Tuesday, July 1, 2025
spot_img

‘SARAKASI’ ZA TFC KASHFA YA MIKATABA YA MBOLEA

 

Shehena ya mbolea


NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) sasa inacheza mchezo wa sarakasi ikionyesha umahiri wake wa kukwepa au kuvuta muda wa kuisaka popote ilipo mikataba ya biashara ya mbolea yenye thamani ya mibilioni ya shilingi iliyoingia baina yake na Kampuni ya Export Trading Group (ETG), (INPUT) ya jijini Dar es Salaam.

 Mikataba hiyo inayodaiwa kughubikwa na vitendo vya kifisadi ilianza kutafutwa mapema Disemba, 2020 baada ya Tanzania PANORAMA Blog kumfikia ofisini kwake Meneja wa TFC,  Kanjel Mloba ikiwa na maswali na baadhi ya nyaraka mkononi na kumuomba ufafanuzi kuhusu madai ya kuwepo kwa vitendo vya ufisadi wa kutisha katika mikataba hiyo.

Katika majibu yake, Kanjel alisema yeye ni mgeni, ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi, mikataba ya mauzo ya mbolea baina ya ETG na TFC hajaiona na kwamba afya yake ilikuwa imeyumba hivyo aliomba apewe muda kuitafuta mikataba hiyo na pia kwenda hospitali kutibiwa huku akiahidi kuweka kila kitu hadharani Disemba 5, 2020, ahadi ambayo hakuitekeleza na hajaitekeleza hadi sasa.

Januari 21, 2021, Tanzania PANORAMA Blog iliripoti habari ya kupotea kwa mikataba hiyo katika Ofisi za Makao Makuu ya TFC zilizoko Oysterbay jijini Dar es Salaam inayohusisha biashara ya mbolea iliyofanywa baina ya serikali ya ETG kuanzia mwaka 2016.

Katika habari yake hiyo, Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa mikataba hiyo ilianza kutafutwa ofisini kwa meneja Kanjel Disemba 5, 2020 bila mafanikio na baadaye katika ofisi za wasaidizi wake ambako pia haikupatikana kabla ya kuiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa haionekani.

Muda mfupi baada ya kuripotiwa kwa habari hiyo, Kanjel aliwasiliana na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kile alichodai ni masikitiko yake kwa kukaririwa akiungama kuhusu kupotea kwa mikataba hiyo lakini Tanzania PANORAMA Blog ilimkumbusha kwa kurejea maandishi yake liliyoyatunza vema yaliyokuwa yakielezea kutopatikana kwa mikataba hiyo.

Baada ya mnyukano mkali, Kanjel alisema amesafiri kikazi na kuomba apewe muda tena aendelee kuitafuta mikataba hiyo huku akitoa ahadi mpya ya kukutana na Tanzania PANORAMA Blog kujibu maswali iliyokuwa imemtumia kwenye e mail yake kama alivyokuwa ameagiza mapema disemba 2020.

Januari 27, 2021, Tanzania PANOROMA Blog iliwasiliana na Kanjel ikimkumbusha kujibu maswali iliyomuuliza lakini alisema bado yuko Dodoma, atapiga simu mwishoni mwa wiki baada tu ya kuwasili ili kupanga miadi ya kuonana kikazi.

Februari Mosi, 2021, Kanjel alikumbushwa tena kuhusu ahadi zake na kusisitiza kuwa mara tu anapoingia mjini Dar es Salaam atapiga simu kama alivyoahidi.

Februari 7, 2021 Tanzania PANORAMA Blog iliwasiliana na Kanjel ikimtaka kutimiza wajibu wake kwa kujibu maswali aliyoulizwa na yeye alisema ni kweli aliingia mjini Dar es Salaam Februari 6, 2021lakini anaondoka Februari 8 kwenda kwenye kikao na kuagiza kuwa atafutwe meneja biashara wa kampuni yake aliyemtaja kwa jina la Siara kujibu maswali kwa sababu mikataba sasa imepatikana.

Hata hivyo, Kanjel ambaye alitoa namba ya simu ya Siara alielekeza atafutwe jumanne ya februari 9, 2020 kwa madai kuwa ni mgonjwa lakini siku hiyo ya jumanne anaweza kuwepo ofisini.

Alipotafutwa Siara kupitia simu yake ya kiganjani alisema yeye yu mgonjwa mahututi hivyo hawezi kuzungumza lolote na hajui anaweza kuwepo ofisini lini kisha alitoa ombi la kuombewa kwa sababu hajui ni nini kitamtokea katika siku chache za usoni.

Kanjel alipopewa taarifa hizo kuhusu Siara na kupewa nafasi ya kutoa maelekezo mengine ili majibu yapatikane, hakujibu.

AWALI, Tanzania PANORAMA Blog iliripoti kuwa kupotea kwa mikataba hiyo kulibainika baada ya Kanjel kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog, mapema Disemba, 2020, iliyoomba ufafanuzi kuhusu madai ya kuwepo ufisadi mkubwa katika biashara ya mbolea baina ya TFC na ETG.

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORANA Blog zilidai kuwa kwa miaka mingi ETG imekuwa ikiiuzia serikali mbolea kupitia TFC na kuchuma mabilioni ya fedha kwa kufanya udanganyifu katika shehena inayochukuliwa na serikali kutoka kwa ETG.

Kwamba, TFC huwa inasaini mikataba ya kununua tani nyingi za mbolea kutoka ETG lakini kiuhalisia TFC huchukua tani kidogo na kuacha nyingine ambazo  huuzwa kwa wateja wengine.

Inadaiwa zaidi kuwa, licha ya TFC kuchukua kiasi kidogo cha mbolea na kuacha nyingine ikiuzwa kwa wateja wengine, ETG hupeleka hati za madai za kulipwa tani zote za mbolea zilizo kwenye mkataba pamoja na gharama za kuhifadhi (Storage) kwa mbolea ambayo haikuchukuliwa na TFC.

Moja ya nyaraka, miongoni mwa zinazoelezea kuwepo kwa ufisadi huo ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona, inasomeka hivi; ‘wizi mkubwa umekuwa ukifanyika eneo la confirmation debit. Wizi umefanyika miaka yote kwa kulipia mbolea hewa.

‘Kwenye deni la USD 3.1 milioni, kuna mbolea ambayo haikuchukuliwa na TFC ambapo meneja wa TFC, Ndg, Salum Mkumba (sasa amestaafu) na Meneja wa ETG (INPUTS) Ndg Manoj, walitakiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo waandae taarifa ili kupata deni halali, wao hawakutekeleza agizo hilo kwa lengo la kuficha ufisadi wao.’

Kanjel alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog mapema mwaka jana kuhusu tuhuma hizo alisema ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi, mikataba ya mauzo ya mbolea baina ya ETG na TFC hajaiona.

Alisema hayupo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza au kuitafuta mikataba kwa wakati huo kwa sababu alikuwa akijisikia vibaya na alikuwa akijiandaa kwenda hospitali kwa matibabu hivyo atafutwe Disemba 5, 2020 atakuwa amekwishaitafuta na kuiperuzi mikataba yote kuona kama ina dosari yoyote au lah ndipo atoe kauli yake.

Disemba 5, 2020 Tanzania PANORAMA Blog iliwasiana na Kanjel kumuuliza kuhusu alichogundua kwenye mikataba baina TFC na ETG kama alivyokuwa ameelekeza lakini alisema bado anaumwa.

Disemba 7, 2020 Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Kanjel kwa mara nyingine na yeye alisema bado hayuko vizuri na kuelekeza atumiwe maswali kwenye e mail yake ili aweze kuyatafutia majibu jambo ambalo Tanzania PANORAMA Blog ililitekeleza.

Disemba 10, 2020 Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Kanjel kuomba majibu ya maswali yake na yeye alijibu mikataba hiyo haionekani hivyo bado anaitafuta na amewaelekeza pia wasaidizi wake waitafute.

Disemba 11, 2020 Tanzania PANORAMA Blog lilimuuliza Kanjel iwapo mikataba husika imepatikana na yeye alijibu kuwa bado anaumwa na mikataba haijapatikana.

Disemba 15, 2020 Kanjel alitafutwa tena na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu suala hilo hilo na kujibu kuwa amesafiri kikazi kwenda mkoani Dodoma lakini mikataba hiyo haijapatikana bado inatafutwa.

Januari 13, 2021 Tanzania PANORAMA Blog liliwasiliana tena na Kanjel na kumuuliza iwapo mikataba hiyo imepatikana na kumkumbusha kujibu maswali aliyotumiwa na yeye alisema mikataba hiyo haipo.

Alipoulizwa Afisa Masoko ya Kampuni ya ETG, aliyejitambulisha kwa jina la Salome Ncheye kuhusu madai hayo alihoji kwanini jambo hilo linafuatiliwa sasa.

“Haya mambo yalifanyika huko nyuma, kwanini unayafuatilia sasa? Wakati yanafanyika mlikuwa wapi? Hiyo mikataba wewe unayo, unaweza kuitoa ukaonyesha kuthibitisha kama hiyo biashara ilikuwepo?

“Tambua hiyo ni mikataba ya siri, nakushangaa unauliza kama umewahi kuiona. Hiyo mikataba nakwambia ni siri baina TFC iliyosaini kwa niaba ya serikali ya muuzaji ETG, wewe umeiona wapi? Kuna nini hapa katikati? Umetumwa na nani? Sisi tunafanya biashara sana na serikali. Nikushauri tu, achana na mamboyasiyokuhusu,” alisema Salome.

Tanzania PAMORAMA Blog itaendelea kuripoti sakata hili kulingana na mwenendo wa uchunguzi inayoufanya.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya