Thursday, September 11, 2025
spot_img

MWAJUMA ALIYEJITWALIA MAMILIONI YA FEDHA ZA BIMA YA KIFO YA BAHARIA ALIYEFIA ITALIA ANAWEZA KUSHTAKIWA

 

Mwanasheria mbobezi wa sheria za mirathi na utatuzi wa migogoro ya dhuluma kwa warithi wa mali za marehemu, Aloyce Komba 

MWANDISHI WA PANORAMA

MWAJUMA Zawayai, dada yake marehemu Yusuph Dali aliyefikwa na umauti April, 2019 kwa kugongwa na gari nchini Italia, anaweza kushtakiwa mahakamani iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa alijinufaisha na mali ya marehemu.

Hayo yameelezwa na mtaalamu wa sheria za mirathi na utatuzi wa migogoro ya dhuluma kwa warithi wa mali za marehemu, Wakili wa Kampuni ya Haki Kwanza ya Dar es Salaam alipokuwa akitoa uchambuzi wa kitaalamu kuhusu taratibu za kisheria zinazompa mtu mamlaka ya kusimamia na kugawa mirathi ya marehemu.

Mwajuma anadaiwa na ndugu zake kujitwalia mabilioni ya fedha za bima ya kifo cha marehemu Yusuph Dali, zilizolipwa na mamlaka za Italia huku akiwa hana mamlaka ya kisheria ya kusimamia na kugawa mirathi na kwamba aliwagawia kidogo baadhi ya ndugu anaowapenda huku wengine akiwanyima.

Mwanasheria Komba ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa mirathi, sura ya 352, kifungu cha 108 kinampa msimamizi wa mirathi majukumu kadhaa yakiwemo ya kutafuta, kukusanya na kusimamia mali yote ya marehemu na madeni, kulipa madeni kwa wadai na gharama ya usimamizi.

Alifafanua kuwa vifungu vya 100 hadi 113 vinafafanua uwakilishi wa kisheria wa usimamizi, mamlaka ya kushtaki au kushtakiwa, mamlaka ya kuuza mali, mamlaka ya matumizi ya fedha ya marehemu kwa maslahi ya warithi wote.

Mwajuma Zawayai


“Kisheria mwenye mamlaka ya kugawa na kusimamia mali isiyogawiwa ni msimamizi wa mirathi ndani ya miezi sita hadi mwaka mmoja akishapewa hati za usimamizi na mahakama. Kukiwa na ushahidi wa mtu kujinufaisha na mali ya marehemu anashtakiwa,” alisema Mwanasheria Komba.

Mwanasheria Komba ametoa ufafanuzi huu wa kisheria ikiwa tayari mtaalamu wa masuala ya Bima, ambaye ni Mkurugenzi Mratibu Kanda wa Shirika la Bima Zanzibar, Ali Makame kutoa ufafanuzi wa sheria ya bima ya kifo.

Makame alieleza kuwa sheria inaelekeza Bima na kifo kulipwa katika akaunti ya mirathi iliyoko Hazina na Hazina ndiyo hugawa fedha hizo kwa warithi na kwamba utaratibu huo ndiyo unaotumika kwa bima za aina hiyo zinazolipwa nchini au nje ya nchi.

Inadaiwa, Mwajuma akiwa hana mamlaka yoyote ya kisheria alidai na kulipwa bima ya kifo ya marehemu Yusuph Dali nchini Italia na kuigawa kwa mujibu wa matakwa yake.  

Mwajuma mwenyewe amekuwa akikataa kutoa ushirikiano wa kueleza anachokijua kuhusu malipo ya bima ya marehemu Dali hata hivyo jana alijibu maswali machache aliyoulizwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu huku akikataa kujibu mengine na kuwaalika baadhi ya watu waliodai ni ndugu zake kuwasiliana na Tanzania PANORAMA kuitaka isitishe kufuatilia suala hilo.

Inadaiwa Marehemu Yusuph Dali, Mtanzania aliyekuwa akijishughulisha na ubaharia alifariki dunia April, 2019 baada ya kugongwa na gari nchini Italia na mwili wake alisafirishwa mwezi mmoja baadaye kurejeshwa nchini na kwenda kuzikwa mkoani Lindi.

Kwamba wakati wa uhai wake, marehemu Dali alimuita Mwajuma kwenda Italia kutafuta maisha lakini walifarakana muda mfupi baadaye kwa sababu marehemu hakupendezwa na aina ya maisha ya dada yake huyo pamoja na magenge aliyokuwa akiandamana nayo hivyo kila mmoja alishika njia yake.

Inadaiwa zaidi kuwa baada ya kifo cha marehemu Dali, Mwajuma ambaye alikuwa bado nchini Italia alihusika katika madai ya bima akisaidiwa na watu ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu hawajapatikana kuzungumza na baada ya kukamilisha taratibu muhimu za madai hayo ndipo mwili wa marehemu ulisafirishwa kuja nchini, ikiwa ni mwezi mmoja tangu alipofariki.

Kwamba Mwajuma hakusafiri na mwili wa marehemu kaka yake kutoka Italia kwa ajili ya kuja kuuzika nyumbani bali alibaki huko akipambana kupata malipo ya bima ya kifo cha Yusuph na baada ya kuyapata, alirejea nchini na kuwagawia baadhi ya ndugu huku kiasi kikubwa cha fedha akikitia kibindoni na kuwanyima ndugu wengine.

Mwajuma aliieleza Tanzania PANORAMA kuwa mgao wa fedha alizopata katika malipo hayo ya bima ya marehemu baharia Yusuph aligawana na wenzake na wengine wamfuate mtoto wa marehemu.

Lakini kabla ya Mwajuma kutoa majibu hayo, Tanzania PANORAMA ilipigiwa simu na mchezaji mpira wa zamani, Iddi Pazi ambaye alijitambulisha kuwa kaka wa marehemu na kuhoji kwanini anafuatiliwa na kuonya kuwa iwapo hali hiyo itaendelea asilaumiwe mtu.

Baadaye mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zawayai naye aliipigia simu Tanzania PANORAMA Blog akieleza kuwa amefikishiwa malalamiko na dada yake Mwajuma kuwa mtu kuna anafuatilia maisha yake hivyo aingilie kati kumsaidia na Tanzania PANORAMA ilimjibu kuwa anachoulizwa Mwajuma ni maswali mepesi ya kawaida yenye lengo la kumpa nafasi ya kuzungumzia au kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma na madai anayoelekezewa.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya