![]() |
Gari hili linapakiwa shehena ya bidhaa kutoka ndani ya stoo ya duka la SK STORE |
NA MWANDISHI WETU
DUKA moja la kuuza bidhaa za jumla linalofahamika kwa jina la SK STORE lililopo eneo Mwembechai, Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam, linaendeshwa kimaajabu.
Mmiliki wa duka hilo ametajwa kwa jina la Salum Khamis ambaye hupatikani dukani hapo kwa nadra na hata anapokuwepo, gari lake huegeshwa mbali na mara nyingi huegeshwa katika kituo cha mafuta cha mwembechai.
Uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog umebaini kuwa duka hilo linafahamika kwa jina la SK STORE na linahudumia maelfu ya wafanyabiashara wa kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika uchunguzi wake, Tanzania PANORAMA Blog imebainika kuwa SK STORE linatumia namba ya mlipa kodi aliyesajiliwa Wilaya ya Ilala na risiti za kielektoniki linazotoa kwa wateja wake zinasomeka kuwa ni za duka lililo nje ya Wilaya ya Kinondoni.
Sambamba na hayo, uchunguzi umeonyesha zaidi kuwa duka hilo kwa sasa linatumia jina la mfanyabiashara mwingine na kwamba limekuwa likibadilisha majina ya biashara mara kwa mara ili kukwepa kulipa kodi.
Aidha, duka hilo linalodaiwa kuwa moja wa biashara zinazoongoza kwa ukwepaji kodi jijini Dar es Salaam na kwamba kuna biashara nyingine iliyojificha ambayo hufanyika dukani hapo.
![]() |
Sehemu ya mbele ya duka la SK STORE |
“Sisi tunalifahamu kama duka la SK STORE, ndilo jina lake la siku zote lakini kwenye vitabu vyao wameishabadilisha jina. Hivi sasa wanatumia jina la mtu mwingine ambaye ni mafia mwenzao. Na limekaa katika eneo ambalo limejifichajicha hivi siyo rahisi sana kwa mtu ambaye siyo mwenyeji kuligundua.
“TIN Number wanayotumia siyo ya kwao, risiti za EFD wanazotoa siyo za kwao, ulipaji wao wa kodi wanajua wenyewe, mzigo wanakopata wanajua wenyewe. Hilo ni duka la maajabu. Ni mfanyabiashara mwenzetu tunamjua kwa sababu tunajuana.
“Hapo ukiingia kujifanya unawafuatilia au unachunguza biashara yao kesho tu unapewa kesi nzito unaishia jela. Kuna wazito nyuma ya hilo duka. Hapo kuna kamera zinarekodi watu wote wanaofika hapo, sasa wakiona wewe ni hatari kwao wanachukua picha yako wanaituma kwa wenye nguvu, huchukui ‘round’ unaning’inizwa,” alisema mmoja wa watoa taarifa.
Alipoulizwa juzi meneja wa duka hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Suleiman alisema mtu anayeweza kuzungumza kuhusu tuhuma hizo ni bosi wake ambaye ndiye mmiliki wa duka hilo.
Suleiman ambaye alikataa kutaja jina la bosi wake alisema amekwenda hospitali na kuitaka Tanzania PANORAMA Blog kubadilishana naye namba za simu ili atakaporejea aifahamishe.
![]() |
Duka la SK STORE lililoko Magomeni Mwembechai |
“Haya mambo wazee naona anayeweza kuyazungumzia ni bosi mwenyewe. Kwanini usimuulize bosi. Kwa sasa yupo hospitali amekwenda kucheck afya yake Ila akirudi tu ntamfahamisha ili mje mzungumze naye yeye. Nipe namba zenu akirejea tu nawapigia mje,” alisema Suleiman.
Hata hivyo, Suleiman ambaye namba yake ya simu imesajiliwa kwa jina la Felix Shayo hakutekeleza ahadi hiyo na alipotafutwa kwa simu yake aliyokuwa ametoa namba alipokea lakini baada ya kuelezwa anayepiga ni mwandishi alisema mpigaji amekosea namba kisha akakata
Alipotafutwa baadaye simu haikuwa hewani.
Tanzania PANORAMA Blog linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu duka hilo la ajabu.