RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia leo wakati wa kuuaga mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
NA MWANDISHI WA PANORAMA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo amewaongoza wananchi wa Zanzibar kuuaga mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena kutokana na maradhi ya moyo.
Katika hotuba yake ya kumuaga Hayati Rais Dk, Magufuli mbele ya wananchi wa Zanzibar, katika Uwanja wa Amani, Rais Dk. Mwinyi amesema taifa bado lina huzuni kubwa kwa kumpoteza Hayati Rais Dk. Magufuli.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Amani, Zanzibar leo.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar zimefanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuonesha upendo kwa kuuaga mwili wa mpendwa kiongozi wao katika ardhi ya Zanzibar ikiwa ni kuonesha na kutambua yale aliyoyatenda.
Rais Dk. Mwinyi amesema Hayati Rais Dk. Magufuli alikuwa mstari wa mbele kuimarisha maisha ya Watanzania kwa misingi ya haki na usawa bila kujali dini, kabila, rangi wala jinsia hivyo kifo chake kimewaachia simanzi kutokana na mapenzi makubwa waliyokuwa nayo wananchi kwake
“Tutaendelea kumkumbuka Rais John Pombe Magufuli kwa jinsi alivyojipambanua kupigania haki za wanyonge na kujidhatiti katika kudumisha Muungano wa Tanzania pamoja na kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Mkurugenzi Mratibu Kanda wa Shirika la Bima la Zanzibar, Imam Ali Makame, akisaini kitabu cha maombelezo leo, cha Hayati Rais Dk, John Pombe Magufuli, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam
“Tutampa ushirikiano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha majukumu yake ya kuwatumikia watanzania.
“Binafsi namtambua fika kwamba ana uwezo mkubwa wa kuyafanikisha majukumu yake mapya kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kisiasa na kiuongozi katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika.” amesema Rais Dk. Mwinyi.
Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amehudhuria kuagwa kwa Hayati Rais Dk. Magufuli katika Uwanja wa Aman Zanzabar, amesema zaidi ya watu bilioni 3.9 duniani wamefuatilia tukio la mazishi ya kitaifa ya Hayati Rais Dk. Magufuli jana mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana jioni, karibu watu bilioni nne duniani walikuwa wanafuatilia tukio hilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia leo wakati wa kuuaga mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli, katika Uwanja wa Amani, Zanzibar.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ilani ya uchaguzi ya CCM itaendelea kutekelezwa kwa kukamilisha yale aliyoyaanzisha Hayati Rais Dk. Magufuli.
“Kwa niaba ya kamati ya mazishi kitaifa, bado tuko kwenye siku za huzuni tangu siku tumetangaziwa kifo cha Rais wetu mpendwa, ni tukio lisilo la kawaida sana kuondokewa na Rais akiwa madarakani, ila ni mipango ya Mungu na sisi viongozi tunaahidi kuendeleza Ilani na kutekeleza na kukamilisha yale aliyoyaanzisha,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema kwa kutambua upendo wa Watanzania, ratiba ya kuaga imehusisha sehemu mbalimbali hapa nchini na kwamba kesho mwili utatoka Zanzibar asubuhi kwa ndege maalum kuelekea mkoani Mwanza na baada ya kuagwa mkoani hapo utasafirishwa kwa gari hadi nyumbani kwake Chato.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akiongoza mapokezi ya mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume leo.
Msafara wa Magari wenye mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli ukielekea Uwanja wa Amani kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar kutoa heshima za mwisho.