![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa WWF, Marco Lambertini |
RIPOTI MAALUMU (6)
Chimbuko la ripoti hii ambayo Tanzania PANORAMA Blog imekwishaitoa sehemu tano ni hekaheka za wazungu kutaka kuzuia mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji.
Hekaheka hizo ziliwainua wataalamu bingwa wa kitanzania wanaotambulika na jumuiya za kimataifa kwa usomi wao kufanya utafiti dhidi ya fitna na uzushi uliokuwa na lengo la kukwamisha mradi huo.
Magwiji hao wazalendo walifanyia utafiti hoja zote za wazungu zilizolenga kukwamisha jitihada za Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi huo na kuandika ripoti hii ya kina na ya kitaalamu inayojibu upotoshaji wao.
Hii ni sehemu ya sita ya ripoti iliyofanyiwa utafiti wa kitalaamu kuhusu hofu, majibu ya hofu, athari za mazingira, mipango ya kudhibiti athari za mazingira, faida baki za Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na unafuu wa gharama za umeme kwa Taifa la Tanzania baada ya mradi huo kuanza kufanya kazi.
SALEH PAMBA, DK. ABUBAKAR RAJABU, *ABDULKARIM SHAH* DK. MAGNUS NGOILE NA DK. THOMAS KASHILILAH
![]() |
Dk, Thomas Kashililah |
Ripoti hii ni andiko lililoandaliwa na wataalamu bingwa wa uchumi
na hifadhi za mazingira juu ya wasiwasi ulioibuliwa na taasisi za kigeni za kimataifa (wazungu) kuhusu uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kujenga Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere kwenye eneo dogo ndani ya Pori la Akiba la Selous, ambalo ni sehemu ya mapori ambayo ni Urithi wa Dunia.
Ripoti hii inasisitiza sababu za mradi huo kutekelezwa na faida kubwa zitakazopatikana utakapoanza kutekelezwa pamoja na changamoto za mbeleni.
Watafiti bingwa katika utafiti wao walizingatia kila aina ya wasiwasi ulioibuliwa na wapingaji wa mradi (wazungu) na sera mbadala zinazoweza kujibu wasiwasi huo na hivyo kujibu hofu zote zilizoibuliwa dhidi ya mradi.
Katika matokeo ya utafiti, watafiti bingwa wanaeleza kinaga ubaga kuwa sababu zilizotajwa na mashirika ya kimataifa (wazungu) kupinga mradi huo hazina ukweli wowote unaoonekana ambao ungeitaka Serikali kufikiria upya uamuzi wake, hivyo wanakubaliana na Serikali kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Bwana la Julius Nyerere (Stigler’s.)
Ripoti inaeleza kuwa, uamuzi uliochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli ndiyo sahihi zaidi na hakuna njia mbadala ambayo itawahakikishia Watanzania, wawekezaji na wadau wengine umeme wa bei nafuu, wa uhakika na endelevu unaofikia megawati 2115.
![]() |
Muonekano wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakapokamilika |
4.1 MAJIBU KWA DUKUDUKU ZILIZOONYESHWA NA WWF
Shirika la Wanyamapori Duniani (WWF) lililalamika juu ya uwezekano wa mafuriko kufunika makazi ya viumbehai yaliyoko nchi kavu kutokana na bwawa kubwa litakalofunika eneo la kilometa za mraba 1,200.
Waliongelea athari za mlolongo wa mabadiliko yatakayotokea kwenye sehemu za chini za mto. Mfano walitaja mabadiliko ya kimsimu katika ujazo wa maji yanayotiririka kama yakipimwa katika meta za ujazo wa maji yanayotiririka kwa mwaka.
Walitaja pia, athari za mabadiliko ya kimsimu katika ujazo wa mashapo kama yakipimwa katika tani zinazosombwa na mto kwa mwaka. Walisisitiza kuwa mabadiliko haya huenda yakasababisha mabadiliko katika Jiomofolojia ya njia za mto, upunguzaji wa Bayoanwai ya majini na kupungua kwa huduma za mfumo wa Ikolojia kwa viumbe ambavyo vina makazi nusu ya chini ya mto.
Hoja yao ilikuwa kwamba kwa kuwa kiasi cha maji na mashapo yanayopelekwa baharini ni sababu kuu zinazodhibiti michakato ya Kiikolojia katika Pwani, kwenye Delta, kwenye maji ya bahari, pamoja na mazingira ya ukanda wa Pwani, basi mito inachukuliwa kama kiunga kikuu kati ya mabara na bahari, ambacho hutekeleza jukumu muhimu katika michakato ya Kijiolojia, Kibaolojia na Kemikali kwenye uso wa ardhi.
Katika mazingira haya, wazungu waliashiria usafirishaji wa maji na usafirishaji wa mashapo katika mito huathiri sana Jiomofolojia ya njia za mito, Nyanda za Delta, na hupeleka mashapo mengi kutoka nchi kavu kwenda bahari ambavyo kwa pamoja hudumisha mazingira ya Kiikolojia yaliyoko Pwani na baharini.
Wazungu hawa waliashiria tena kuwa katika karne iliyopita, mifumo mingi ya mito ulimwenguni ilipata mabadiliko makubwa kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli kubwa za kibinadamu zilizojumuisha mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kanuni za mito, uondoaji wa maji, uharibifu, na uchimbaji mchanga.
Kwa hivyo walionekana kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kisayansi na wa kimazoea kuelewa mabadiliko ya mifumo ya mito na kutathmini sababu zinazoweza kudhibiti mabadiliko hayo kwani uchambuzi wa kimahesabu kuhusu mabadiliko ya msimu katika eneo la Kijiografia unaweza kutoa rejea nzuri ya kupunguza mafuriko, kuboresha mkondo wa mto na usimamizi bora wa bonde la mto katika siku zijazo.
Kwa kifupi, WWF walionyesha wasiwasi juu ya uhusiano kati ya ukubwa wa bwawa na eneo la mafuriko yanayoweza kutokana na ukubwa huo; athari za miundombinu ya mradi; idadi kubwa ya wafanyikazi wa mradi; athari za mradi katika usafirishaji wa mashapo na madhara yake kwa Mofolojia ya mto; na mambo anwai yanayohusiana na ubora wa maji.
![]() |
Makazi ya watu ndani ya Nyanda za Delta ambayo yamekuwepo kwa miongo mingi |
Hoja hizi zilizotolewa na WWF zimetafitiwa na hapa chini tunatoa majibu yetu ya kitaalamu ikiwa ni pamoja na mitazamo sahihi ya kisera kama majibu kwao.
HOJA YA WWF: Kupungua kwa viumbe hai vya majini na nje ya bwawa. Hoja ni kwamba spishi zingine zinategemea kuhama hama kupita Bwawa la Stiegler’s na zingezuiwa na bwawa lenye kasi ndogo ya mtiririko wa maji unaobadilika badilika.
MAJIBU YETU: Bwawa linaruhusu kupitisha idadi kubwa ya samaki. Hapo awali kunaweza kuwa na ucheleweshaji wa kupita lakini baadaye kutakuwa na kupita kwa samaki chini ya mkondo bila kukoma.
HOJA YA WWF: Jamii ya samaki iliyobadilishwa katika eneo la Hifadhi ya Rufiji. Hifadhi itatoa makazi kwa spishi tofauti (na labda zisizo za asili). Jumla ya viumbehai inaweza kuongezeka na kuipita idadi ya awali na spishi za mito zinaweza kuhamishwa. RUBADA wanazungumzia tani 3,700 kwa mwaka kama mavuno ya kudumu na tani 20,000 kwa mwaka kama mavuno ya awali haswa kwa samaki jamii ya Tilapia.
MAJIBU YETU: Idara ya Uvuvi itatoa mwongozo na uwezo wa kusimamia hali wakati wa hatua za mwanzo za operesheni. Serikali ina uwezo wa kudhibiti vitendo vya uvuvi kama ilivyokuwa ikifanywa mahali pengine nchini kama vile huko Ziwa Victoria nk.
![]() |
Ziwa Victoria |
HOJA YA WWF: Uwekaji wa mashapo juu ya bwawa. Kiasi kikubwa cha mashapo kitatulia ndani ya mto mara tu kasi ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji itakapopungua na hivyo kutengeneza kero za kimazingira na athari za maji kujaa kwa kurudi yalikotoka.
MAJIBU YETU: Mto utakuwa na mashapo kidogo kwa sababu sehemu kubwa ya mto hupita kwenye misitu minene ambayo huhifadhi maji safi na mzigo mdogo wa mashapo. Walakini, gharama ya kuondoa mashapo haizidi ile ya kuzalisha umeme na mafuta.
HOJA YA WWF: Ongezeko la wadudu na mimea inayovamia maji. Madini na viinilishe baki vitakavyoingia kwenye bwawa vinaweza kusababisha kuzaliwa kwa mimea kama vile mwani inayofunika uso wa maji na kuzuia uwezekano wa uvukizi wa maji.
Pia kuna uwezekano wa uvamizi wa wadudu wanaoshambulia mimea ya majini. Mambo haya yanaweza kusababisha tatizo katika kusimamia ubora wa maji ya bwawa na shida za utendaji katika kuendesha kituo cha umeme wa maji.
MAJIBU YETU: Kiwango cha viinilishe vya majini kitapungua kwa sababu ya shughuli za kuhifadhi mazingira katika mkondo wa juu wa mto kupitia programu kama vile REGROW na SAGCOT.
Pia viinilishe vingi vitanaswa na mabwawa yaliyoko sehemu ya juu ya mto pamoja na ardhi oevu ya Kilombero. Mimea inayovamia inaweza kuvamia hifadhi lakini Serikali inaweza kuanzisha mimea mikubwa ili kukabiliana nayo na kwa hivyo hifadhi itatunzwa mara kwa mara.
HOJA YA WWF: Utengenezaji wa matabaka ya maji katika bwawa na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Ikiwa utengenezaji wa matabaka ya maji katika bwawa utatoka bwawa litazalisha Hewa ya Ukaa na Hewa ya Methane kwa viwango vya juu kuliko mifumo ya Ikolojia ambayo inachukua nafasi yake.
MAJIBU YETU: Athari za kujitokeza matabaka ya maji katika bwawa ni ndogo. Uzalishaji wa Hewa ya Ukaa utakuwa mdogo kwa sababu vichaka katika eneo ambalo litafunikwa na maji ya bwawa vitafyekwa kabla ya kujaza maji katika bwawa.
HOJA YA WWF: Ubora wa maji. Katika mazingira maalumu ubora wa maji unaweza kuharibiwa na uchafuzi wa mito unaotokea kuanzia kandoni mwa mto kwa njia ya upepo, au mmomonyoko wa mchanga, kwa mfano ule uliobeba zebaki.
MAJIBU YETU: Hakuna vitisho dhidi ya ubora wa maji katika Ruaha / Rufiji, Bonde la Mto. Mabaki ya zebaki yanaweza kutokea katika maeneo ambayo kuna Madini ya Dhahabu ya kawaida. Kwa hali hiyo hakuna Madini ya Dhahabu katika Bonde la Ruaha / Rufiji.
![]() |
Eneo la uso wa maji katika Hifadhi ya Taifa Ruaha |
HOJA YA WWF: Uvukizi. Eneo kubwa la uso wa maji huongeza viwango vya uvukizi; ukubwa wa maji yaliyovukizwa itakuwa na madhara makubwa.
MAJIBU YETU: Kutakuwa na uvukizi zaidi, ambao hauwezi kusababisha madhara kwa Ekolojia ya eneo hilo; kwa hivyo ukubwa wa maji yaliyovukizwa haitakuwa tishio.
HOJA YA WWF: Mmomonyoko wa upepo wa mwambao. Matope makubwa na matuta ya mchanga wakati wa kiangazi yanaweza kusababisha dhoruba za vumbi.
MAJIBU YETU: Bustani zitafunika sehemu kubwa ya eneo lenye matope kwani kutakuwepo na bustani za mboga mboga, pamoja na mazao ya kudumu na ya msimu. Wazo la kufunuliwa kwa matope hayatakuwa muhimu kwani eneo lenye kilimo cha umwagiliaji litakuwa pana na karibu mwaka mzima kutakuwa na kifuniko cha mimea kwenye uso wa nchi.
HOJA YA WWF: Uharibifu wa makazi ya viumbe wa nchi kavu. Kwa kulinganisha kilometa za mraba 1,200 ambazo ni makazi ya wanyamapori ni kubwa kuliko mbuga nyingi za kitaifa za Tanzania.
Bayoanwai ya ardhi na wingi wa wanyama ni kubwa kwa sababu zifuatazo: uanwai wa miundo ya makazi hayo; upatikanaji wa chakula na maji; na uwanda mkubwa na umbali kutoka kwenye bwawa.
Selous hutoa makazi muhimu ulimwenguni kwa spishi zenye haiba na zilizo hatarini; hakuna habari juu ya vitisho vinavyoweza kuzikumba spishi zilizo wenyeji katika eneo la mradi.
MAJIBU YETU: Kwa kulinganisha, sio kweli kwamba kilometa za mraba 1,200 ni kubwa kuliko Hifadhi nyingi za Kitaifa za Tanzania. Kwa hivyo, mradi hautabadilisha sana sifa za Selous.
