NA MWANDISHI WETU
Mkazi mmoja wa Magomeni jijini Dar es Salaam anayedaiwa kufanya biashara ya kusafirisha binadamu katika nchi za maziwa makuu amejitetea kuwa yeye ni wakala wa visa wa ubalozi wa Saudi Arabia hapa nchini.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jana ofisini kwake Kariakoo karibu na makao makuu ya klabu ya Yanga, Jangwani Dar es Salaam, mtu huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) alisema ofisi yake inajishughulisha na uwakala wa visa kwa watanzania na raia wa mataifa ya kigeni wanaotaka kusafiri kwenda Saudi Arabia.
Alisema ofisi yake hiyo ameifungua miaka miwili iliyopita lakini tangu ilipoanza kufanyakazi hajawahi kupata mteja wa kumsafirisha.
Ali alikanusha madai kuwa amekuwa akijihusisha na biasharaya kusafirisha watu kwenda Falme za Kiarabu kwa ajili ya kufanya kazi za ndani lakini anaowasafirisha wanapofika huko hukamatwa mateka na hufungiwa katika nyumba za siri kabla ya kuanza kutumikishwa kwenye maeneo ya starehe nyakati za usiku.
Alisema anayo barua kutoka Serikali ya Saudi Arabu inayomtambulisha kuwa wakala wake wa visa aliyoionyesha ikiwa imebandikwa ukutani ndani ya ofisi yake lakini alipoombwa ionwe na kupigwa picha alikataa.
“Hayo madai si ya kweli, mimi ni wakala wa visa wa Serikali ya Saudi Arabia, ninawatafutia visa watu wanaotaka kusafiri kwenda Saudi Arabia lakini sijawahi kujihusisha na biashara ya kusafirisha watu.
“Ofisi hii nimeifungua miaka miwili sasa na tangu niifungue sijawahi kusafirisha mtu, ninayo barua inayonitambulisha kuwa wakala wa visa wa Saudi Arabia, hiyo hapo na najua serikali ilikwishataza kabisa hiyo biashara.
Majuzi hapa tuliitwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, tulikuwa na kikao kirefu sana na mimi nilihudhuria. Walitupa maelekezo ya kufanya kazi zetu kwa sababu kuna tatizo kubwa sana la waafrika wanaokwenda nchi za kiarabu kuteswa na kuuawa huko,” alisema Ali.
Uchunguzi wa muda mrefu wa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu mtandao wa biashara ya kusafirisha watu umemtaja mtu huyo kuwa mmoja wa watu wanaojihusisha na biashara hiyo na anasafirisha zaidi raia wa Tanzania na Burundi pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Mtu hyo anadaiwa kusafirisha watu wasiopungua 2,000 kila mwaka akiwaahidi kwenda kufanya kazi katika mataifa ya Arabuni na hasa Oman.
Katika uchunguzi wake Tanzania PANORAMA Blog limebaini kuwa mtu huyo mbali na kuwa na ofisi Karioakoo, alikuwa na ofisi nyingine maeneo Mwananyamala ambako alikuwa akihifadhi hati za kusafiria za watu waliokuwa kwenye orodha ya kusafirishwa lakini baada ya kupata msukosuko kutoka kwa maofisa wa serikali aliihamishia Magomeni.
Tanzania PANORAMA Blog litachapisha rupoti maalumu kuhusu uchunguzi lilioufanya kuhusu biashara hiyo haramu.