Thursday, July 17, 2025
spot_img

WINGU JEUZI LATANDA YADI YA MAGARI NAMBA 678 KURASINI

 

Vipuli vilivyotolewa kwenye magari aina ya Scania yaliyoko yadi namba 678, Barabara ya Kilwa, Kurasini kabla havipalekwa kusikojulikana

 MWANDISHI WA PANORAMA

HOFU ya wizi wa vipuli vya magari imetanda katika yadi ya magari makubwa namba 678, (Customer Bonded Ware House) iliyoko barabara ya Kilwa, Kurasini ambayo sambamba na kuhifadhi magari ambayo hajalipiwa kodi imekuwa ikitumika kama karakana.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya yadi hiyo zimeonyesha kuwa mafundi magari wamekuwa wakifungua vipuli vya magari na kuvipeleka kusikojulikana na pia wamekuwa wakiingiza vipuli chakavu kutoka nje na kuvifunga katika magari ambayo yameondolewa vipuli vyake vipya vilivyokuja na magari hayo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mafundi magari wanaohusika kuondoa vipuli katika magari yaliyo ndani ya yadi hiyo na kuvipeleka kusikojulikana kisha kuleta vingine chakavu wanatekeleza kazi hiyo kwa maelekezo ya mmiliki ya yadi aliyetajwa kwa jina la Issac Abdallah.

Inadaiwa kuwa vifaa vinavyoondolewa katika magari hayo hupelekwa kuuzwa katika maduka ya vipuli vya magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam na Kariakoo, kwenye magereji na kwa baadhi ya wenye magari makubwa ambao wanahitaji kubadili vipuli vilivyotumika kwenye magari yao kwa muda mrefu.

Kwamba, mafundi hao ambao huuza vipuli hivyo kwa bei kubwa, hununua vipuli vingine vilivyotumika muda mrefu kwa bei ya chini katika eneo la Gerezani Kariakoo na kwenda kuvifunga katika magari waliyotoa vipuli vipya.

Fundi magari akiwa juu ya moja ya magari makubwa aina ya Scania (roli) lililofunguliwa vipuli ndani ya yadi namba 678 iliyopo Barabara ya Kilwa, kurasini


“Kinachofanyika ni sawasawa na wizi kwa sababu hawa mafundi ambao Issac ndiye anayewaleta huwa wanakuja kufungua ‘spare’ mpya kwenye magari mapya ambayo yanahifadhiwa hapa kabla ya kulipiwa kodi na kuchukuliwa na wenyewe, wakifungua wanakwenda kuziuza kwenye maduka ya ‘spare’ Kariakoo au katikati ya jiji.

“Wanunuzi wengine ni wenye magereji yanayotengeneza magari makubwa na wana wateja wao pia ambao ni wamiliki wa magari makubwa ambayo yanakuwa yanahitaji ‘spare’ baada ya zilizopo kuchoko, wakishawauzia huwa wanapitia gerezani na kununua  ‘spare’ zilizochoka na kuja kuzifunga pale walipotoa mpya.

“Ndiyo maana waagizaji magari kila mara wanalia magari wanayoagiza kuwa yanakuja na vipuli vilivyochoka na au wanayakuta magari yao hayana baadhi ya vipuli, chanzo cha yote haya ni wizi unaofanyika kwenye hii yadi na Issac anajua kila kitu.

“Na tunashangaa kwa sababu yadi hii kama zilivyo nyingine kazi yake ni kuhifadhi magari ambayo hayajalipiwa kodi lakini hii sasa pamoja na kutumika kama yadi inatumika pia kama karakana, sijui sheria inasemaje katika hili,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Alipoulizwa Issac Abdallah ambaye ofisi yake ipo kwenye kona ya Barabara ya Lumumba na Mtaa wa Amani katika Jengo la Rissa Barbaque,  ghorofa ya tano, kuhusu tuhuma hizo alikiri yadi yake kujishughulisha na shughuli za utengenezaji magari mbali ya kuyahifadhi kama ulivyo utaratibu wa kawaida kwa kile alichoeleza kuwa ingawa ana leseni ya kuhifadhi magari lakini ameruhusiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kufanya shughuli za utengezaji magari ndani ya yadi hiyo.

Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa awali, Issac ambaye pia hujishughulisha na biashara ya kuuza magari alikuwa na yadi ya magari huko Sinza, Dar es Salaam akiwa na ushirika wa kibiashara na raia mmoja wa Pakistani ambaye alipata kukamatwa kwa makosa ya kukwepa kulipa kodi kabla ya kudhaminiwa na kutimka kutoka hapa nchini.

Tanzania PANORAMA Blog inaendelea na uchunguzi wa suala hili.       

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya