NA MWANDISHI WETU
TUHUMA mpya za ufisadi zimeanza kuibuliwa katika Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), safari hii zikielekezwa kwa kigogo mmoja mstaafu anayedaiwa kukimbia kwenye utumishi wa shirika hilo baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.
Imedaiwa na vyanzo vya habari vilivyo karibu na kigogo huyo mstaafu kuwa alijihusisha na ukwapuaji wa mali za shirika hilo pamoja na matumizi mabaya ya ofisi wakati akiwa mtumishi wa ngazi ya mkurugenzi katika TPDC.
Kwamba kigogo huyo mstaafu (jina tunalihifadhi kwa sasa) alijimilikisha mali nyingi za TPDC zikiwemo nyumba kumi za shirika zilizouzwa, sambamba na kukwapua fedha nyingi kabla ya kuacha kazi ghafla ili kukwepa hatua zilizokuwa zikichukuliwa na serikali ya awamu ya tano dhidi ya watumishi wa umma waliojihusisha na vitendo vya ufisadi.
“Isieleweke kuwa nina husda naye au vyovyote vinginevyo, hapana. Huyu mzee ni mzee wangu, ni ndugu yangu, ninamjua. Ila aliyoyafanya si sawa na naungama kwamba alitutumia vibaya wakati ule kufanikisha mambo yake.
“Najua wapo waliopata kufikishwa mahakamani katika shirika hilo kwa tuhuma mbalimbali ila hapa sitaki kuongelea kesi za hao. Serikali ifanye uchunguzi kwa baadhi ya wastaafu waliokimbia kwenye utumishi baada ya kuanza kwa vita dhidi ya ufisadi. Iangalie fedha walizonazo kwenye akaunti zao benki kama zinalingana na kipato walichokuwa wakikipata.
“Nikupe mfano wa huyu mzee wetu. Yeye wakati wa uuzwaji wa nyumba za TPDC zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam alikuwa bosi pale na alijiuzia nyumba kumi lakini kwenye karatasi zao huko kaandika alinunua nyumba tatu tu. Uchunguzi ukifanyika serikali itajua kila kitu.
“Kuna watumishi wanaulizwa kuhusu mali nyingi walizochuma wakiwa kwenye utumishi katika ofisi za umma na inapobainika hawana maelezo ya kuridhisha hatua zinachukuliwa dhidi yao lakini wapo ambao hawajaguswa kama huyu. Sasa huyu ngoja nikutajie kwa uchache mali alizochuma akiwa ofisini TPDC.
“Ana majumba Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Arusha. Ana mashamba makubwa sehemu mbalimbali nchini
Arusha ana maghorofa huko Njiro, Tanga ana nyumba maeneo ya Kange alizonunua kwenye mnada wa benki, Morogoro ana nyumba huko Kihonda na mjini.
 “Ana watoto wawili wa jinsia ya kike aliowasomesha Marekani na wamechukua uraia wa huko. Hivi kwa kipato cha kawaida mkurugenzi anaweza kusomesha watoto wawili Marekani na kununua majumba katika mikoa yote hiyo hapa nchini?
“Kuna jambo nalikamilisha ili nisiingilie mambo ya mahakama kwa sababu kulikuwa na kesi ya familia mahakamani baina yake na mkewe, nitakuja kukupa kila kitu,” alisema mmoja wa watu wa karibu na kigogo huyo mstaafu.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na madai hayo, kigogo huyo hakukubali wala kukanusha bali alisema anawapa kazi watu wake wamuandalie majibu.
Alisema anashangaa kufuatiliwa sasa wakati amestaafu miaka mingi iliyopita.
“Nimewapa watu wangu waniandalie majibu kama wataniletea majibu on time well and good, wameleta majibu out of time well and good,” alisema.
Alipoulizwa tena baadaye kama amepatiwa majibu na watu wake aling”aka kwa ukali na kuonya asifuatiliwe.
Tanzania PANORAMA Blog inafanya uchunguzi wa kina wa uuzwaji wa nyumba za shirika hilo unaodaiwa kughubikwa na mizengwe na ufisadi kabla ya kuchapisha ripoti yake.