![]() |
Chanjo ya virusi vya Corona inayofahamika kwa jina la AstraZeneca |
NA ABBAS MWALIMU
0719258484
KUNA na mjadala mpana na hali ya sintofahamu tangu kuanza kutumika kwa chanjo ya kuzuia virusi vya ugonjwa wa Corona au UVIKO-19 (COVID-19) mwezi Februari, 2021.
Hali inayozidisha mashaka zaidi inatokana na baadhi ya nchi duniani kuanza kusitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca Oxford baada ya chanjo hiyo ya kuzuia virusi vya Corona kuleta madhara ya kusababisha damu kuganda kwa waliotumia.
Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limeripoti watu saba kufariki nchini humo baada ya kupatiwa chanjo ya Oxford-AstraZeneca.
Kwa mujibu wa BBC, zaidi ya watu 30 kati ya milioni 18 waliopatiwa chanjo mpaka tarehe 24 mwezi Machi walipata tatizo la kuganda damu na kwamba bado haijawa wazi kama vifo hivyo vinatokana na athari ya kuganda kwa damu inayosababishwa na chanjo hiyo au lah.
Huku hayo yakijiri, Mganga Mkuu na Mshauri Mkuu wa Afya nchini Uingereza, Chris Whitty ameshauri Waingereza wajifunze kuishi na Covid 19 kama walivyojifunza kuishi na ugonjwa wa mafua (Flu). Kauli kama hii pia iliwahi kutolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson.
![]() |
Mganga Mkuu na Mshauri Mkuu wa Afya wa Uingereza, Chris Whitty |
Kwa upande mwingine Ujerumani, Ufaransa na Italia zimesitisha kutumia chanjo ya AstraZeneca ikiwa ni baada ya nchi kadhaa kuelezea madhara yaliyojitokeza kwa waliopewa chanjo hiyo.
Nchi hizo za Ufaransa, Ujerumani sambamba na Uholanzi na Canada zimeagiza chanjo hiyo itumike kwa wazee tu.
Nchi za Denmark na Norway zimeacha kugawa chanjo hiyo mwezi Machi baada ya baadhi ya waliopewa kuripotiwa kuganda au kuvuja damu pamoja na dalili nyingine.
Iceland, Bulgaria, Ireland na Netherland pia zimetangaza kusitisha ugawaji wa chanjo hiyo tangu mwezi Machi huku Hispania pia ikisema itasitisha kwa siku 15 kuangalia hali halisi.
Barani Afrika, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeamua kuahirisha utoaji wa chanjo hiyo ambapo Wizara ya Afya nchini humo imesema ugawaji utafanyika baada ya kukamilika kwa uchunguzi kuhusu athari hizo.
Hali hii inazua maswali kadhaa juu ya uwezo wa chanjo hizo kuzuia virusi vya Corona, athari zinazoweza kusababishwa kwa binadamu, ukomo wa nguvu ya chanjo zenyewe na namna zilivyotengenezwa katika maabara.
Jambo lingine linalozua sintofahamu na ukakasi juu ya chanjo hizi za COVID-19 ni kwamba makampuni yote yanayozalisha chanjo hizi zilizopo sokoni kwa sasa yanatoka katika nchi ambazo ni Wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani UNSC P5.
Kuthibitisha hili ni kwamba, chanjo ya Sinopharm inatengenezwa nchini China, chanjo ya AstraZeneca Oxford inazalishwa nchini Uingereza, chanjo ya Sputnik inazalishwa nchini Urusi na chanjo ya Pfizer inazalishwa nchini Marekani.
Nchi hizi zote nne zinaunda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa sambamba na nchi ya Ufaransa ambayo bado haijaingiza/haijazalisha chanjo yake na kuingiza sokoni.
Nchi hizi zenye kura ya veto (kura yenye kuamua kila kitu) katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (Rejea ibara ya 39 ya UN Charter) zimekuwa zikilalamikiwa kwa kutazama maslahi yao kwanza dhidi ya maslahi ya ulimwengu kama walivyoeleza Brock na Simon (2021:436) katika kitabu chao ‘The Justification of War and International Order’ waliposema:
‘The veto power of the five permanent members of the Council (the P5); intended to protect their core interests,* has been used much more widely to prevent the Council from acting in respect of issues where the P5 believe that they or their clients and allies have any skin in the game, which,of course, is most issues.’
Tabia hii ya mataifa haya yenye kura ya turufu (veto) kuangalia maslahi yao kwanza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inatia shaka hata kwenye masuala kama haya ya afya za binadamu ambapo mataifa yote haya yanaangalia namna ya kunufaika.
Al-Rodham (2007) yeye aliongezea kwa kusema, ‘mataifa haya hutekeleza maslahi yao kwa kujifanya yanasimamia maslahi ya Umoja wa Mataifa wakati yanasimamia maslahi yao binafsi.’
Kuwepo kwa makampuni haya yanayozalisha chanjo kutoka nchi zenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunazidisha maswali kwamba je, hizi ni chanjo tu ama ni biashara?
Kwamba labda nchi zinazoonekana kuwa zinazuia mpango huu wa kibiashara wa mataifa yenye kura ya turufu zipigwe vita ya kimkakati mpaka zikubaliane na biashara ya wakubwa?
KWA NINI HOFU NA MASWALI HAYO YANAKUJA?
Kwa maoni yangu nadhani maswali na mtazamo na kitendo cha kukataa chanjo kwa baadhi ya nchi vinakuja kutokana na sababu zifuatazo:
Mosi; Kutokuwepo kwa uwazi kutoka kwa makampuni yanayotengeneza chanjo juu ya madhara ya chanjo hizo kwa mfano, kwa nini hawakuwahi kuonya labda chanjo hizo zinaweza kusababisha madhara ya kuganda kwa damu kama walipitia hatua zote za kitaalamu za kutengeneza chanjo?
Pili; kutokuwepo kwa uwazi juu ya ukomo wa nguvu ya chanjo kwa mfano je ni baada ya muda gani chanjo hizo zinaisha nguvu ndipo watu wachomwe tena? Je ni wiki, mwezi, mwaka au miaka au zinadumu milele?
Tatu; kutokuwepo kwa uwazi juu ya kundi gani la watu watumie na kundi gani wasitumie au watumie kwa kiasi gani? Wazee? Vijana au watoto?
Kwa ufupi maswali haya na mengine mengi sambamba na mitazamo hiyo kutopatiwa majibu ya kitaalamu kunaonesha wazi kuwa kuna matatizo katika uzalishaji wa chanjo hizi.
Huenda labda namna chanjo hizo zilivyoandaliwa hazikuzingatia baadhi ya masuala ama kuna hatua za kitaalamu hazikufuatwa kikamilifu n.k, ambazo kimsingi zingeweza kujibu maswali mbalimbali na hoja wakati ule wa utafiti kuliko ambavyo zinatolewa na wale wanaozikataa hivi sasa.
Binafsi ninaamini kwamba chanjo ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu lakini naamini zaidi kuwa maswali ya wale wanaotilia shaka taratibu zilizotumika katika kupata chanjo hizi yakijibiwa kwa ufasaha na kitaalamu itasaidia kuondoa dhana kwamba chanjo hizi si kinga dhidi ya COVID-19 bali ni biashara ya mataifa yenye kura ya turufu na kwamba yule anaepingana nao apigwe vita.
Yasipojibiwa maswali hayo kwa hoja zilizoshiba ni wazi dhana ya kwamba ni mpango wa biashara ya mataifa yenye uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa (UN) itaendelea kushika kwa sababu zipo rejea mbalimbali zinazoelezea namna makampuni makubwa ya dawa yanavyojiingizia faida kupitia magonjwa bila ya kujali afya za watu.
Brezis, Mayer katika andiko lake la Big Pharma and Health Care: Unsolvable Conflict of Interest between Private Companies and Public Health cha mwaka 2008 alieleza hayo.
Naye Ferner katika andiko lake la The influence of Big Pharma: Wide ranging report identifies many areas of influence and distortion la mwaka 2005 aliainisha uchunguzi uliofanywa na Bunge la Makabwela la Uingereza (House of Commons) lilivyobaini namna makampuni makubwa ya dawa yanavyojitajirisha kwa kuwakandamiza wanyonge.
![]() |
Bendera za nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UNSC P5) |
Ripoti hiyo, The influence of the Pharmaceutical industry’ ya Kamati ya Afya ya House of Commons ilibainisha kwamba makampuni makubwa ya dawa huwashawishi madaktari, ‘charities,’ makundi yanayohusika kutetea haki za wagonjwa, wanahabari na wanasiasa na wale ambao msimamo wao ni dhaifu na haueleweki ili kuweza kufanikisha azma yao ya kunyonya wanyonge kupitia afya.
