisi wasikie anachokiongea.
Robo saa baadaye alipopigiwa simu na kuulizwa kama amekwishafika polisi ili ajibu maswali aliyoulizwa alikata simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya kiganjani ulioandikwa kwa lugha ya kichina.
Tanzania PANORAMA ilimtumia maswali iliyokuwa inataka ufafanuzi kutoka kwake ambayo licha ya kuyapokea hakujibu na alipopigiwa tena aliandika ujumbe mfupi mwingine kuwa yuko polisi.
Wafanyakazi wa kiwanda cha kuyeyusha plasiki kinachomilikiwa na Ivan wamelalamika kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu, wananyanyaswa na pia hawana mikataba ya ajira.
Katika malalamiko hayo, wafanyakazi hao wameeleza kuwa kiwanda hicho kinachafua na kuharibu mazingira kwa kutupa hovyo chupa plaski zinazokusanywa mitaani kwenda kuyeyushwa kiwandani hapo na kwamba mazingira ya kiwanda hicho ni hatarishi kwa afya za wafanyakazi na hakuna mfumo wa kuhifadhi taka na maji yenye kemikali, vinavyotumika katika uyeyushaji.
Wakizungumza kwa ombi la majina yao kuhifadhiwa, walisema mwajiri wao Ivan, anawafanyisha kazi ngumu za uyeyushaji chupa kwa kutumia kemikali bila kuwapa vifaa vya kujikinga (Soksi maalumu za mikononi na viatu vigumu) na amekuwa akiwafukuza kazi bila kufuata sheria za ajira.
“Tuomba na sisi kilio chetu kisikike, tunafanya kazi katika mazingira magumu, kazi yetu hapa ni kuyeyusha chupa, tunatumia kemikali ambazo sisi hatuzifahamu majina lakini hatuna soksi za mikononi wala viatu magumu, tunashika hizo kemikali kwa mikono tu.
“Hatuna vifaa vya kuziba pua na mdomo, wenzetu wanaosafisha chupa nao hawana soksi za mikononi wakati chupa nyingine zinaokotokwa majalalani kabla ya kuja kuyeyusha hapa, wapo wenzetu waliogua kutokana na mazingira magumu ya kazi lakini waliishia kufukuzwa kazi.
“Hatuna mikataba ya kazi isipokuwa wenzetu wachache ambao nao wanashiriki kutukandamiza kwa sababu wao wapo karibu na hawa wachina na wanalipwa vizuri kidogo, hatuna pensheni, hatupimwi afya zetu. Kiukweli tunafanya kazi hapa kwa sababu hatuna namna nyingine ya kuishi lakini usalama wa afya zetu haupo na wengi tunaambulia magonjwa tu, tunaomba serikali itusikie ije ifanye uchunguzi hapa,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Aidha walisema bosi wao, Ivan amejijengea uzio wa kutoguswa kwa kujenga urafiki na baadhi ya viongozi wa eneo hilo ambao licha ya kuona chupa zinazookotwa na kupelekekwa kiwandani hapo zikitupwa hadi nje ukuta wa kiwanda na kuziba barabaraba, hakuna hatua zinazochukuliwa.
Alipoulizwa Ivan ambaye uchunguzi umebaini kuwa jina lake halisi ni Aifang Zhong alisema takataka zote nje ya kiwanda chake amekwishaziondoa lakini alishindwa kujibu malalamiko ya wafanyakazi kufanya kazi ngumu zenye kuhatarisha afya zao bila soksi za mikono na viatu vigumu.
Zhong alipobanwa alimpa simu mtu ambaye alikataa kujitambulisha jina na wadhfa wake katika kampuni hiyo ambaye alisema malalamiko yote hayo yana nia ovu na kuomba kuonana na waandishi jambo ambalo Tanzania PANORAMA ililikataa na kusisitiza kupata majibu lakini mzungumzaji huyo hakuwa tayari.