Wednesday, December 25, 2024
spot_img

MAJIBU YA MASWALI YALIYOLETWA NA WWF NA UNESCO

 

RIPOTI MAALUMU (4)

Hii ni sehemu ya nne ya ripoti maalumu ya utafiti wa kitalaamu kuhusu hofu, majibu ya hofu, athari za mazingira, mipango ya kudhibiti athari za mazingira, faida baki za mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere na unafuu wa gharama za umeme kwa Taifa la Tanzania baada ya mradi huo kuanza kufanya kazi.

 

Dk. Thomas Kashilalih

SALEH PAMBA, DK. ABUBAKAR RAJABU, *ABDULKARIM SHAH* DK. MAGNUS NGOILE NA DK. THOMAS KASHILILAH

MAMLAKA ya Mfuko wa Wanyamapori Ulimwenguni (WWF) na Uongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na

Utamaduni (UNESCO), kwa nyakati tofauti, walibainisha wasiwasi wao baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuamua kuendeleza Mradi wa Umeme wa Maji wa Korongo la Stiegler.

Kwa upande wake, UNESCO ilionyesha dukuduku kadhaa. Mosi, UNESCO ilisema: zabuni inayotoa kibali cha ukataji wa miti kwa hekta 143,638 ndani ya hifadhi, inaonyesha kuwa ukataji miti mkubwa utakaotokea ni hatari ya dhahiri kwa hifadhi kulingana na aya ya 180 ya miongozo ya uendeshaji hivyo UNESCO inaamua kuliweka suala hili miongoni mwa sababu za kuendelea kuijumuisha hifadhi hiyo kwenye orodha ya urithi wa dunia ulio hatarini.

Pili, UNESCO ilisisitiza tena msimamo wake kwamba, ujenzi wa mabwawa yenye ujazo mkubwa ndani ya mipaka ya hifadhi ambazo ni urithi wa ulimwengu haiendani na hadhi ya hifadhi ambazo ni urithi wa dunia, haiendani na dhamira iliyotolewa na serikali ya Tanzania wakati mabadiliko ya mipaka ya hifadhi hiyo yalipopitishwa mnamo 2012, inakiuka katazo la kutokufanya shughuli zozote za maendeleo ndani ya Pori la Akiba la Selous na eneo lake la bafa bila idhini ya awali ya Kamati ya Urithi wa Dunia.

Hivyo, UNESCO inasisitiza ombi lake kwa Serikali ya Tanzania kutathmini kikamilifu athari za jumla za mradi wa umeme wa maji katika maporomoko ya Stiegler na mazingira yake mapana kupitia tathmini ya mkakati ya mazingira, ambayo itafanywa kwa viwango vya juu zaidi vya kimataifa bila kusahau kuchukua hatua za kuangalia njia mbadala ili kukidhi mahitaji yake ya kuzalisha wa umeme.


Tatu, UNESCO ilisema Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha kuwa uvunaji wa magogo uliopangwa na shughuli zingine zote zinazohusiana na mradi wa umeme wa maji katika maporomoko ya Stiegler, ambao utaathiri thamani bora ya ulimwengu ya hifadhi kwa kiwango ambacho kitakuwa kingumu kukarabatiwa, usiendelee kabla ya kukamilika kwa tathmini ya mkakati ya mazingira na uhakiki wake na IUCN, na UNESCO inaiomba Serikali ya Tanzania kukaribisha uongozi wa kituo cha urithi wa dunia pamoja na tume ya ukaguzi ya IUCN kuja kukagua maendeleo ya mradi, kutathmini hali ya uhifadhi wa mazingira na kusaidia kukamilisha hali inayotarajiwa ya uhifadhi wa mazingira ili kufungua milango kwa ajili ya kuiondoa hifadhi kutoka katika orodha ya urithi wa dunia ulio hatarini.

Aidha, UNESCO ilionyesha dukuduku juu ya uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuingia mkataba na kampuni ya Misri ili kutekeleza mradi huu.

Magogo ya miti


Dukuduku zilizoibuliwa na WWF, zikiwemo kubwa na ndogo, zilitokana na uelewa wao kwamba msanifu wa mradi na mkandarasi ni

Kampuni ya Brazil inayoitwa Odebrecht ambayo tayari ilionyesha nia ya utekeleza mradi wa umeme wa maji katika maporomoko ya Stiegler mnamo 2013 chini ya utaratibu wa kuzalisha na kuuza umeme kwa serikali.

Kwa hivyo majibu yetu yatakuwa katika hatua mbili, tukianza kwa kujibu dukuduku za WWF na kisha zile za UNESCO.

MAJIBU KWA DUKUDUKU ZILIZOONYESHWA NA WWF

Shirika la WWF lililalamika juu ya uwezekano wa mafuriko kufunika makazi ya viumbehai yaliyoko nchi kavu kutokana na bwawa kubwa litakalofunika eneo la kilometa za mraba 1,200.

Shirika hilo liliongelea athari za mlolongo wa mabadiliko yatakayotokea kwenye sehemu za chini za mto.

Mfano lilitaja mabadiliko ya kimsimu katika ujazo wa maji yanayotiririka kama yakipimwa katika mita za ujazo wa maji yanayotiririka kwa mwaka.

Walitaja pia, athari za mabadiliko ya kimsimu katika ujazo wa mashapo kama yakipimwa katika tani zinazosombwa na mto kwa mwaka.

Walisisitiza kuwa, mabadiliko haya huenda yakasababisha mabadiliko katika jiomofolojia ya njia za mto, upunguzaji wa bayoanuwai ya majini na kupungua kwa huduma za mfumo wa ikolojia kwa viumbe ambavyo wakazi wa nusu ya chini za mto.

Hoja yao ilikuwa kwamba, kwa kuwa kiasi cha maji na mashapo yanayopelekwa baharini ni sababu kuu zinazodhibiti michakato ya kiikolojia katika pwani, kwenye delta, kwenye maji ya bahari, pamoja na mazingira ya ukanda wa pwani, basi, mito inachukuliwa kama kiunga

Mafuriko


kikuu kati ya mabara na bahari, ambacho hutekeleza jukumu muhimu katika michakato ya kijiolojia, kibaolojia na kemikali kwenye uso wa ardhi.

Katika mazingira haya, waliashiria, usafirishaji wa maji na usafirishaji wa mashapo katika mito huathiri sana jiomofolojia ya njia za mito, nyanda za delta na hupeleka mashapo mengi kutoka nchi kavu kwenda bahari, ambavyo kwa pamoja hudumisha mazingira ya kiikolojia yaliyoko pwani na baharini.

Waliashiria tena kuwa, katika karne iliyopita, mifumo mingi ya mito ulimwenguni ilipitia mabadiliko makubwa kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli kubwa za kibinadamu zilizojumuisha mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kanuni za mito, uondoaji wa maji, uharibifu, na uchimbaji mchanga.

Kwa hivyo, walionekana kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kisayansi na wa kimazoea kuelewa mabadiliko ya mifumo ya mito na kutathmini sababu za kudhibiti mabadiliko hayo, kwani uchambuzi wa kimahesabu kuhusu mabadiliko ya msimu katima eneo la kijiografia unaweza kutoa rejea nzuri ya kupunguza mafuriko, kuboresha mkondo wa mto na usimamizi bora wa bonde la mto katika siku zijazo.

Kwa kifupi, WWF walionyesha wasiwasi juu ya uhusiano kati ya ukubwa wa bwawa na eneo la mafuriko yanayoweza kutokea kutokana na ukubwa huo; athari za miundombinu ya mradi; idadi kubwa ya wafanyikazi wa mradi; athari za mradi katika usafirishaji wa mashapo na madhara yake kwa mofolojia ya mto; na mambo anwai yanayohusiana na ubora wa maji.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya