![]() |
Mmoja wa wakurugenzi wa MeTL, Mohamed dewji |
NA MWANDISHI WETU
SAKATA la kughushi nyaraka na sahihi, pamoja na utapeli linaloiandama Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) ya mkoani Dar es Salaam, sasa limewekwa wazi baada ya mdai, Kampuni ya Ravji Construction Limited ya mkoani Kilimanjaro kueleza namna mazungumzo ya kuuziwa kiwanja namba 105 yalivyoanza, makubaliano ya gharama za ununuzi, malipo yalivyofanyika, MeTL ilivyoghushi nyaraka na sahihi na kesi ilivyofunguliwa polisi.
Mlolongo wa madai haya ni mwendelezo wa kilio cha Kampuni ya Ravji Construction Limited inayodai kutapeliwa na MeTL maelfu ya Dola za Marekani katika mauziano ya kiwanja kilichopo eneo la Mbezi, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaaam na sasa inaomba huruma za Rais Dk. John Magufuli ili iweze kulipwa fedha ilizotapeliwa na MeTL.
![]() |
Rais, Dk. John Magufuli |
Govind Varsani Ravji, aliyeiwakilisha Kampuni ya Ravji Construction Ltd katika biashara hiyo ameieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa alikutana na mmoja wa wakurugenzi wa MeTL, Januari 2011 na kuzungumza kindugu kuhusu mauziano ya kiwanja hicho na kwamba walifikia makubaliano ya kukinunua kwa Dola za Marekani 700,000.
Ravji anasema baada ya kufikia makubaliano hayo, kampuni yake iliilipa MeTL kwa awamu, ambapo Machi Mosi, 2011, kupitia akaunti ya MeTL iliyopo Benki ya Standard Chartered, ilitumbukiza Dola za Marekani 200,000 na kupatiwa risiti yenye nambari 1181.
Huku akionyesha lundo la nyaraka alizokuwa nazo, Ravji anaeleza zaidi kuwa za Agosti 26, 2011 kampuni yake ilitumbukiza kwenye akaunti ya MeTL Dola za Marekani 200,000 na kupatiwa risiti yenye nambari 5051 na mwezi Disemba mwaka huo huo wa 2011, ilifanya malipo mara mbili, ikianza na yale iliyofanya Disemba 12 ilipotumbukiza Dola za marekani 100,000 na kupatiwa risiti nambari 7570 na Disemba 21, ilitumbukiza Dola za Marekani 100,000 na kupata risiti nambari 7833.
Anasema, hata baada MeTL kupokea kiasi hicho kikubwa cha malipo bado haikuweza kutoa hati ya kiwanja husika huku ikisisitiza kumaliziwa malipo yake yaliyosalia kwanza na kuonyesha jinsi ilivyokuwa na uhitaji wa fedha hizo, mmoja wa wakurugenzi wake anayedaiwa kuhusika moja kwa moja na sakata hilo, Murtaza Alihussein Dewji alimtumia Ravji ujumbe katika simu yake ya kiganjani ambao Tanzania PANORAMA Blog limeuona ukisomeaka hivi;
“Dear Ravjibhai. I am travelling and the title deed for Mikocheni plot no. 105 is ready with our cashier Mohamed Yusuf 075503…… Pls pay the balance of 2 peti and collect it. M.Dewji.”
Ravjia anasema alimweleza Murtaza kuwa watakuwa tayari kumalizia malipo hayo baada ya kupatiwa hati ya kiwanja lakini Murtaza aliibuka na kauli mpya kuwa kiasi kilichobaki ni Dola za Marekani 200,000 na kwamba hati hiyo imepotea hivyo aliomba apewe muda wa kufanya utaratibu wa kupata hati nyingine.
Anasema kuanzia hapo walianza kuvutana kabla ya MeTL kupitia kwa Murtaza kuibuka na hati ya makubaliano (MOU) ya ununuzi wa kiwanja iliyokuwa ikionyesha kuwa makubaliano yaliyofikiwa wawili ni hao katika kuuziana kiwanja hicho ni Dola za Marekani milioni 1.2.
![]() |
MOU inayodaiwa kughushiwa na MeTL |
Nyaraka hiyo (Memorandum of Understanding) ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeona inaonyesha kuwa makubaliano ya kuuziana kiwanja namba 105 kilicho Mbezi aneo la viwanda yalitiwa sahihi Machi Mosi 2011 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 1.2, siku ambayo Kampuni ya MeTL ilitumbukiziwa Dola za Marekani 200,000 na kampuni ya Ravji Construction Ltd.
Inasomeka zaidi kuwa malipo hayo yatafanyika kwa awamu tano na kwamba awamu ya kwanza tayari ilishafanyika tarehe hiyo ya makubaliano na zaidi kwamba, malipo yaingizwe kwenye akaunti ya MeTL.
“Kuwepo kwa nyaraka hiyo kulitushtua kwa sababu hatukuwahi kusaini makubaliano ya aina hiyo. Hivyo tulilazimika kufungua kesi ya kughushi hati na sahihi. Kesi hiyo ilikuwa na RB, inayosomeka WH/IR/2657/2014 ya Kituo cha Polisi Wazo Hill.
“Kesi hiyo nayo ina simulizi yake ambayo nitaitoa baadaye kwa sababu licha ya uchunguzi kukamilika, mpaka leo aliyebainika kughushi nyaraka na sahihi hajapata kufikishwa mahakamani. Sasa ndipo sisi tulipolazimika kuanza kusaka msaada kwa viongozi wetu, tumeanza kuhangaika muda mrefu kuomba msaada na tuliwahi kutoa tangazo kabisa gazetini tukiomba viongozi wetu watusaidie lakini huyu jamaa ana nguvu, bado tunahangaika kupigania haki yetu,” alisema.
Alipotafuwa mmoja wa wakurugenzi wa MeTL, Mohamed Dewji, maarufu kwa jina MO, simu yake ya kiganjani iliita bila majibu ingawa Tanzania PAMORAMA Blog lilikwishamtumia maswali kwenye simu yake ya kiganjani ambayo licha ya kuonyesha kuwa ameyapata na kuyasoma, hajapata kujibu chochote.
Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu wa MeTl, Hassan Dewji alipoulizwa, alisema yupo msibani hivyo hawezi kuzungumza chochote na kutoa namba ya mwanasheria ya kampuni aliyemtaja kwa jina la Catherineili ili aulizwe yeye.
Catherine Kisasa, mwanansheria wa MeTL alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani alisema ni kweli kampuni yake ilikuwa na mgogoro na kampuni ya Ravji ambayo ilikiuka makubaliano ya mauziano ya kiwanja hicho.
“Ni kweli, hilo jambo lipo, hawa tulifikishana mpaka mahakamani, tuliwauzia kiwanja hicho kwa gharama ya Dola za Marekani 600,000 lakini walilipa Dola za Marekani 300,000 kiasi kilichobakia wakashindwa kulipa, tukaanza kusumbuana mpaka tukawapeleka mahakamani ambako tuliyazungumza yakaisha.
“Ajabu ni kwamba kumbe wao walikuwa wamefungua kesi nyingine baada ya kushikwa masikio na watu, sasa kesi ile ya awali ilipoisha kukawa na kesi nyingine ambayo sisi tulishindwa kujua tunaingiaje, lakini nayo imeisha hivi karibini. Tuliwapa hadi hati ya kiwanja wale, tulisumbuana sana,” alisema Catherine.
Alipoulizwa kuhusu MOU ya mauziano ya kiwanja hicho iliyosainiwa na Murtaza kwa niaba ya MeTL inayoonyesha mauziano ya kiwanja hicho ni Dola za Marekani milioni 1.2 na kwamba MOU hiyo ilichunguzwa na kubainika kuwa ilikuwa ya kughushi alisema anaomba arejee kwenye mafaili yake kwanza kabla ya kujibu na kuomba apewe saa moja ndipo apigiwe tena.
Alipopigiwa Catherine baada ya saa moja alisema hawezi kuzungumza chochote mpaka atakapoonana na mwandishi uso kwa uso huku akihoji jina la mwandishi na taasisi anayofanyia kazi.
Juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC) Ramadhani Kingai aliieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa amemuagiza Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinal (RCO) Kinondoni kufuatilia faili la tuhuma za kughushi zinazowaandama baadhi ya mabosi wa MeTL lilikwama wapi na kuahidi kutoa taarifa mwishoni mwa wiki hii.
TANZANIA PANORAMA BLOG INAENDELEA NA UCHUNGUZI WA KASHFA HII AMBAPO KESHO ITARIPOTI JINSI UCHUNGUZI WA MAKACHERO WA POLISI ULIVYOBAINI SAHIHI ILIYOGHUSHIWA NA METL KATIKA MOU ILIYOSAINIWA NA MURTAZA ALIHUSSEIN DEWJI KWA NIABA YA METL