Pia mradi utaongeza maumbo mengine ya ardhi katika Selous ambayo yatasaidia wanyama wa majini. Lakini juhudi za sasa za kuhifadhi wanyamapori zimeonyesha matokeo mazuri na kuongezeka kwa idadi ya Tembo na spishi zingine.
HOJA YA WWF: Kuongezeka kwa wawindaji haramu. Ujangili unawezeshwa na uwezekano wa kufika katika hifadhi ya akiba na kuingia ndani ya hifadhi unaotokana na uwepo wa barabara za kudumu na za muda mfupi.
Wawindaji haramu bado wanatumia njia zilizoundwa na watafutaji wa mafuta mnamo miaka ya 1970. Barabara kuu ya kufika katika hifadhi inatarajiwa kuwa na urefu wa kilomita 120 kuanzia Chalinze.
MAJIBU YETU: Uwepo wa miradi ya kiwango kama Bwawa la Umeme wa Stiegler’s itahitaji usalama wa hali ya juu kama ilivyo kwa mali kama hiyo nchini na mahali pengine. Kwa hivyo, kuelezea kuongezeka kwa idadi ya majangili kwa sababu ya barabara iliyopendekezwa ya lami kwenda kwenye Bwawa inaweza kuwa haina maana kama hali ilivyo.
Bwawa litavutia usalama mzito ndani na karibu na hifadhi ambapo kupitia mfumo huu wa usalama utaratibu wa kuingia na kutoka kwenye hifadhi utasimamiwa. Hakika, kutakuwa na usalama wa aina yake kwa ajili ya Bwawa na Pori la Akiba.
Kwa hivyo tishio la ujangili litakabiliwa kwa kiwango kikubwa. Hii inawezekana kutokana na uzoefu wa mabwawa ya umeme nchini ambapo mipango ya usalama imekuwa ya aina yake. Pia kuna kitengo kipya cha TAWA cha kupambana na ujangili. Kwa kumalizia, hebu tuulize: ni wapi duniani ambao majangili hutumia barabara nzuri?
HOJA YA WWF: Shinikizo la muda kwa wanyama pori na misitu kutoka kwa wafanyakazi wa ujenzi na watu wanaoweka kambi porini. Ikiwa kambi hazina uzio na kwa kuangalia wingi wa wafanyikazi katika mradi huu basi wafanyakazi hawa na watumiaji wa kambi watatumia maliasili zilizo katika hifadhi.
![]() |
Shughuli za ujenzi wa Bwana la Kufua Umeme la Julius Nyerere zinazoendelea zinazingatia tahadhali zote za kitaalamu kulinda wanyama na mazingira |
MAJIBU YETU: Makambi yatakuwa na uzio yakiwa yamejengwa ndani ya hifadhi katika namna ambayo inazuia watumiaji wa makambi kuzagaa kwenye hifadhi; kutakuwepo na matumizi ya gesi na umeme kwa wafanyakazi wanaotoa huduma za kijamii katika mradi. Serikali imeajiri walinzi wa kutosha kushika doria wakati wa ujenzi wakilenga kulinda wanyamapori.
HOJA YA WWF: Uharibifu wa mazingira unaofanyika kwa njia ya kutifua ardhi na hasa kutokana na utengenezaji wa barabara, njia za mawasiliano, kambi, maeneo ya viwanda, machimbo ya kokoto na malundo ya mchanga.
Kufungua eneo la viwanda kunaweza kusababisha uharibifu wa mazingira unaofanyika kwa njia ya kutifua ardhi kwa kiwango kikubwa ambayo inaweza kuchukua miongo kadhaa kukarabatiwa na hasa katika misitu mikavu na kwenye mazingira ya Savanna.
MAJIBU YETU: Shughuli za kutifua ardhi zinazojulikana ndani ya SGR zitakuwa chini ya usimamizi wa mpango mkuu wa usimamizi wa hifadhi pamoja na hatua za kupunguza madhara zilizoainishwa katika ESMP ambayo ni sehemu ya ESIA ya mradi huo.
HOJA YA WWF: Uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kuzalisha harufu mbaya, kelele, taka ngumu na maji machafu. Vikosi vya wajenzi, mashine, kambi zinaweza kufanya uchafuzi mwingi wa mazingira.
MAJIBU YETU: Uchambuzi wa athari na mipango ya udhibiti wake katika hatua za awali, wakati wa ujenzi, operesheni za kijenzi na kufunga mradi tayari zimezingatiwa katika ESMP ambayo ni sehemu ya ESIA ya mradi huu.
HOJA YA WWF: Kupunguza mvuto kwa watalii. Watalii wa uwindaji na wa picha ndio vyanzo vikuu vya mapato kwa usimamizi wa Selous na jambo muhimu kwa Tanzania na wanaweza kuzuiwa kutembelea eneo hilo ambalo litapoteza tabia yake asilia na kuonekana kama jangwa.
Eneo la Kaskazini, ambapo mradi wa Stiegler’s uko na ambayo ni rahisi kufikika imetengwa kwa kiasi kikubwa kwa utalii wa picha. Utalii wa picha ni tasnia ndogo ikiwa inahudumiwa na vitanda 248 tu katika kambi za kaskazini, lakini ina uwezo wa kukua.
Utalii karibu na eneo la bwawa unaweza kupata nafuu mara tu ujenzi utakapomalizika lakini utalii kando ya maziwa ya chini ya Rufiji na katika maeneo ya Pwani unaweza kupata uharibifu mkubwa kwa muda. Jambo hili ni muhimu kiuchumi.
![]() |
Idadi ya Tembo inazidi kuongezeka kutokana na usalama uliopo baada ya kuanza kwa ujenzi wa Bwana la Julius Nyerere |
MAJIBU YETU: Suala la kupungua kwa vivutio kwa watalii sio kweli. Wanyama wa porini wataongezeka kwa idadi kutokana na usalama kuongezeka na bwawa lenyewe litakuwa kivutio kikubwa kwa watalii. Utalii wa picha itakuwa faida ya ziada kwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Uendeshaji wa bwawa utazingatia uwepo wa maziwa na mifumo thabiti wa Ikolojia katika sehemu ya chini ya mto.
HOJA YA WWF: Kushuka na kupanda kwa kiwango cha ujazo wa maji yanayopita kwenye bwawa. Kwa sababu ya jukumu lake la kipekee katika mfumo wa umeme, mradi wa Stiegler’s utalazimika kuzalisha nishati yote ya umeme wakati wa mahitaji ya kiwango cha chini na wakati wa mahitaji ya kiwango cha juu.
Kwa hiyo, kiwango cha ujazo wa maji yanayopita kwenye bwawa kitabadilika badilika kulingana na mahitaji ya nishati katika wakati husika. Jambo hili linaweza kusababisha kuongezeka na kushuka kwa ghafla kwa maji katika eneo lililoko sehemu ya chini ya bwawa.
MAJIBU YETU: Uendeshaji wa bwawa utazingatia matakwa ya historia kuhusu viwango vya ujazo wa maji yanayopita kwenye sehemu mbalimbali za mto Rufiji kwa mwaka.
HOJA YA WWF: Kubadilisha historia ya viwango vya ujazo wa maji yanayopita kwenye sehemu mbalimbali za Mto Rufiji kwa mwaka. Bwawa litaondoa mafuriko madogo na kupunguza mafuriko makubwa.
Jambo hili litapunguza uwezo wa sehemu ya chini ya mto kusafirisha mashapo, kuchonga mkondo wa mto, kuungana na maziwa yaliyo ndani ya Selous na kwenye eneo la mafuriko ya mto na kudumisha mienendo ya asili ya Delta.
Vipindi vya mtiririko wa kiwango cha chini ambayo inaweza kuwa muhimu kwa mfano, kufukua mchanga kwa ajili matumizi ya wanyama kama vile mamba, pia vitaondolewa.
MAJIBU YETU: Ni ukweli kwamba makazi ya viumbehai yaliyoko Pwani huathiriwa na mabadiliko katika viwango vya maji yanayotiririka kuingia baharini ambapo mabadiliko haya hutokea katika kipindi kilichopo kati ya kujaa kwa bahari na kupwa kwa bahari.
Kwa sababu hizi, wakati wa kiangazi maji safi hupungua na wakati wa mvua maji safi huenda karibu na bahari. Tunaona mabadiliko haya kama mabadiliko ya kawaida ndani ya mifumo, inajidhibiti. Uendeshaji wa bwawa utazingatia matakwa ya historia kuhusu viwango vya ujazo wa maji yanayopita kwenye sehemu mbalimbali za Mto Rufiji kwa mwaka. Kwa hivyo mtiririko wa maji utaendelea kama kawaida.
HOJA YA WWF: Kupunguza mzigo wa mashapo na mabadiliko katika Jiomofolojia isipokuwa kwa mchanga mwembamba ambao unabaki umesimama, mwanzoni hakuna mashapo yatakayopita kwenye bwawa na kujaza maeneo ya chini.
Sehemu ya mto iliyo chini ya korongo la Stiegler’s itashuhudia mmomonyoko katika kingo na kitako chake na baada ya muda, utabadilisha mkondo wake na kuathiri matumizi ya watu na miundombinu pamoja na makazi ya viumbe katika eneo la mafuriko na Delta.
Pwani inaweza kurudi nyuma kuelekea baharini. Baada ya muda ufanisi wa kunasa na kuhifadhi mashapo utapungua na mashapo zaidi yatapita.
MAJIBU YETU: Mabadiliko ya Ukanda wa Pwani ni ya muda mfupi. Kulingana na historia ya mabwawa yaliyopo kwenye nusu ya juu ya mto ambayo yalijengwa katika miaka ya 1970 na 1980 matukio kama haya hayajawahi kushuhudiwa.
Ikitokea, usanifu wa bwawa umetengenezwa kiasi kwamba kuna vichochoro katika sehemu ya kitako na katikati ya kitako na uso wa juu wa bwawa kwa ajili ya kutoa mashapo yanayohitajika ili kujaza maeneo yaliyo katika sehemu ya chini ya mapromoko ya Stiegler’s. ESMP ilipendekeza kwamba miongozo ya kudhibiti tatizo la mashapo kurundikana katika bwawa ifuatwe.
HOJA YA WWF: Kupungua kwa viumbehai vya majini katika bwawa. Mabadiliko katika ukubwa wa mashapo na ujazo wa maji yanayotiririka; ubora wa maji kwa kuzingatia kiwango cha matope, chumvi na joto; kufikika kwa nusu ya juu ya mto kwa sehemu ya mizunguko ya maisha ya viumbehai na Jiomofolojia ya mto vitabadilisha hali ya makazi ya viumbe vyote vya majini pamoja na spishi zilizo hatarini.
Kwa mfano, Dugong na Kasa wa baharini, spishi za uvuvi wa kujikimu na spishi zinazofaa kibiashara; kwa mfano Kamba na Kambale. Athari za mabadiliko ya kiwango cha matope na upelekaji wa viinilishe kwenye miamba ya matumbawe kwenye eneo la Mafia haijulikani.
![]() |
Bonde la Mto Rufijji, Ikwiriri |
MAJIBU YETU: Maisha ya majini katika sehemu iliyo chini ya bwawa yanaweza kuathiriwa na upungufu wa viumbehai. Mto Rufiji ulikuwa umesababisha upoteaji mkubwa wa maisha ya binadamu hapo zamani, kwa hivyo usimamizi thabiti wa mto utapunguza hatari ya maisha ya mwanadamu katika sehemu ya chini ya mto.
HOJA YA WWF: Kupungua kwa huduma za Kiikolojia kwa watu ambao ni wakazi wa sehemu ya chini ya mto.
Zaidi ya watu 150,000 hukaa katika Delta ya Rufiji na eneo la mafuriko na wengine 50,000 wanakaa visiwa vya Pwani inayotazamana na Delta hii.
Maisha ya wengi wa watu hawa hutegemea uvunaji wa maliasili au shughuli zingine zinazotegemea huduma za Kiikolojia kama vile uvuvi, kilimo katika ukingo wa mto kinachotegemea mafuriko ya msimu na uvunaji wa miti ya mikoko kwa ajili ya mkaa. Shuguhuli za kujikimu biashara ya uvuvi mdogo ni muhimu kwa ajili ya upatikanaji wa Protini. Pia, viwango vya umaskini katika eneo hili ni kubwa kuliko wastani wa kitaifa.
MAJIBU YETU: Sasa inawezekana kudhibiti mafuriko kupitia uundaji wa mifereji ya umwagiliaji, mifumo ya tahadhari ya mapema na kujenga uwezo wa jamii kuhusu njia za kupunguza au kuepuka hatari.
Delta ya Rufiji inatoa eneo kubwa la ardhi inayofaa kwa umwagiliaji na uwezo uliotajwa wa umwagiliaji unawezekana sana. Upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei rahisi utasaidia njia za ziada za maisha kama vile viwanda vya usindikaji kilimo na hivyo kupunguza utegemezi wa maliasili.
USIKOSE KUSOMA SEHEMU YA SABA YA RIPOTI HII.