![]() |
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe |
NA CHARLES MULLINDA
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema amepokea kwa masikitiko na huzuni habari za kifo cha Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dk. John Magufuli kilichotangazwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Machi 17, majira ya saa tano usiku akiwa mkoani Tanga.
Zitto ameeleza hayo katika tamko lake rasmi na lenye saini yake linaloeleza zaidi kuwa Hayati Rais Dk. Magufuli wakati wa uhai wake amekuwa kiongozi wa nchi katika nyadhifa mbalimbali na kwa hakika alitekeleza wajibu wake kwa juhudi kubwa na kwamba taifa litamkumbika kwa mchango wake kwenye maendeleo ya nchi.
“Kwa niaba ya Chama cha ACT Wazalendo na kwa niaba yangu binafsi natoa pole kwa mama yetu Janeth Magufuli na familia nzima ya hayati John Pombe Magufuli, tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Natuma salamu zangu za rambirambi kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa na wanachama wa CCM kwa kuondokewa na mwenyekiti wao wa taifa.
“Natoa pole kwa Rais Mteule, ndugu Samia Hassan kwa msiba huu mzito kwa taifa letu. Katika nyakati hizi za majonzi makubwa tunamtakia rais mteule kheri, ujasiri na ushupavu katika kutekeleza majukumu yake,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Zitto.
Aidha, Zitto anaandika kuwapa pole watanzania wote kwa msiba mkubwa na kuwaombea wawe na moyo wa subira, mshikamano na umoja katika kipindi kigumu cha maombelezo.