Bwawa la Julius Nyerere |
RIPOTI MAALUMU (3)
HII ni sehemu ya tatu ya ripoti maalumu ya utafiti uliofanywa na watalaamu bingwa wazalendo dhidi ya hekahela za wazungu za kutaka kuzuia ujenzi wa mradi mkubwa wa bwawa la Julius Nyerere katika Mto Rufiji.
Ripoti hii ni matokeo ya fitna za wazungu zilizowainua wataalamu bingwa wa kitanzania wanaotambulika na jumuiya za kimataifa kwa usomi wao kufanya utafiti dhidi ya fitna na uzushi huo uliokuwa na lengo la kuikwamisha serikali.
Magwiji hao wamefanyia utafiti hoja zote za wazungu zilizolenga kukwamisha jitihada za Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi wa umeme wa maji katika Mto Rufiji na kuandika ripoti ya kina inayojibu upotoshaji wa wazungu.
Ni ripoti iliyofanyiwa utafiti wa kitalaamu kuhusu hofu, majibu ya hofu, athari za mazingira, mipango ya kudhibiti athari za mazingira, faida baki za mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere na unafuu wa gharama za umeme kwa Taifa la Tanzania baada ya mradi huo kuanza kufanya kazi.
Dk. Thomas Kashililah |
SALEH PAMBA, DK. ABUBAKAR RAJABU, *ABDULKARIM SHAH* DK. MAGNUS NGOILE NA DK. THOMAS KASHILILAH
Athari za mradi zilizoibuliwa na WWF na UNESCO zilianzia kwenye pendekezo la kwanza la Kampuni ya Brazil inayoitwa Odebrercht, ambayo ilionyesha nia ya kujenga mradi wa umeme wa maji katika Korongo la Stiegler’s baada ya uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.
Mtekelezaji huyu wa mradi (Odebrercht) alikusudia kufadhili gharama za mradi huo chini ya Mkataba wa Ununuzi wa Umeme (PPA) na Kampuni ya Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).
Lakini, kampuni hiyo ya Brazil iliuacha mradi huo baada ya kuibuka madai ya ufisadi katika miradi yake iliyo sehemu baki ulimwenguni.
Pia ilikumbwa na ukosefu wa fedha hivyo makubalino yake na serikali yakafutwa.
Kwa kuzingatia mahitaji ya umeme yanayoibuka kwa sababu ya harakati mpya ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kuelekea uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli iliamua kukabiliana na ongezeko kubwa la matumizi ya umeme kwa sababu ya matumizi ya viwanda na biashara kwa kufufua mradi huu.
Rais Dk. John Magufuli |
Uamuzi huu ulisukumwa na sababu zingine tatu na vipaumbele kadhaa mbali na uzalishaji wa nishati kwa ajili ya matumizi ya viwandani.
Moja, serikali ilitaka kutoa umeme kwa bei nafuu kwa jamii za vijijini ifikapo mwaka 2025 na kutoa maji safi kwa wote. Pili, serikali ilitaka kusambaza umeme wa bei nafuu na endelevu kwa ujenzi unaoendelea wa vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya, kila moja kuwa na vifaa vya kisasa.
Umeme vijijini |
Na tatu, serikali ilitaka kusaidia ujenzi wa mfumo wa reli ya kiwango ya mwendo kasi (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma.
Katika mazingira haya, serikali ilitafiti uhitaji wa kutumia umeme wa gharama nafuu za uzalishaji, wenye bei rahisi na endelevu. Hatimaye serikali ilibainika kwamba kwa kuangalia gharama ya kuzalisha yuniti moja ya umeme, umeme wa maji ulikuwa ndio wenye gharama za chini kabisa, yaani shilingi 36 kwa kila yuniti.
Kwa upande mwingine, ilibainika kwamba uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nyuklia ni shilingi 65; kwamba, uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nguvu ya upepo ni shilingi 103.05; uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nguvu ya jua ni shilingi 103.05; uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nguvu ya mvuke ni shilingi 114.50.
Umeme wa upepo |
Pia uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nguvu ya makaa ya mawe ni shilingi 118; uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa gesi asilia ni shilingi 147 na uzalishaji wa yuniti moja ya umeme wa nguvu ya mafuta ya kioevu ni shilingi 546.
Bila kujali ukubwa wa hifadhi ya gesi asilia na ukubwa wa hifadhi ya makaa ya mawe nchi iliyonayo, nishati ya umeme wa maji ina gharama ya chini zaidi kwa kila yuniti. Kwa hivyo ni busara kutumia nishati ya umeme wa maji kwenye kaya, viwandani na katika biashara.
Ni ufahamu wetu kwamba wakati ulimwengu ulioendelea ulipoanza kuzalisha Nishati ya Nyuklia walikuwa wanatafuta umeme endelevu na mkubwa ili kuwezesha maendeleo yao ya viwandani na kukidhi mahitaji ya kiuchumi ya kijamii licha ya changamoto zilizojitokeza pamoja na teknolojia za nyuklia, changamoto hizo baadaye zilitatuliwa.
Vivyo hivyo, mradi wa umeme wa maji katika Mto Rufiji pia una changamoto kadhaa ambazo zinaweza kupunguzwa kama ilivyokuwa kwenye uzalishaji wa nguvu ya nyuklia huko Ulaya.
Tanzania imesaini Mkataba wa Urithi wa Dunia wa 1972; ni mwanachama wa Jumuiya ya Kimataifa ya Uhifadhi na Maumbile (IUCN); pia ni mwanachama aliyejitolea kabisa na anafuata kanuni na masharti ya muungano huu; na hajawahi kukiuka kanuni za uhifadhi wa mazingira.
Msimamo huu unaonyeshwa wazi na uamuzi wake wa kutenga sehemu kubwa ya ardhi kwa ajili ya hifadhi licha ya kilio cha umma kudai ardhi zaidi kwa kilimo na mifugo.
Kwa mfano Tanzania imetenga asilimia 40.5 karibu kilometa za mraba 383,000 ya ardhi yake kwa uhifadhi, na asilimia 29.5 ya hizi kilometa za mraba ambayo ni sawa na kilometa za mraba 279,000, imetengwa kwa ajili ya usimamizi wa wanyamapori.
Eneo hili kwa ajili ya usimamizi wa wanyamapori linahusisha maeneo 28 ya uwindaji, maeneo 42 yanayodhibitiwa na maafisa wa wanyama pori, na maeneo 38 ya usimamizi wa wanyamapori.
Pia inajumuisha asilimia 11, yaani kilometa za mraba 104,000 kwa ajili ya maeneo manne ambayo ni vitalu vinavyosimamiwa chini ya Mkataba wa Ramsar, hifadhi za misitu zinazofunika kilometa za mraba 35,257 na mbuga za baharini.
Kwa hivyo uamuzi wa serikali kutumia kilometa za mraba zipatazo 1,000, ambazo ni sawa na asilimia 0.2 ya ardhi iliyotengwa kwa uhifadhi ambayo sawa ni sawa na asilimia 2 ya kilometa za mraba 50,000 za Pori la Akiba la Selous, kujenga bwawa ambalo litazalisha jumla ya MW 2115, limepingwa na baadhi ya Taasisi za Kimataifa bila sababu za msingi, bila kutaja kuenea kwa matumizi ya nishati ya kuni, ambayo haiendani na kanuni za utunzaji wa mazingira, ambazo tayari Tanzania imeahidi kuziheshimu.
Hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania ni pamoja na sheria anuwai zilizotungwa kulinda maliasili, kuweka wizara kamili zinazohusika na uhifadhi wa mazingira, ambapo wizara iliyotajwa inaongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linaripoti katika wizara hii. Na katika siku za hivi karibuni serikali ilibadilisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na kuipa hadhi inayokaribiana na hadhi kamili ya kijeshi ili iweze kupambana na vitisho vyovyote vya ujangili kwa kutumia nguvu zilizo karibu sawa na nguvu za jeshi.
Watalii wakiwa Selous |
Idadi ya watalii katika Pori la Akiba la Selous itaongezeka kwa sababu ya ujenzi wa Bwawa la Umeme la Stigler’s, kutokana na ujenzi wa barabara zinazopitika kwa mwaka mzima kwenda na kutoka katika hifadhi, na kwa ajili ya kuimarika kwa usalama ndani na karibu na mfumo wa Ikolojia wa Hifadhi.
Kwa hiyo, bila hata kuangalia masuala mengine, bwawa la Stiegler’s peke yake litakuwa kivutio kwa wageni wa ndani na nje. Kuhusu jambo hili, tayari tumeona miradi kadhaa inayofanana ulimwenguni ambayo inavutia mamilioni ya watalii hata bila wanyamapori.
Mifano ni pamoja na Bwawa la Akasombo huko Ghana, Bwawa la Kariba linalopakana na Zambia na Zimbabwe, Bwawa la Cabora Bassa huko Msumbiji, Bwawa la Inga huko DRC na Bwawa la Owen Falls huko Uganda.
Bwawa la kuzalisha umeme la Akosombo, Ghana |
Pia kuna mabwawa ya Bhakra-Nangal, Idukki, Srisailam, Tehri, Hirakund na Nathpa Jhakri nchini India. Nchi za Pakistan, Canada, Cameron, China, USSR, USA, Kenya na Afrika Kusini zina mabwawa kama haya.
Kwa hiyo tunatarajia watalii zaidi kutembelea Hifadhi ya Wanyama ya Selous kuona wanyama pori na Bwawa la Umeme la Stiegler’s.
Usalama katika Pori la Akiba la Selous utaimarishwa wakati na baada ya ujenzi wa bwawa, na hii itaongeza thamani kwa shughuli zilizopo za kupambana na ujangili ambazo kwa sababu yake, tumeona ongezeko kubwa la tembo katika miaka miwili iliyopita.
Lakini, sababu zinazoambatana na kupungua kwa tembo katika mfumo wa Ikolojia wa Hifadhi hapo zamani hazihusiani na ujenzi wa bwawa, kama inavyoonyeshwa na WWF na UNESCO katika taarifa yake kwenda kwa waandishi wa habari, wao walitaja mradi kuwa chanzo cha kupungau kwa tembo wakati upungufu wa tembo ulikuwepo hata kabla ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa bwawa.
Tembo |
Mnamo Disemba 2018, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifunga mkataba na mkandarasi rasmi kuanza kazi ya ujenzi wa bwawa.
Kufuatia uamuzi wa kuendelea na mradi huo, UNESCO ilielezea wasiwasi wake kupitia taarifa kwa umma ambayo ilitaja masuala kadhaa kuhusu usalama wa hifadhi hii iliyo Urithi wa Dunia.
UNESCO ililalamikia uamuzi uliochukuliwa na serikali kwa sababu ya kuwepo kwa kiporo cha masuala kadhaa ambayo yalikuwa hayajapatiwa suluhisho na pande mbili kuhusu athari za uamuzi wa kujenga bwawa katika Pori la Akiba la Selous.
Maswala yanayohusu shirika hili la ulimwengu yalipelekwa kwenye mikutano ya hapo awali na uamuzi uliochukuliwa katika miaka ya 1982 wakati hifadhi ilipowekwa katika hadhi ya urithi wa ulimwengu, ambapo serikali ilionyesha nia ya kutumia eneo dogo la ardhi katika hifadhi kwa madhumuni mengine ya kiuchumi.
Kwa uhakika, utafiti wetu ulibaini kuwa pendekezo la kujengwa bwawa katika maporomoko ya Stigler’s lilibuniwa mwaka 1960, likarekebishwa mwaka 1972 na kukarabatiwa mwaka 1980, karibu miaka miwili kabla ya hifadhi kuteuliwa kama urithi wa ulimwengu.
Kwa hiyo uamuzi wa sasa wa serikali sio mpya na ulijulikana mapema kwa mashirika ya dunia kama ambavyo mawasiliano anuwai kati ya Serikali ya Tanzania na UNESCO kuhusu Uranium na mradi wa Umeme wa Stiegler’s kwa miaka kadhaa yanavyoonyesha.
Katika mawasiliano haya, kila upande ulijadili msimamo wake kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa upande mmoja na athari za kiuchumi kwa upande mwingine.
Kwa kuzingatia ushahidi huu, ni mantiki kuhitimisha kuwa eneo la hifadhi linaweza kutumika kwa miradi ya kiuchumi kwa faida ya watu wengi bila kuathiri sana mfumo wa ikolojia katika hifadhi.
Baada ya uchambuzi, Serikali ya Tanzania iliiomba UNESCO kuiondoa hifadhi hii kutoka kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa ulimwengu yaliyo hatarini.
UNESCO walikataa ombi hili katika vikao vyake vya 36, 40 na 41 (Saint-Petersburg, 2012; Istanbul / UNESCO, 2016; Krakow, 2017).
UNESCO walitaja kushuka kwa idadi ya tembo kutokana na ujangili mzito bila kufanya juhudi zozote za kupata sababu sahihi za tukio hilo ambalo tayari lilikuwa limebaki kuwa historia.
Kwa kuwa SGR iko kwenye uwanda unaofunika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 50,000 za msitu, Mto Rufiji na vijito vyake pamoja na korido ya Selous-Niassa kuelekea Msumbiji, ikiwa na kilomita za mraba 42,000, zote hizi zinaweza kuwa ni sababu mbili zilizochangia katika kushuka kwa idadi ya tembo katika miaka husika kwa sababu ya kupalilia ujangili.
Pori la Niassa, Msumbuji |
Kwa maoni yetu, ni jambo muhimu kutamka kuwa kuhifadhi mazingira peke yake sio kitu cha thamani kwa kizazi cha leo ikiwa hakuruhusu utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa watu.
Kwa hivo tunaona kwamba, miradi ya kuhifadhi mazingira na miradi ya maendeleo ya kiuchumi havitenganishiki kamwe.
Kutokana na ukweli huu, hamu ya taifa kujenga bwawa juu ya Mto Rufiji ilichukua msimamo tofauti wakati mradi huo ulipojumuishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2025 na baadaye kuingizwa katika Mpango Kabambe wa Mfumo wa Umeme wa Tanzania (2016).
Dira ya kuelekea 2025 na Mpango Kabambe wa Mfumo wa Umeme (2016) ni mikakati inayotafuta kutimiza mahitaji ya umeme wa bei rahisi, wa uhakika na endelevu kwa ajili ya kukukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kwa hivo, ukisoma kwa makini Mpango Kabambe wa Mfumo wa Umeme Tanzania (2016) mkazo ni juu ya matumizi ya nishati mbadala, ambayo inajumuisha umeme wa maji.
Mpango mkuu wa kuzalisha umeme unaonyesha thamani kubwa ya uwekezaji kwenye vyanzo vingine lakini haukukataa kabisa matumizi ya umeme wa maji, kwa kuwa umeme wa maji unazalisha faida kubwa kutokana na mtaji kidogo kwani ndio mfumo wa kuzalisha umeme wenye gharama ndogo zaidi za kuzalisha yuniti moja ya nishati, yaani shilingi 36 kwa kila yuniti.
Mpango huu pia unataja hitaji la kushughulikia nishati ya nchi ambayo ni ya bei rahisi na endelevu ifikapo mwaka 2040.
Serikali ya Tanzania inatarajia kuunganisha kwenye gridi ya taifa zaidi ya asilimia 90 ya kaya zake ambazo ni sawa na asilimia 70 ya idadi ya watu wanaoishi katika maeneo ya vijijini, ambao hutumia nishati ya jadi haswa kuni katika kaya zao.
Grid ya Taifa |
Chimbuko la nishati nchini Tanzania ni pamoja na kuni asilimia 90, mafuta ya petroli asilimia 8, umeme asilimia 1.5, na vyanzo vingine asilimia 0.5.
Aidha, chini ya asilimia 30 ya Watanzania wa wijijini wanapata umeme, jambo ambalo linamaanisha kwamba asilimia 80 ya nishati inayotokana na kuni inatumiwa katika maeneo ya vijijini.
Kwa hivyo, utegemezi mzito kama huo kwenye kuni unamaanisha uharibifu wa misitu yetu kwa sababu ya ukataji mkubwa wa miti. Tanzania ina msitu unaofunika eneo la kilometa za mraba 35,257 ambazo zinamomonyoka kwa kasi ya takriban kilometa za mraba 412 kila mwaka.
Zaidi ya hayo uchambuzi ulionyesha kuwa ukosefu wa umeme wa uhakika na wa bei rahisi ulilazimu watumiaji wengi katika sekta za biashara, viwanda na makazi kutumia jenereta za dizeli, na imebainika kuwa karibu asilimia 45 ya wafanya biashara nchini Tanzania wanamiliki jenereta za dizeli kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa usambazaji wa umeme, licha ya bei kubwa za dizeli na madhara yake kwa mazingira.
Ukubwa wa nishati ya kuni ambayo inatumika kama chanzo kikuu cha nishati katika jamii na taasisi za vijijini, na matumizi ya jenereta za dizeli zinazomilikiwa kibinafsi, vimeilazimu nchi kutafuta umeme wa uhakika na wa bei rahisi kwa wote.
Mwishowe nishati hii itapunguza kasi ukataji miti na kwa hiyo kudhibiti kiwango cha mmomonyo wa hifadhi za misitu.
Wakata kuni wakisafirisha kuni |
Ikiwa tunaweza kudhibiti au kupunguza matumizi ya kuni, hakika tutaweza kupunguza wasiwasi kuhusu ukataji miti.
Kuna uhusiano wa sababu na matokeo kati ya misitu na upatikanaji wa mvua, kwa maana kwamba misitu iliyohifadhiwa vema itasababisha kuongezeka kwa mvua na hivyo kuongezeka kwa usambazaji wa maji.
Na njia pekee ya kubadili mwelekeo wa ukataji miti ni kutoa umeme wa kuaminika na wenye bei rahisi katika maeneo ya vijijini na kwa hivyo hupunguza sana utegemezi wa kuni kama chanzo cha nishati.
Kwa hiyo, uamuzi wa kuchagua umeme wa maji kama chanzo cha nishati ni muhimu, kama ukilinganishwa na gesi asilia, makaa ya mawe, mafuta, jotoardhi, nyuklia na kadhalika.
INAENDELEA