MWANDISHI WA PANORAMA
HALI si shwari katika Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam baada ya mgogoro wa ardhi baina ya mwekezaji Mtanzania, Flora M’mbungu Schelling na uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kigamboni kuanza kuchukua sura ya vitisho na kupoka kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya mwekezaji huyo lililo ufukweni mwa Bahari ya Hindi.
Tanzania PANORAMA Blog imeelezwa kuwa mwekezaji huyo amekimbia nchini baada ya kutishiwa maisha yake kwa sababu ya kukataa kuliachia eneo hilo linalodaiwa kumezewa mate na kunyemelewa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa.
Inadaiwa kuwa, Serikali ya Wilaya ya Kigamboni imeanza mchakato wa kumnyang’anya mwekezaji huyo eneo lake analolimiki kihalali kwa zaidi ya miaka 30 sasa ili kuligawa kwa wananchi bila kumlipa fidia yoyote na kwamba baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kigamboni walishiriki mipango miovu ya kufunga biashara zake ikiwemo ya hoteli ya kitalii ndani ya eneo hilo ili kumpunguzia nguvu za kiuchumi na pia kumtesa kisaikolojia.
Kiongozi anayedaiwa kuhusika moja kwa moja katika mipango miovu dhidi mwekezaji huyo ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni (DC) Sarah Msafiri, kwamba baada ya kuendesha fitna za chini kwa chini za kulipoka eneo hilo kutofanikiwa, alituma greda kwenda kuharibu miti asili aliyooteshwa kwa ajili ya kuvutia watalii kwa madai kuwa anachonga barabara kwa ajili ya wananchi kupita kwenda baharini kufanya shughuli za uvuvi kwa sababu mwekezaji anawazuia kupita kwenda kujitafutia riziki.
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni (DC) Sarah Msafiri |
DC Msafiri alipotafutwa na Tanzania PANORAMA Blog wiki iliyopita na kuulizwa kuhusu kadhia hiyo alisema ametingwa na kazi nyingi na hata alipotumiwa maswali kwa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani, licha ya kuonyesha kuwa ameyapata na kuyasoma, hakujibu.
Aidha, eneo ambalo greda hilo lilifanya uharibifu wa kung’oa miti asilia kwa maelekezo ya DC Msafiri kuwa linachonga barabara kwa ajili ya wananchi kupita kwenda baharini ambalo limeonwa na Tanzania PANORAMA Blog, barabara hiyo haipo na sasa limeota nyasi na miti imeanza kustawi upya.
Msimamizi wa eneo hilo la uwekezaji, Viola Sweya ambaye amefanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya mwekezaji huyo na Serikali ya Wilaya ya Kigamboni, alieleza kuwa hali ni tete kwa sababu watu wasiojulikana wamekuwa wakivamiwa na kujipimia viwanja huku wengine wakileta wateja kwa ajili ya kuwauzia na wanapowauliza wanadai kuwa DC Msafiri amewaruhusu kujitwalia viwanja ndani ya eneo hilo kwa sababu ni mali ya Serikali.
“Hapa hali ni mbaya, vita ya ardhi ni mbaya sana. Tunaishi kwa wasiwasi kwa sababu tunaweza kushambuliwa tukapoteza maisha ukizingatia hata bosi wetu ameishakimbia nchini kutokana na vitisho alivyokuwa akivitapa alipokuwa akikataa kuachia eneo lake.
“Mimi ninavyojua eneo lote hili ni mali ya Schelling kihalali kabisa, hati zote za umiliki wa viwanja hivi anazo na alikuwa akilipa kodi zote za Serikali. Alinunua maeneo haya zamani sana, mwaka 1992 na siyo hivyo tu, mwaka 2010 alijiunga na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kwa hiyo ni mwekezaji anayetambulika mpaka TIC na hapa amewekeza yaani kwa kiwango cha chini kabisa ni zaidi ya shilingi bilioni tatu.
“Mimi nimefanya kazi kwake kwa muda mrefu sana hivyo ninajua ukweli wote na hata ukitaka nikupe hati halali za hapa uzichapishe nakupa. Alipopanunua palikuwa peupe kama jangwa, yeye akaanza kupanda miti na kujenga hizo nyumba zenye mwenekano wa kiasili kwa ajili ya watalii na ile hoteli kule pamoja na kusafisha ufukwe wote huu.
![]() |
Msikiti uliojengwa na wangazija karne ya 14 na kukarabatiwa hivi karibuni na mwekezaji Flora Schelling kwa ajili ya matumizi ya shughuli za utalii. |
“Ule msikiti wanaosema anazuia watu kusali ulikuwa gofu, historia ya eneo hili ukiuliza kwa wenyeji wanasema msikiti huo uliojengwa na waganzija karne ya 14 na pembeni hapo kuna makaburi ya baadhi yao, hilo eneo la makaburi sasa halitumiki, lakini ajabu wanasema eti kazuia watu kuzika, kaangalie au uliza wanakijiji hapa kama kuna mtu anazikwa hapo.
“Palipoanza kupendeza sasa maana hata huo msikiti ulikuwa gofu, aliponunua ulikuwa umebakia ukuta mmoja tu, yeye akaukarabati kwa sababu ya kuwa kivutio cha utalii, hapo akaanza kupata misukosuko, wakubwa huko serikalini wakitaka kumnyang’anya kwa sababu ni mwanamke lakini alikuwa na hati zote halali hivyo akawa anawashinda ila alipokuwa huyu DC wa sasa, Msafiri ndipo ikawa vita.
“Mwanzoni kabisa alikuja kirafiki kama anakuja kutembea, bosi kuona kiongozi kamtembelea akafurahi akamtembeza kote, akawa anamuuliza amewezaje kupatunza na kuotesha hii miti ya asili akamwambia ametumia gharama kubwa sana na bidii pia. Akamuuliza kama anamiliki eneo lote hili kihalali, bosi akamtolea hati zote, basi wakawa wamekaa ufukweni kule wanaongea huku DC naye akisema anatafuta eneo kama hilo.
“Ajabu sasa baada ya siku chache akageuka. Ndipo vita ilipoanza, mara kasema amezuia watu kutumia msikiti, halafu wakadai amezuia wananchi kutumia makaburi, mara amezuia njia ya kwenda ufukweni kwa ajili ya wananchi kufanya shughuli za uvuvi, yaani wamepelekana mpaka wizarani lakini vitisho vilipozidi bosi akaona kuna hatari, akakimbia akatuacha tupalinde wakati yeye akijaribu njia nyingine ya kupata haki yake akiwa mbali, lakini sasa ndiyo hivyo, wanakuja watu hapa kila siku, wengine madalali tunawajua kabisa wanasema wametumwa na DC kupima viwanja. Hawana vitambulisho wala barua yoyote, tukiwauliza wanasema twende kwa DC, basi ni hofu tu,” alisema Viola.
Mbali na maelezo hayo ya Viola, moja ya nyaraka za mgororo huo ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeona inaonyesha kuwa eneo linalogombaniwa linamilikiwa na Kampuni za Oyster Camp Ltd, Ras Bamba Sailing Club Ltd na Ras Bamba Hotel Limited ambazo Mkurugenzi Mtendaji wake ni Schelling.
Nyaraka zinaonyesha kuwa mchakato wa kampuni hizo kumiliki ardhi hiyo ulianza mwaka 1989 na mwaka 1992 Wizara ya Ardhi ililiingiza eneo hilo kwenye ramani ya mipango miji baada ya kuridhia maombi ya umiliki wa ardhi hiyo yaliyotolewa na kampuni hizo.
“Kampuni zote tatu zilifuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria katika kumilikishwa ardhi hizi kuanzia ngazi ya kijiji, wilaya mpaka wizara. Tulijiunga na TIC mwaka 2010 ili tutambulike kama wawezekaji halali.
![]() |
Hifadhi ya uoto wa asili iliyo ndani ya eneo la uwekezaji la Ras Bamba. |
“Katika eneo hilo tumewekeza zaidi ya shilingi bilioni tatu. Katika eneo hilo tumeweza kuweka miundombinu ya umeme kilomita 2.2 na mabomba ya maji katika eneo lote gharama zaidi ya Dola za Marekani 100,000, inasomeka moja ya sehemu ya nyaraka zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog iliyoandikwa Machi 20, 2020 kwenda Serikali ya Wilaya ya Kigamboni.
