Shehena ya mbolea ambayo imekuwa ikisambazwa hapa nchini, (Picha kwa hisani ya mtandao) |
NA CHARLES MULLINDA
MIKATABA ya biashara ya mbolea yenye thamani ya mabilioni ya shilingi, baina ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Kampuni ya Export Trading Group (ETG), (INPUT) ya jijini Dar es Salaam, imepotea.
Mikataba hiyo imepotea katika Ofisi za Makao Makuu ya TFC zilizoko Oysterbay jijini Dar es Salaam na inahusisha biashara iliyofanywa kuanzia mwaka 2016 ambapo ETG ilikuwa ikiiuzia TFC mbolea.
Kupotea kwa mikataba hiyo kumethibitishwa na Meneja Mkuu wa TFC, Kanjel Mloba ambaye tangu Desemba 3, mwka jana hadi sasa amefanya jitihada za kuitafuta ofisini kwake pamoja na kwenye ofisi za wasaidizi wake bila mafanikio.
Kupotea kwa mikataba hiyo kulibainika baada ya Kanjel kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog, mapema Disemba, 2020, iliyoomba ufafanuzi kuhusu madai ya kuwepo ufisadi mkubwa katika biashara ya mbolea baina ya TFC na ETG.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORANA Blog zilidai kuwa kwa miaka mingi ETG imekuwa ikiiuzia serikali mbolea kupitia TFC na kuchuma mabilioni ya fedha kwa kufanya udanganyifu katika shehena inayochukuliwa na serikali kutoka kwa ETG.
Kwamba, TFC huwa inasaini mikataba ya kununua tani nyingi za mbolea kutoka ETG lakini kiuhalisia TFC huchukua tani kidogo na kuacha nyingine ambazo huuzwa kwa wateja wengine.
Inadaiwa zaidi kuwa, licha ya TFC kuchukua kiasi kidogo cha mbolea na kuacha nyingine ikiuzwa kwa wateja wengine, ETG hupeleka hati za madai za kulipwa tani zote za mbolea zilizo kwenye mkataba pamoja na gharama za kuhifadhi (Storage) kwa mbolea ambayo haikuchukuliwa na TFC.
Moja ya nyaraka, miongoni mwa zinazoelezea kuwepo kwa ufidadi huo ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona, inasomeka hivi; ‘wizi mkubwa umekuwa ukifanyika eneo la confirmation debit. Wizi umefanyika miaka yote kwa kulipia mbolea hewa.
‘Kwenye deni la USD 3.1 milioni, kuna mbolea ambayo haikuchukuliwa na TFC ambapo meneja wa TFC, Ndg, Salum Mkumba (sasa amestaafu) na Meneja wa ETG (INPUTS) Ndg Manoj, walitakiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo waandae taarifa ili kupata deni halali, wao hawakutekeleza agizo hilo kwa lengo la kuficha ufisadi wao.’
Kanjel alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog mapema mwaka jana kuhusu tuhuma hizo alisema ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi, mikataba ya mauzo ya mbolea baina ya ETG na TFC hajaiona.
Alisema hayupo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza au kuitafuta mikataba kwa wakati huo kwa sababu alikuwa akijisikia vibaya na alikuwa akijiandaa kwenda hospitali kwa matibabu hivyo atafutwe Disemba 5, 2020 atakuwa amekwishaitafuta na kuiperuzi mikataba yote kuona kama ina dosari yoyote au lah ndipo atoe kauli yake.
Disemba 5, 2020 Tanzania PANORAMA Blog iliwasiana na Kanjel kumuuliza kuhusu alichogundua kwenye mikataba baina TFC na ETG kama alivyokuwa ameelekeza lakini alisema bado anaumwa.
Disemba 7, 2020 Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Kanjel kwa mara nyingine na yeye alisema bado hayuko vizuri na kuelekeza atumiwe maswali kwenye e mail yake ili aweze kuyatafutia majibu jambo ambalo Tanzania PANORAMA Blog ililitekeleza.
Disemba 10, 2020 Tanzania PANORAMA Blog ilimtafuta Kanjel kuomba majibu ya maswali yake na yeye alijibu mikataba hiyo haionekani hivyo bado anaitafuta na amewaelekeza pia wasaidizi wake waitafute.
Disemba 11, 2020 Tanzania PANORAMA Blog lilimuuliza Kanjel iwapo mikataba husika imepatikana na yeye alijibu kuwa bado anaumwa na mikataba haijapatikana.
Disemba 15, 2020 Kanjel alitafutwa tena na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu suala hilo hilo na kujibu kuwa amesafiri kikazi kwenda mkoani Dodoma lakini mikataba hiyo haijapatikana bado inatafutwa.
Januari 13, 2021 Tanzania PANORAMA Blog liliwasiliana tena na Kanjel na kumuuliza iwapo mikataba hiyo imepatikana na kumkumbusha kujibu maswali aliyotumiwa na yeye alisema mikataba hiyo haipo.
Alipoulizwa Afisa Masoko ya Kampuni ya ETG, aliyejitambulisha kwa jina la Salome Ncheye kuhusu madai hayo alihoji kwanini jambo hilo linafuatiliwa sasa.
“Haya mambo yalifanyika huko nyuma, kwanini unayafuatilia sasa? Wakati yanafanyika mlikuwa wapi? Hiyo mikataba wewe unayo, unaweza kuitoa ukaonyesha kuthibitisha kama hiyo biashara ilikuwepo?
Magari yakipakia mbolea katika ‘yadi’ ya ETG |
“Tambua hiyo ni mikataba ya siri, nakushangaa unauliza kama umewahi kuiona. Hiyo mikataba nakwambia ni siri baina TFC iliyosaini kwa niaba ya serikali ya muuzaji ETG, wewe umeiona wapi? Kuna nini hapa katikati? Umetumwa na nani? Sisi tunafanya biashara sana na serikali. Nikushauri tu, achana na mambo yasiyokuhusu,” alisema Salome.
Tanzania PAMORAMA Blog itaendelea kuripoti sakata hili kulingana na mwenendo wa uchunguzi inayoufanya.