![]() |
Mkuu wa Wialaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri |
NA MWANDISHI WETU
FLORA M’mbugu Schelling, mwekezaji Mtanzania anayemiliki eneo lenye uoto wa asili linalojulikana kwa jina la Ras Bamba, lililoko Kigamboni mkoani Dar es Salaam, amemlalamikia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri kuwa anatumia madaraka yake vibaya kumtisha na kuvamia eneo lake.
Schelling amedai kuwa DC Msafiri amekuwa akivamia eneo lake kwa madai kuwa anakwenda kulikagua huku akimshambulia mwekezaji huyo kwa maneno makali na kumtaka aliachie eneo hilo kwa hiari yake vinginevyo serikali itatumia nguvu kumnyang’anya bila kutoa sababu kwanini aliachie au kunyang’anywa.
Katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog, Schelleng amesema yeye na mumewe ambaye ni raia wa Uswiss aliyekuwa akifanya kazi Benki ya Dunia na aliyehusika kusimamia awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa barabara za mwendo kasi mkaoni Dar es Salaam, walinunua eneo hilo miaki mingi iliyopita na kuamua kutunza uoto wa asili uliokuwa katika eneo hilo.
Anasema eneo hilo ambalo liko ufukweni likiwa limejengwa hoteli, pia lina wana wanyama na ndege wa aina mbalimbali ambao wote wanatunzwa vizuri kwa gharama za mwekezaji wenyewe na kwamba walichonga barabara kurahisisha usafiri ndani ya eneo hilo.
Katika malalamiko yake hayo, Schelleng anasema baada ya Msafiri kuteuliwa kuwa DC wa Kigamboni alifika katika eneo lake la Ras Bamba na kuonyesha kulipenda kisha akawa anatembelea hapo kila mara huku akiwahoji wamiliki kama wana umiliki halali wa eneo hilo na namna walivyoweza kuutunza uoto wa asili katika eneo hilo pamoja na ndege na wanyama.
Anasema baada ya kumueleza DC huyo kuwa eneo hilo wanalimiliki kihalali, alianza kubadilika na kuwa mkali huku akisema mwekezaji haruhusiwi kumiliki eneo lenye uoto wa asili hivyo anapaswa kuhama vinginevyo serikali itamuhamisha kwa nguvu.
Schelleng anasema DC Msafiri baada ya kuona vitisho vyake vya maneno vinashindwa kufanikiwa alituma greda kwenda kuchonga barabara ndani ya eneo la Ras Bamba ambalo liliharibu kwa kiwango kikubwa eneo la uoto wa asili pamoja na kung’oa miti iliyotunzwa kwa muda mrefu baada ya kufanya uharibifu huo liliondoka.
“Barabara ipo, hiyo hapo, inakwenda mpaka ufukweni na nzuri tu. Lakini yeye baada ya kuona vitisho vyake sisi havitutikisi kwa sababu tunamiliki eneo hili kihalali alikwenda akatuma greda, likaja tukaelezwa linachonga barabara.
“Tulishangaa kwa sababu barabara ipo ila tulipoambiwa hiyo ni amri yake tukajua tu ni mwendelezo wa kutushughulikia. Lile greda liliharibu eneo la uoto wa asili na kung’oa miti ovyo kisha likaondoka bila kuchonga hiyo barabara yenyewe. Sasa yeye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya, ana mamlaka makubwa tu, hapa wilayani hatuna pengine pa kukimbili bali tulikwenda TAKUKURU,’ alisema Flora.
Anasema malalamiko yake TAKUKURU yalijibiwa kwamba ayapeleke baraza la ardhi ambalo linaweza kusikiliza na kutoa uamuzi mmiliki halali wa eneo hilo ni nani.
DC Msafiri ametumiwa maswali tisa ya kuomba ufafanuzi na majibu kuhusu malalamiko hayo ambayo licha ya kuonyesha kuwa ameyapata na kuyasoma hakujibu chochote na alipopigiwa simu kuombwa kuzungumzia suala hilo alisema ametingwa na kazi nyingi.
Tanzania Panorama Blog inaendelea kufuatilia sakata hili.