![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo |
MWANDISHI WA PANORAMA
Novemba 6, 2020, mwanafunzi Labna Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St Marys iliyopo eneo la Mbezi, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam aliripotiwa na wazazi wake kutoweka shuleni katika mazingira ya kutatanisha huku uongozi wa shule hiyo ukiwa umeficha siri ya tukio hilo.
Wazazi wa Labna waliripoti tukio hilo Kituo cha Polisi Stakishari na Novemba 18, 2020 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Daniel Chongolo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Kinondoni aliunda Kamati Maalumu ya kuchunguza tukio hilo lililoghubikwa na usiri mkubwa na kunyamaziwa na vyombo vya habari na katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog, DC Chongolo alisema Serikali haitalala mpaka mwanafunzi huyo atakapopatikana na itatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu sakata hilo.
Tanzania PANORAMA Blog ambayo ndiyo pekee iliripoti tukio hilo na kuendelea kulifuatilia kwa karibu ilielezwa na wajumbe wa kamati ya DC Chongolo kuwa wakati wa uchunguzi wao walibaini mambo mazito ikiwemo nyumba wa Kamanda wa juu wa Jeshi la Magereza iliyozungushiwa ua, ndani ya ua huo kulikuwa kukifanyika kilimo cha bangi na vijana waliokuwa wakiishi humo walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya.
Aidha, Tanzania PANORAMA Blog lilielezwa kuwa mwanafunzi Labna alitoroshwa shuleni na mtoto wa kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Magereaza na kupelekwa katika nyumba hiyo ambako alivutishwa bangi, kufanyishwa kazi za ndani na kuingiliwa kimwili.
Ikiwa ni takribani miezi sita sasa tangu tukio hilo lilipotokea na DC Chongolo kuunda kamati maalumu ya kulichunguza, haijapata kutolewa taarifa yoyote ya uchunguzi huo licha ya kamati kukamilisha uchunguzi wake Disemba 15, 2020 ambao ulifungiwa kabatini.
Tanzania PANORAMA Blog limefanikiwa kuiona ripoti hiyo ya uchunguzi na hapa linaichapisha neno kwa neno.
TAARIFA YA KAMATI MAALUM YA MKUU WA WILAYA YA KINONDONI KUCHUNGUZA TUKIO LA KUPOTEA KWA MWANAFUNZI LUBNA SALIM SAID WA SHULE YA SEKONDARI ST. MARY’S HIGH SCHOOL, MANISPAA YA KINONDONI – DAR ES SALAAM, NOVEMBA, 2020
SEHEMU YA KWANZA
![]() |
Labna Salim Said |
1. UTANGULIZI
1. Tukio la kupotea Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Mary’s
Mnamo tarehe 06/11/2020 majira ya saa saba (13:00hrs) huko Goba Kituo cha Polisi iliripotiwa taarifa ya kupotea mwanafunzi wa bweni katika Shule ya Sekondari St. Mary’s High School, aitwaye LUBNA SALIM SAID wa kidato cha tatu, (III).
Kuwa mwanafunzi huyo alitoroka shuleni hapo tangu tarehe 04/10/2020na mpaka tarehe hiyo akawa hajaonekana, hivyo mara baada ya taarifa hiyo, uchunguzi ulianza mara moja ikiwa ni pamoja na kufika shule ili kufanya mahojiano na baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo, hata hivyo ushirikiano ulikua hafifu kutokana na jukumu la mitihani ya taifa inayo endelea katika shule hiyo.
1:2 Kuundwa tume ya kamati ya uchunguzi wa tukio
Tarehe 18/11/2020 iliundwa tume ya watu wanne ambao ndio walioendelea na uchunguzi ambao waliweza kufika hadi nyumbani kwa Afande SACP-RAMADHANI NYAMKA, Kamishna wa Magereza mwenye mtoto wake aitwaye RAHIM NYAMKAambaye ndiye anaye tuhumiwa kuwa na mahusiano na mwanafunzi huyo, lakini katika mahojiano na baadhi ya ndugu wa RAHIM akiwemo kaka yake aitwaye RIFAT NYAMKAajulikanaye kama ‘Bobu’ alikiri kumfahamu binti huyo kama mpenzi wa mdogo wake lakini akadai kwa sasa hajui alipo.
Tarehe 12/12/2020 majira ya 02:00hrs A/INSP.GWAKE I/C CID GOBAambaye pia ni miongoni mwa watu wa tume alipata taarifa toka kwa wazazi wa mwanafunzi kuwa kuna taarifa mtoto wao ameonekana maeneo ya STAKISHARI BANANA, baada ya taarifa hizo mkaguzi huyo akawasiliana na Mkuu wa Upelelezi STAKISHARI ambaye alimuunganisha na mkaguzi wa zamu aitwaye INSP. SYLVESTERambapo walifanikiwa kumkamata binti huyo na kumfikisha katika kituo cha STAKISHARI.
Baada ya kuhojiwa, binti huyo alikiri kutoroshwa na RAHIM NYAMKA usiku huo na kulala nyumbani kwa kijana huyo ambapo asubuhi alimuamuru aondoke kurudi shule au kwenda nyumbani kwao.
Lakini kutokana na uoga wa binti huyo aliamua kwenda kwa mpenzi wa dada yake ambako alikaa huko hadi jioni ya tarehe 05/10/2020 na kupewa pesa kiasi cha sh: 30,000/ na shemeji yake aitwaye JACKSON S/O ambaye alimpa hela hiyo na kumshauri aende nyumbani, lakini kutokana na uoga wake alikutana na kijana aitwaye RAMADHAN S/O ambaye hakujua kama ni mwanafunzi na kuamua kwenda kukaa naye huko STAKISHARI CHA MOTO.
Katika mahojiano na binti huyo alizidi kueleza kuwa kuna siku alirudi tena kwa RAHIM NYAMKA na kukaa huko siku takribani tano (5) huku RAMADHAN ambaye anaishi naye akimuaga kama kaenda nyumbani kwao, baadaye akarudi tena mpaka alipokamatwa huku mwanaume wake akiwa bado hajarudi.
1:3 Kuundwa kwa Kamati ya Uchunguzi ya Wilaya
Kamati ya Usalama ya Wilaya, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh. Daniel Chongolo aliiagiza kamati aliyoiteua tarehe 18/11/2020 baada ya tukio la kupotea mwanafunzi huyo, kuendelea na uchunguzi na kubaini chanzo chake. Tukio hilo lilisababisha taharuki kwa wazazi na wanafunzi na jamii nzima kwa ujumla.
![]() |
DC Chongolo |
Mkuu huyo wa wilaya aliielekeza kamati aliyoiteua kuchunguza chanzo cha tukio la kupotea kwa Mwanafunzi LUBNA SALIM SAID wa kidato cha III wa Shule ya Sekondari St. Mary’s High School iliyopo Mbezi Juu, Wilaya ya Kinondoni. Kamati hiyo iliundwa na wajumbe wanne (4) kutoka taasisi mbalimbali za serikali kama ifuatavyo;
i. Joseph M. Kapere, Afisa Elimu Sekondari – Kinondoni (Mwenyekiti)
ii. Mdhibiti Ubora wa Shule.
iii.Insp Gwaki (Polisi (RPC) Kanda ya Kinondoni).
iv. Ngusa Mabula (DSO Manispaa ya Kinondoni).
1:4 Chimbuko la Kamati ya Uchunguzi
Chimbuko la kamati ya uchunguzi wa tukio la kupotea kwa mwanafunzi katika Shule ya Sekondari St. Mary’s High School, lilitokana na maamuzi ya Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ya Kinondoni baada ya kupata taarifa juu ya kutoweka mwanafunzi huyo tangu tarehe 04 Octoba 2020.
1:5 Hadidu rejea zitakazoiongoza kamati ya uchunguzi
Hadidu za rejea zifuatazo ziliiongoza kamati kufanya uchunguzi wa tukio la kupotea kwa mwanafunzi LUBNA SALIM SAID:
i. Sababu zilizopelekea mwanafunzi kutoroka.
ii.Kubaini iwapo taratibu za wanafunzi wa bweni zinazingatiwa.
iii.Kubaini taratibu zinazofuatwa kwa mwanafunzi wa bweni asipoonekana kwa sababu yoyote ile.
iv. Watu/wanafunzi waliosaidia na kushuhudia mwanafunzi akitoroka.
v. Kubaini iwapo mazingira ya shule yanashawishi wanafunzi kutoroka au kuacha shule.
vi.Kubaini mahali alipo mwanafunzi kwa kipindi ambacho hakuwepo shule wala nyumbani kwao.
vii.Kubaini jitihada za wazazi katika kumtafuta mwanafunzi.
1:6 Utaratibu wa kazi ya kamati ya uchunguzi
Kamati hii katika kutekeleza majukumu yake ilikagua mazingira ya eneo la tukio na kupata maelezo kutoka vyanzo mbalimbali, kutafsiri maelezo toka kwa watu mbalimbali na kuandaa taarifa ya uchunguzi wa tukio hilo la kupotea kwa mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekondari St. Mary’s High School.
1)Muda wa kazi
Kamati hii ilifanya kazi yake kuanzia tarehe 19/11/2020 siku ya Jumanne hadi siku ya Jumanne tarehe 15/12/2020.
2) Njia zilizotumika kukamilisha kazi
Kamati ilitumia njia mbalimbali ili kufikia lengo la uchunguzi wa tukio la kupotea mwanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Mary’s High School. Njia hizo ni kama zilizooneshwa hapo chini.
3)Kukagua eneo la tukio.
Kamati ya wilaya ilifika kukagua eneo la tukio katika Shule ya Sekondari St. Mary’s High School ili kujiridhisha kama mwanafunzi anaweza kutoroshwa, au kutoroka mwenyewe.
4)Kufanya mahojiano na makundi mbalimbali, ikiwemo walimu, wanafunzi na watumishi wasio walimu, wazazi pamoja na jamii inayoizunguka shule.
Usikose kusoma sehemu ya pili ya ripoti ya kamati hii kesho