Alipoulizwa Fundi Mussa, kiongozi wa kikundi cha uvuvi kinachofamika kwa jina la Beach Menejiment Unit (BMU) kinachofanya shughuli za uvuvi ndani ya eneo la ufukwe linalomilikiwa na Schelling, kuhusu madai ya kuwepo kwa katazo la kuingia eneo hilo kutoka kwa mwekezaji alisema taarifa hizo siyo sahihi na kwamba ndiyo anazisikia kwa mara ya kwanza.
![]() |
Mwenyekiti wa BMU, Fundi Mussa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mgogoro wa eneo la uwekezaji la Ras Bamba |
“Mimi ndiye mwenyekiti wa BMU, jina langu naitwa Fundi Mussa, dada Flora Schelling hamzuii mtu yeyote kuingia eneo hili kujitafutia riziki kama amejitambulisha, hizo taarifa siyo za kweli,” alisema Mwenyekiti Mussa.
Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwepo katazo kutoka kwa mmiliki wa eneo hilo la kutumia msikiti na kwamba eneo la makaburi nalo limezuiliwa na mwekezaji, alisema jambo hilo hawezi kuliingilia kwa sababu lipo nje ya utawala wake ingawa anajua madai hayo yote ni ya uongo ila yanatengenezwa kwa sababu maalumu.
“Tatizo la makaburi na msikiti siwezi kuingilia huko kwa sababu liko nje ya utawala wangu. Huo msikiti historia yake ni ndefu. Wazee wa zamani sana waliokuwa wakiishi eneo hili, ndiyo walikuwa wakiutumia. Una karne nyinyi sana na huyo mwekezaji alipopanunua hapa aliukuta ni gofu tu, ulikuwa umebaki ukuta mmoja tu lakini kuta nyingine zote zilikuwa zimeanguka.
“Nakwambia mimi ni mzaliwa wa hapa, nimefanya kazi ya uvuvi kwa miaka 20 sasa, huyo mwekezaji hafukuzi mtu na hajakaza matumizi ya msikiti wala hakuna kaburi inayotumika pale sema hao wakubwa wana mambo yao tu ila sisi wadogo hatuwezi kuingilia ndugu yangu ila kama haki inatendeka, basi waache hiyo dhambi ya kumnyang’anya huyo mama eneo lake.
“Sisi wavuvi hatuna tatizo naye, si umetukuta tupo hapa kwenye eneo lake na kuna walinzi lakini tunavua salama tu, sasa kuna shida gani? Huo msikiti wanaosema umekatazwa, mimi ni muislamu na ninavua humu zaidi ya miaka 20 lakini sijawahi kuutumia kwa sababu ni gofu. Lakini hiyo vita ya wakubwa acha wamenyane wenyewe,” alisema Fundi
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta DC Msafiri leo na kumuuliza kuhusu madai ya kuwa katikati ya mgogoro huo na kukumbushwa kujibu maswali aliyotumiwa wiki iliyopita lakini alisema jambo hilo amekwishalitolea ufafanuzi na kwamba yupo msibani.
“Hili suala nimeishaliongelea sana, kwanza mimi nipo msibani au nisubirini nirudi,” alisema DC Msafiri.
![]() |
Hotel iliyo ndani ya eneo la utalii la Ras Bamba Kigamboni, Dar es Salaam ambayo sasa imefungwa kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya mwekezaji na Serikali ya Wilaya ya Kigamboni |
Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kufuatilia sakata hili ikiwa ni pamoja na madai kuwa kiongozi mmoja mwandamizi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amempoka ardhi mwananchi mwenye uhusiano wa karibu na Schelling sambamba na kigogo mwingine wa Wizara ya Fedha na Mipango aliyejenga nyumba ya kifahari jirani na eneo la mwekezaji huyo kuvuta umeme kwa mabavu kutoka kwenye nguzo zilizogharamiwa na Schelling.