Tuesday, June 24, 2025
spot_img

RIPOTI: MWANAFUNZI ST. MARY’S ALIVUTISHWA BANGI

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Daniel Chongolo

RIPOTI YA KUPOTEA KWA MWANAFUNZI WA ST MARY’S ILIYOFICHWA KABATINI HII HAPA (2)

MWANDISHI WA PANORAMA

Novemba 6, 2020, mwanafunzi Labna Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Marys iliyopo eneo la Mbezi, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam aliripotiwa na wazazi wake kutoweka shuleni katika mazingira ya kutatanisha huku uongozi wa shule hiyo ukiwa umeficha siri ya tukio hilo.

Wazazi wa Labna waliripoti tukio hilo Kituo cha Polisi Stakishari na Novemba 18, 2020 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Daniel Chongolo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni aliunda Kamati Maalumu ya kuchunguza tukio hilo lililoghubikwa na usiri mkubwa na kunyamaziwa na vyombo vya habari na katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog, DC Chongolo alisema Serikali haitalala mpaka mwanafunzi huyo atakapopatikana na itatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu sakata hilo.

Tanzania PANORAMA Blog ambayo ndiyo pekee iliripoti tukio hilo na kuendelea kulifuatilia kwa karibu ilielezwa na wajumbe wa kamati ya DC Chongolo kuwa wakati wa uchunguzi wao walibaini mambo mazito ikiwemo nyumba wa Kamanda wa juu wa Jeshi la Magereza iliyozungushiwa ua, ndani ya ua huo kulikuwa kukifanyika kilimo cha bangi na vijana waliokuwa wakiishi humo walikuwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Aidha, Tanzania PANORAMA Blog lilielezwa kuwa mwanafunzi Labna alitoroshwa shuleni na mtoto wa kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Magereaza na kupelekwa katika nyumba hiyo ambako alivutishwa bangi, kufanyishwa kazi za ndani na kuingiliwa kimwili.

Ikiwa ni takribani miezi sita sasa tangu tukio hilo lilipotokea na DC Chongolo kuunda kamati maalumu ya kulichunguza, haijapata kutolewa taarifa yoyote ya uchunguzi huo wala ripoti hiyo kuwasilishwa kwake licha ya kamati kukamilisha uchunguzi wake Disemba 15, 2020 ambao ulifungiwa kabatini.

Tanzania PANORAMA Blog limefanikiwa kuiona ripoti hiyo ya uchunguzi na hapa linaichapisha neno kwa neno. Hii sehemu ya pili.

Mwanafunzi Labna Said


SEHEMU YA PILI: MAUDHUI

2.    LENGO LA UCHUNGUZI

Kamati ya wilaya iliamua kufanya uchunguzi wa mazingira ili kubaini chanzo cha tukio la kupotea mwanafunzi Lubna Said   Salim katika Shule ya Sekondari St. Mary’s iliyopo Mbezi Juu Manispaa ya Kinondoni.

 2.1.            HISTORIA FUPI NA USAJILI WA SHULE

Shule ya Sekondari St. Mary’s High School imesajliwa tarehe

30/03/2000 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa namba ya usajili S.1060 kama shule ya bweni na kutwa. Shule hii inamilikiwa na mtu binafsi.

Aidha shule hii ina kidato cha kwanza (1) hadi cha sita (6) na ina jumla ya wanafunzi 305 kati yao 151 ni wavulana na 154 ni wasichana.

2.2 HADIDU ZA REJEA ZILIZOONGOZA KAMATI NA NAMNA ILIVYOZIFANYIA KAZI NA YALIYOJITOKEZA

1)Kuchunguza mazingira na chanzo cha kupotea kwa mwanafunzi.

Kamati ya uchunguzi ilifanya ukaguzi katika eneo la tukio na kuthibitisha kutokuwepo kwa mwanafunzi Lubna Salim Said. Katika uchunguzi huo yafuatayo yalibainika:

1 Mwanafunzi Lubna Salim Said alitoroka/alitoroshwa usiku kwa kusaidiwa na vijana wanafunzi ambao wanasoma katika shule hiyo ya St Marys High School.

Vijana hao ni Mohamed Mablock, Dylan Mbagaro na Daniel Raphael.Wanafunzi hawa walihojiwa na kamati na kukiri kuhusika katika kumsaidia Lubna kuruka ukuta na kutoroka au kutoroshwa.


2.                Mahojiano kati ya kamati na jamii inayoizunguka eneo la shule.

Kamati ilifanya mahojiano na watu kadhaa, ambapo waliohojiwa walizungumza yafuatayo:

i.Ntipoo Yissambi (Mkuu wa Shule) alipoulizwa na kamati uligundua lini kuwa Lubna ametoka na haonekani shuleni, mkuu wa shule  alijibu kuwa “niligundua tarehe 4/10/2020 saa kumi usiku kupitia kwa matron kuwa mtoto mmoja baada ya ‘preparation’ ya usiku hakuonekena.”

Pia mkuu wa shule ilimwagiza Matron aangalie vyumba vyote vya wanafunzi kutokana na namna mazingira ya shule yalivyo. Matron alijitahidi kufanya hivyo lakini hakufanikiwa kwa usiku wa tarehe 4/10/2020.

Kesho yake mkuu wa shule alimpigia simu mama yake Lubna ili kujua kama atakuwa alikwenda kwake, mama yake na Lubna alimjibu kuwa yeye yupo Shinyanga na akaahidi kuuliza kama Lubna engekuwa kwa kaka yake.

Siku inayofuata mama yake Lubna alimweleza mkuu wa shule kuwa huyo mwanafunzi hayupo kwa kaka yake. Mkuu pia alisema “wanafunzi wenzake wanasema Lubna Salim Said hataki kusoma.

Bodi ya shule iliendelea kumhoji: je ulitoa taarifa kwa mamlaka kuhusu kutoonekana kwa mwanafunzi? Mkuu alisema “hakutoa taarifa kwa mamlaka husika  kwa wakati hadi tarehe ya uchunguzi wazazi ndio walioripoti. Mahojiano na Polisi yalifanyika tarehe 6/11/2020.

ii Maelezo ya wanafunzi wenzake:

Samwel Wasele, kidato cha nne alidai ameongea na Lubna Salim Said kupitia kwa Rahim Nyamka kuwa Lubna Salim Said alikuwa kwake, wajumbe waliomba wapelekwe hapo, juhudi zilifanyika lakini hazikuzaa matunda kwani hawakumuona.

Wajumbe waliomba Samwel awapeleke kwa kina Rahim na walipofika waliishia kuongea na Rahim getini bila kuingia ndani hivyo kushindwa kujua kama Lubna Salim Said yupo au hayupo.

Rahim ni kijana aliyehitimu kidato cha nne hapo hapo  St. Mary’s High School mwaka 2019 na alishawahi kushirirki kuwatorosha wanafunzi 9 kwenda disco kwa maelezo ya mkuu wa shule Bwana Ntipoo.

Wanafunzi wawili Jackosn na Samwel walienda nyumbani kwa Rahim wakiwa nje walisikia “mtoto katudekia amepewa  bangi amelala.”

iii Wanafunzi wengine waliomsaidia Lubna Salim Said kutoroka ni hawa wafuatao: Mohamed Moblok, Dylan Mbagoro na Daniel Raphael.

iv Mahojiano na vijana waliokutwa kwa akina Rahim walieleza yafuatayo:

 a Lubna Salim Saidi alikua na Rahim kwa takribani siku tatu.

 b Lubna Salim Said alikua akifanya kazi za usafi nyumbani kwa Rahim.

c Lubna Salim Said alivutishwa bangi.

V Vijana wengine waliohojiwa kwa nyakati tofauti ni pamoja na hawa wafuatao. Rifati Nyamka, David Mtembez, Wilson Godfrey, Mgeni Hassan, Sunday Omary na Igibri Ngwelio.

Hawa vijana wanakaa ‘servant quarter’ yenye vyumba viwili kwa mzee Nyamka na wanajishughulisha na kazi ya kurekodi muziki.

‘Servant Quarter’ ina vyumba viwili, sebule na choo au jiko. Na chumba kimoja kinachotumika na Rahimu kilivunjwa baada ya ridhaa ya mwenyekiti wa mtaa na mjumbe wake mmoja.

Hicho chumba (Gheto) kilikuwa na harufu mbaya na kilitawaliwa na harufu ya bangi. Vijana wanne kati yao walikuwa wamesuka rasta.

Vijana hao walikiri kumuona Lubna Salim Said na kuwa alikuwa akivutishwa bangi na alikuwa akifanya kazi mbalimbali kama za usafi (kupiga deki).

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC) Daniel Chongolo ambaye kamati aliyoiunda kuchunguza sakata la Shule yta Sekondari ya St. Mary’s, haijampatia ripoti 


3.                Kiwango cha usalama katika shule.

i.                        Kamati ilibaini kuwepo kwa kiwango kisichoridhisha cha usalama katika shule hiyo kutokana na kutodhibiti muingiliano na mawasiliano baina ya wanafunzi na wasio wanafunzi katika shule hiyo.

3.2.5 Uzingativu wa taratibu za uendeshaji na usimamizi wa shule

Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2002 sura ya 353 inampa Kamishna wa Elimu mamlaka ya kusajli taasisi za elimu ikiwemo shule za sekondari.

Shule ya Sekondari St. Mary’s High School ni miongoni mwa shule iliyosajiliwa kama shule ya  bweni na kutwa.

 i.                        Kamati imebaini kuwepo kwa vyumba vinavyotumika kama mabweni visivyokidhi vigezo vya bweni ya kulaza wanafunzi jambo ambalo ni kinyume na taratibu za ujenzi.

Itaendelea 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya