Thursday, September 11, 2025
spot_img

KAMPUNI YA USAFI LEDSO YAFANYA USANII HATARI

 

Taswira ya uongozi wa juu wa Kampuni ya Ledso Consolidated limited

MWANDISHI WA PANORAMA

KAMPUNI ya Usafi ya Ledso Consolidated Limited ya jijini Dar es Salaam inayodaiwa kuwa na mazingira magumu ya kazi, kukiuka sheria za ajira na kuwashughulikia kwa nguvu zisizoonekana watu wanaofuatilia mwenendo wake usioridhisha, inaendeshwa kisanii.

Tanzania PANORAMA Blog imethibitisha pasipo shaka kuwa kampuni hiyo inaendeshwa kisanii katika uchunguzi wake dhidi ya madai ya wafanyakazi hao baada ya mmiliki wake, Leyla Sosovela kukana kuimiliki na kukana namba yake ya simu alipopigiwa wiki iliyopita ili kutoa ufafanuzi wa madai ya wafanyakazi hao.

Pamoja na hilo, mmiliki wa kampuni hiyo, Leyla ambaye alishindwa kujibu maswali aliyoulizwa baada ya kusakwa hadi alipopatikana na kubanwa, alitoa majina ya watu wasiokuwa wafanyakazi wa kampuni yake hiyo na kudai kuwa ni wafanyakazi na kwa nyadhifa walizonazo ndiyo wasemaji wa Ledso.

Mapema wiki iliyopita, Leyla Sosovela alipotafutwa na Tanzania PONORAMA kupitia simu yake ya kiganjani ya mtandao wa tigo iliyo kwenye maelezo ya mtandaoni ya kampuni anayoimiliki na kuulizwa kuhusu tuhuma inayoelekezewa, alisema haijui Kampuni ya Usafi ya Ledso Consolidated Limited, hana kampuni wala hajawahi kumiliki kampuni toka azaliwe na wale yeye siyo Leyla Sosovela.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA katika mtandao wa tigo ulibaini kuwa simu hiyo ni ya Leyla Sosovela na uchunguzi zaidi uliofanywa kuhusu mmiliki wa Kampuni ya Ledso Consolidated Limited na uthibitisho kutoka kwa wafanyakazi vilionyesha pasipo shaka kuwa yeye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo.

Baada ya hayo kubainika, Tanzania PANORAMA ilimsaka Leyla hadi ilipofanikiwa kumpata na kumuuliza pamoja na tuhuma na madai ya wafanyakazi wake, ni kwanini anajikana mwenyewe, anaikana kampuni yake, anaikana namba yake ya simu na kwanini anasema uongo lakini alishindwa kujibu chochote isipokuwa alitoa namba ya simu ya mtu aliyemtaja kwa jina la Hamisi aliyedai kuwa ni mwanasheria wa kampuni yake na kuomba atafutwe ili azungumze kwa niaba yake.

Alipotafutwa Hamisi ambaye uchunguzi wa awali umebaini kuwa jina lake ni Hamisi Mohamed alikiri kuwa mwanasheria wa Kampuni ya Ledso na kuomba apewe maswali akayafanyie kazi pamoja na kuwasiliana na mteja wake kabla ya kuyajibu na kwamba muda huo alikuwa mahakamani, jambo ambalo lilifanyika.

Alipotafutwa baadaye alisema anachojua kuhusu wafanyakazi wa Kampuni ya Ledso, wote wana mikataba ya mwaka mmoja kwa sababu kampuni hiyo kazi zake ni za mkataba wa mwaka mmoja tu.

Alipoulizwa kuhusu madai ya wafanyakazi kufanyishwa kazi katika mazingira magumu na mwajiri kukiuka sheria za ajira alisema anaomba muda zaidi wa kuwasiliana na mteja wake kabla hajatoa ufafanuzi wa madai hayo lakini katika hatua ya kushangaza alipopigiwa tena na tena ili kutoa ufafanuzi kama alivyoahidi hakupokea simu.

Alipotafutwa kwa mara nyingine Leyla na kuelezwa hilo aliitaka Tanzania PANORAMA kuachana na mwanasheria Hamisi na kutoa namba ya simu ya mtu aliyemtaja kwa jina moja la Robby aliyedai kuwa ni Meneja Rasilimali Watu wa kampuni yake kuwa ndiye mwenye majibu yote ya uhakika.

Alipopigiwa Robby ambaye Tanzania PANORAMA imebaini jina lake kamili ni Robert Kisaka naye aliomba muda ili awasiliane kwanza na mwajiri wake kabla ya kuzungumza jambo lolote na baada ya muda mfupi alipiga simu na kueleza kuwa madai yote ya wafanyakazi hao hayana msingi.

“Mama anasema madai hayo yote hayana msingi, sikiliza bwana mwandishi mimi sasa nakuhakikishia mama yupo vizuri kwenye kila kitu kwa sababu mikataba ipo, makato ya pensheni anawapelekea wafanyakazi, afya zao wanapimwa, WCF cheti anacho, hilo la kubadili jina la kampuni halipo kwa sababu yeye kampuni aliyonayo na aliyowahi kumiliki ni hii tu ya Ledso, halafu hilo la nguvu zisizoonekana ninyi mnaweza kulithibitisha wapi?” alisema Kisaka.

Alipoulizwa kuhusu madaia ya ukwepaji kodi alisema hilo aliulizwe bosi wake na alipoulizwa idadi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wenye mikataba ya ajira alishindwa kujibu.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo waliohojiwa na uchunguzi wa kina wa Tanzania PANORAMA umebaini kuwa kampuni hiyo haina Meneja Rasilimali Watu anayeitwa Robert Kisaka au Robby na ilisisitizwa na wafanyakazi kuwa anachokifanya mwajiri wao ni usanii ambao iwapo serikali itafanya uchunguzi wa kina itabaini jinsi asivyokuwa mkweli.

“Hao watu hawapo kabisa, huyo HR hayupo Ledso atakuwa katafuta mtu mtaani ili aseme uongo, uchunguzi ukifanyika hapa yatabainika mambo mengi mbona. Huyo mama alikuwa na kampuni zamani anajua mwenyewe kwanini aliifuta na mimi mwenyewe nilisafiri naye sana mpaka Iringa na yeye anajua na kama anabisha nipo nitatoa ushahidi,” alisema mmoja wa wafanyakazi wanaolalamika.

Awali, wafanyakazi wa Kampuni ya Usafi ya Ledso Consolidated Limited walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan atume wasaidizi wake kwenye kampuni hiyo wakasikilize malalamiko yao na kuyatafutia ufumbuzi

Hayo waliyasema wakati wa mahojiano yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam walipoeleza kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu na kwamba mwajiri wao amekuwa akikiuka sheria za ajira kwa muda mrefu lakini wanashindwa kujitokeza hadharani kueleza matatizo yao kwa sababu ya woga.

Walitaja baadhi ya kero wanazokutana nazo katika mazingira yao ya kazi kuwa ni pamoja kufanya kazi ngumu za usafi pasipo kupimwa afya zao, kutokuwa na mikataba ya ajira, kutokuwa na malipo na pensheni na kufukuzwa kazi kinyume cha taratibu na sheria za kazi.

Tanzania PANORAMA inaendelea na uchunguzi ili kubaini, pamoja na mambo mengine ukweli wa madai ya wafanyakazi hao.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya