Thursday, July 17, 2025
spot_img

WAFANYAKAZI KAMPUNI YA LEDSO WAOMBA HURUMA YA RAIS SAMIA

 

Rais Samia Suluhu Hassan

MWANDISHI WA PANORAMA  

Wafanyakazi wa Kampuni ya Usafi ya Ledso Consolidated Limited iliyopo jijini Dar es Salaam wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan atume wasaidizi wake kwenye kampuni hiyo wakasikilize malalamiko yao na kuyatafutia ufumbuzi

Wakizungumza leo na Tanzania PANORAMA jijini Dar es Salaam, wamesema wanafanya kazi katika mazingira magumu na kwamba mwajiri wao amekuwa akikiuka sheria za ajira kwa muda mrefu lakini wanashindwa kujitokeza hadharani kueleza matatizo yao kwa sababu ya woga.

Walitaja baadhi ya kero wanazokutana nazo katika mazingira yao ya kazi kuwa ni pamoja kufanya kazi ngumu za usafi pasipo kupimwa afya zao, kutokuwa na mikataba ya ajira, kutokuwa na malipo na pensheni na kufukuzwa kazi kinyume cha taratibu na sheria za kazi.

“Tunajua Mheshimiwa Rais ni mama na anasoma mitandao kwa sababu mara kadhaa tumemsikia kwenye hotuba zake anasema kuwa anasoma mitandao. Sisi wafanyakazi wa Ledso Consolidated Limited tuna malalamiko dhidi ya kampuni yetu, tunaonewa na tunafanya kazi katika mazingira magumu sana, tunaomba atume wasaidizi wake waje watusikilize.

“Wakija wakatusikiliza pia wafanye uchunguzi wao, watajua tatizo lilipo, wala hatusemi kwa majungu wala hatutaki upendeleo na tumeamua kuja kwenu kwa sababu hatuna namna ya kumfikia ila kwake ni rahisi kujua shida zetu sisi Watanzania wake kwa kusoma kupitia kwenu waandishi.

“Mimi hapa nina zaidi ya miaka miwili kazini lakini sina mkataba wa kazi, sijawahi kupimwa afya yangu, sina pensheni yoyote, tupo wafanyakazi zaidi ya 300 fikiria serikali inakosa pesa kiasi gani ambazo ingepata kutoka kwenye mishahara yetu na tumekuwa lakini ni woga kwa sababu bosi siyo mtu wa mchezo, ana imani ile nyingine hivyo kuumia ni rahisi ndiyo maana tunaomba mama atume watu wake waje waongee na sisi.

“Kwanza hii kampuni imebadilishwa jina, huyu bosi ana zabuni nyingi sana za taasisi za serikali na hizo zabuni sisi tunajua anazipataje, waje viongozi tutawaambia na wao watachunguza watajua ukweli.

Alipoulizwa mkurugenzi wa kampuni hiyo kupitia simu ya kiganjani ambayo imesajiliwa kwa jina la Leila Sosovela iliyopo kwenye taarifa za mtandaoni za kampuni hiyo alikana kujua lolote kuhusu kampumi hiyo na kueleza kuwa yeye hana kampuni.

Tanzania PANORAMA inaelendelea na uchunguzi ili kubaini, pamoja na mambo mengine. ukweli wa madai ya wafanyakazi hao.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya