![]() |
Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli |
NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza siku 21 za maombolezo ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 17, mwaka huu, majira ya saa 12 jioni kutokana na maradhi ya moyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Machi 18 na kusainiwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, imeeleza kuwa sambamba na maombolezo ya siku 21, katika kipindi hicho, bendera za chama zitapepea nusu mlingoti na kutakuwa na kitabu cha salamu za rambirambi na maombolezo katika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma, Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM (OND) Lumumba jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa hiyo, CCM kimeeleza kupokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Rais Dk. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
“CCM kimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha ndugu John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa iliyotolewa na mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza ndg. Magufuli amefariki kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo, kitaalamu ‘Atrial Fibrillation.’
“Ndg John Pombe Joseph Magufuli amekuwa Mwenyekiti wa CCM kutoka mwaka 2016 mpaka umauti ulipomfika na amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka mwaka 2015 mpaka kifo chake.
“Wakuu wa chama, Mzee Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Mzee Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti Tanzania Zanzibar wameshauriana na kukubaliana kwamba Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itaketi kikao maalumu siku ya jumamosi, tarehe 20 Machi, 2021, saa 8 mchana katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM (OND) Lumumba jijini Dar es Salaam,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa wanachama wote wa CCM wawe na moyo mkuu, waendelee kuwa watulivu, wasimame imara na waendelee kutafakari mchango wa kipekee na wa kihistoria kwa taifa wa Rais Dk. Magufuli.
Inaelekeza shughuli za chama hicho zinazohusu uchanguzi ndani ya chama hicho kusimama kwa muda mpaka yatakapotolewa maelekezo mengine.