Ferner (2005) alifafanua ripoti ya Kamati ya Afya ya Bunge la Makabwela kama ifuatavyo:
‘The House of Commons Health Commitee examined the means the Big Pharma use to achieve this noble end (and) they found an industry buys (that) influence over doctors, charities, patient groups, journalists and whose regulation is sometimes weak and ambiguous.’
Makampuni makubwa ya dawa hupata faida kubwa pindi yanapokuja na dawa au chanjo ya kudhibiti ugonjwa fulani ambapo watu hununua wa wingi ili kujilinda. Haya yalibainishwa na Meller na Ahmed (2019) katika andiko lao ‘How Big Pharma Reaps Profir While Hurting Everyday Americans’ walipoeleza yafuatayo:
‘Pharmaceuticals companies profit margins receive significant bumps when they launch new drugs specifically speciality drugs used to treat life-threatening conditions’ (Meller na Ahmed, 2019).
Kama Meller na Ahmed (2019) wanasema makampuni makubwa hupata faida kubwa sana pindi yanapozindua dawa mpya ya kupambana na ugonjwa unaotishia maisha, je suala kama hili litaondoaje dhana kuwa makampuni makubwa yapo kibiashara zaidi katika kupambana na COVID-19?
Meller na Ahmed (2019) wanaendelea kubainisha kuwa Kamati ya Fedha ya Bunge la Seneti ilibaini kuwa mwaka 2013 kampuni ya Gilead Science iliyotengeneza dawa ya Solvadi ilijiongezea faida pasina kujali upatikanaji na uwezo wa watu kumudu dawa hiyo.
Kwa kukazia Muller na Ahmed (2019) waliainisha yaliyoelezwa kwenye Ripoti ya Uwajibikaji ya Serikali ya Marekani yaani Government Accountability Office (GAO) ambayo ilibaini kuwa faida ya makampuni makubwa ya dawa ilikuwa kati ya asilimia 15 mpaka 20 kwa kipindi hicho.
JE CHANJO HIZI NI KINGA AU BIASHARA?
Ripoti ya GAO ilisomeka kama ifuatavyo na hapa ninanukuu; ‘Among the largest 25 companies, annual average profit margin fluctuated between 15 and 20 percent’ (GAO Report page 39).
Muller na Ahmed wanasema; ‘Kwa mwaka 2018 peke, maCEO wa makampuni makubwa ya Allegran, Johnson&Johnson na Pfizer Inc. walivuna jumla ya Dola za Marekani Milioni 90.’
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Kampuni ya AstraZeneca imeingiza kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 1 na inatarajia kuingiza kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 18.4 kwa kuuza dozi milioni 700 mwaka huu 2021.
Jambo la ajabu ni kwamba tumeona baadhi ya nchi na taasisi kama Shirika la Afya Duniani (WHO) zikijaribu kutumia vitisho kulazimisha nchi ambazo hazijanunua dawa hizo kununua kwa lazima.
Kwa maoni yangu, jambo hilo ni kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kama ilivyoainishwa katika ibara ya pili, ibara ndogo ya nne ya UN Charter ambayo inasomeka kama ifuatavyo:
‘All Members shall refrain in their international relations from the threat or use of force against the territorial integrity or political independence of any state, or in any other manner inconsistent with the Purposes of the United Nations.’
Binafsi ninaamini kuwa kukubali ama kukataa chanjo kwa nchi linabaki kuwa ni suala la mamlaka ya dola husika (Sovereignty) kwa kuzingatia mazingira yake na maslahi ya taifa na hivyo basi kulazimisha dola huru kukubali lile ambalo dola hilo linaona si sahihi ni kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kama inavyoeleza ibara hiyo hiyo ya pili ibara ndogo ya saba kwamba:
‘Nothing contained in the Present Charter shall authorize the United Nations to intervene in matters which are essentially within the domestic jurisdiction of any state…’
Mimi nafikiri kabla ya kuzilazimisha nchi kununua chanjo kuna umuhimu wa kuwepo kwa Mkataba wa Kimataifa wa COVID-19 ili kila nchi iridhie kwanza kwa kuzingatia kanuni ya Pacta Sunt Servanda, hapo ndipo ulazima unaweza ukawepo kwa kufuata sheria za kimataifa ila vinginevyo hii itakuwa kama vita dhidi ya wale wanaopinga chanjo hizo huku vita hiyo ikiwa imetangazwa bila kuzingatia sheria za kimataifa za vita za mwaka 1949.