![]() |
Kifaa feki kinachotumika katika mashine ya kukata vigae ambacho kimenunuliwa katika duka la Khambhalai |
NA MWANDISHI WA PANORAMA
MFANYABIASHARA Fakhruddin Khambhalia wa jijini Dar es Salaam anadaiwa kuingiza nchini bidhaa bandia zenye nembo ya Kampuni ya Makita Corporation ya Japan.
Khambhalia anadaiwa kuingiza bidhaa hizo kutoka China zikiwa zimetengezwa kwa ubora duni na kuziuza kwa bei ya chini na kwamba anafanya hivyo huku akijua yeye siyo wakala wa Kampuni ya Makita Corporation Japan.
Bidhaa hizo ni pamoja na vifaa vya umeme, vifaa vinavyotumika kutengeneza au kuunda vifaa vya ujenzi na zana mbalimbali za matumizi anuai ya shughuli za majumbani ikiwa ni pamoja na vifaa vya kukatia majani.
Madai hayo yametolewa na Mfanyabiashara Adamu Ntobi wa jijini Dar es Salaam aliyeiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa amenunua bidhaa katika duka la Khambhalai lilipo eneo la Gerezani, Kariakoo akiamini kuwa ni halisi lakini baada ya kuichunguza aligundua kuwa siyo halisi.
“Mimi nilielekezwa kwenye duka la huyo bwana na jamaa yangu baada ya kumkuta akiwa na bidhaa za Makita, hizo bidhaa ni imara na zina bei sasa nilipomkuta nayo na aliponiambia bei nikaona ya chini kabisa, nikaamua kwenda hapo kununua.
“Wakati nanunua sikuichunguza sana kwa sababu niliamini ni bidhaa halisi lakini baada ya kuitumia kwa muda mfupi tu ikakorofisha, sasa wakati nachunguza kilichokorofisha ndiyo nikagundua siyo bidhaa ya Makita wenyewe wa Japan bali hizi zinatengenezwa China.
“Nikaamua kurudi kwenye lile duka pale Gerezani nikamuuliza kijana aliyeniuzia mbona bidhaa yao ni Makita China badala ya Makita Japan akasema kuna viwanda vingi lakini nilipokaa naye chembe ndiyo akanambia ukweli kuwa bosi wao huwa anachukua bidhaa halisi za Makita anazituma China anatengezewa za bandia.
“Yule kijana alinambia huko China huwa zinatengezwa mtaani kwa bei nafuu na ndiyo maana zikija hapa zinauzwa kwa bei ya chini tofauti na zile halisi zinazotengezwa Japan ambazo bei yake ni aghali na hizo yupo wakala wao hapa mjini ila sijui yupo wapi,” alisema Ntobi.
Alipotafutwa Khambhalai, simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu yake ya mkononi hakujibu.
![]() |
Jengo la Makao Makuu ya Kampuni ya Makita Corporation lililopo Japan |
Kampuni ya Makita Corporation makao yake yapo Sumiyoshicho Anjo Aichi nchini Japan na ilianzishwa mwaka 1915 ikijihusisha na utengenezaji na uuzaji wa vifaa vya umeme wa magari na pia kufanya matengenezo na baadaye ilijipanua shughuli zake kwa kuongeza zaidi bidhaa mbalimbali inazozalisha.
Makita Corporation ina matawi katika nchi 30 duniani na nchini Japan ina matawi 35 na inasifika kwa kutengeneza bidhaa zenye ubora usiokuwa wa kutiliwa shaka.