![]() |
Samani za ndani zinazotengenezwa na Kampuni ya Canghui Traders Limited ya Dar es Salaam |
MWANDISHI WA PANORAMA
KAMPUNI ya Canghui Traders Limited ya jijini Dar es Salaam inayojihusisha na uagizaji na uuzaji wa vifaa vya ujenzi na samani za ndani inadaiwa kukiuka masharti ya leseni yake ya biashara, sheria ya kazi na kuwakandamiza wafanyakazi wake.
Hayo yameelezwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog mapema wiki na kudai kuwa kampuni hiyo inakwepa kulipa kodi stahiki za serikali kwa kufanya kazi zilizo nje ya masharti ya leseni yake ya biashara.
Walisema kampuni iliyoko Urafiki, Wilaya ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam inayomiliki na raia wa China anayefahamika zaidi kwa jina moja la Denis, leseni yake ni ya kutengeneza, kuagiza na kuuza vifaa vya ujenzi na samani za ndani lakini imekuwa ikichukua tenda za ukandarasi mdogo ikiwemo kufunga madirisha, milango na kuweka vigae katika majengo mbalimbali.
Aidha, walidai kuwa mwajiri wao anakiuka sheria za kazi kwa kutowapa wafanyakazi mikataba ya ajira, hawasilisha makato ya fedha za pensheni za wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wafanyakazi hawapimwi afya zao licha ya kufanyakazi katika mazingira yenye vumbi na hasa wanapopelekwa kwenye shughuli za ujenzi.
Tanzania PANORAMA Blog ambayo jana ilifika katika ofisi hizo ilishuhudia mmoja wa wateja aliyejitambulisha kuwa ni fundi ujenzi akiuzuiwa vigae vilivyovunjika kwa bei ndogo alivyodai kuwa anakwenda kuvitumia kukamilishia ujenzi wa nyumba aliyochukua zabuni ya kuijenga na Denis alimpa punguzo kubwa bei.
“Huyu Mchina ndiyo kawaida yake, wanakuja hapa mafundi anawauzia vigae ambavyo ni ‘reject’ ambavyo kiuhalisia havifai kuuzwa au kwenda kutumika kujengea, anaviuza kwa bei ya chee na hatoi risiti kwenye mauzo ya aina hiyo ndiyo maana mafundi wengi wanakimbilia hapa kuja kuchukua vitu visivyokuwa na ubora na vilivyoharibika na kwenda kujengea nyumba za wateja wao. Kiukweli ana mambo mengi sana yasiyofaa,” kilieleza chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya kampuni hiyo.
Alipoulizwa Denis kupitia simu yake ya kiganjani ambayo imesajiliwa kwa jina la Baosheng Ge alimuomba mwandishi asubiri kidogo kasha amuite msemaji lakini aliiacha simu hewani kwa muda mrefu hadi ilipokatika na alipopigiwa tena na tena hakupokea.
Jitihada za kuzitafuta mamlaka za kodi na zile zinazohusika na ajira kuzungumzia mwenendo wa wafanyabiasha wanaokiuka masharti ya leseni zao na sheria za ajira zinaendelea.