Saturday, April 19, 2025
spot_img

WATANZANIA NA USINGIZI WA NJOZI TATU

NA MWANDISHI WETU

KWA mwaka wa pili sasa, Watanzania wanalala usingizi ulioambatana na jonzi tatu.

Njozi hizo ni, mosi; Wakala wa Barabara (TANROADS), pili; barabara ya juu iliyopo eneo la Tazara inayofahamika zaidi kwa jina la Mfugale Flyover, na tatu; Mhandisi Patrick Mfugale.

Walianza kuota njozi hizi usiku wa kuamkia Septemba 16, 2018 baada ya kuanza kutumika kwa barabara ya juu ya Mfugale iliyopo eneo la Tazara, Septemba 15, 2018.

Kabla ya hapo, Watanzania hasa waliokuwa wakitumia barabara ya Julius Nyerere na Nelson Mandela, walikuwa wanaota wamefukuzwa au kupewa barua ya karipio kali kwa kuchelewa kazini.

Wasafiri walikuwa wanaota wameachwa na ndege au treni na wafanyabiashara waliota hasara na kupoteza saa nyingi wakiwa katika foleni.


Ali Msafiri, mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye alihudhuria uzinduzi wa Mfugale Flyover alinukuriwa na vyombo vya habari akieleza hivi:

“Kuzinduliwa kwa Mfugale Flyover kutaturahisishia usafiri wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na hata wasiokuwa wakazi wanaofika katika jiji hili kubwa la kibiashara nchini Tanzania.

“Wananchi tutakuwa tumepata fursa na foleni na msongamano utabaki ndoto sasa. Lile tatizo sugu na la miaka mingi la kwenda kazini sasa naona limeisha.”

Watanzania wengi walikuwa wakilala hoi kutokana na shida ya usafiri iliyokuwa ikisababishwa na foleni. Wakazi wa Jiji la Dar  es Salaam wanaotumia barabara za Nyerere na Mandela kwenda kazini na kurudi nyumbani walilazimika kulala kuanzia saa tano usiku na kuamka saa 10 alfajili ili kuwahi kupambana na foleni.

Wasafiri wanaosafiri kwa ndege au treni ya Tazara nao walilazimika kutenga muda wa hadi saa tatu za kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam au pembezoni kwenda uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere au Stesheni ya Reli ya Tazara kwa sababu ya foleni na msongamano wa magari.

Wafanyabiashara na wasafirishaji wanaotumia barabara hizo walikuwa wakipoteza fedha na muda mwingi kukabiliana na foleni na shughuli za kiuchumi kwa taifa na raia mmoja mmoja zilikuwa zikikutana na changamoto kubwa kutokana na tatizo la foleni katika barabara hizo.


Daniel Masanja, Dreva la roli ambaye mara nyingi hutumia barabara ya Mandela kusafirisha mizigo inayotoka bandarini ambaye naye alihudhuria uzinduzi huo, yeye alikaririwa akisema hivi;


“Kulikuwa na shida kubwa sana. Tulikuwa tunapoteza fedha nyingi sana kwa kukaa saa nyingi barabarani, sasa tutasafirisha mizigo ya wateja na kuifikisha kwa wakati, hakika tutaongeza tija. Tutalala tukiota njonzi njema za barabara ya juu ya Mfugale.”


Septemba 16, 2018, wanafunzi, wafanyakazi, wafanyabiashara, wasafirishaji na wasafiri walitumia barabara za Nyerere na Mandela kwa mara ya kwanza zikiwa hazina msongamano baada ya kuzinduliwa kwa Mfugale Flyover.

Mfugale Flyover ni barabara ya kwanza ya juu katika historia ya Tanzania inayounganisha sehemu kuu za Jiji la Dar es Salaam na maeneo makuu ya kiuchumi kama Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Bandari ya Dar es Salaam, machinjio ya Vingunguti na barabara zinazoelekea viwandani.

Ni barabara inayojumuisha njia kuu nne na daraja. Imetatua tatizo la msongamano na foleni na sasa imeongeza muda wa watu kufanya kazi badala ya kutumia muda mwingi wakiwa wamekwama barabarani kwenye foleni.


Kuanza kutumika kwa Mfugale Flyover kumewafanya Watanzania na wageni wanaotumia barabara za Nyerere na Mandela kulala usingizi mwororo huku wakiota ndoto ya kupita barabara ya juu ya Mfugale kuwahi katika shughuli zao za kiuchumi, masomo na usafiri.

Hii ndiyo ndoto ya kwanza ambayo Watanzania wanaota sasa kila walalapo usingizi.


Ndoto ya pili wanayoota sasa Watanzania ni TANROADS. Watanzaia wanaiota TANROADS kuwa taasisi yao iliyoshirikiana na kampuni kubwa ya ujenzi kutoka Japan ya Sumitomo Mitsui Construction Co. LTD kujenga barabara ya kwanza ya juu iliyopewa jina la Mhandisi Mfugale kwa mafanikio makubwa.

Wanaota maneno ya Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliyeitaka TANROADS kuitunza barabara hiyo na sasa ikiwa imepita miaka miwili tangu kuzinduliwa kwake, ipo katika mwonekano mzuri kutokana na uangalizi makini wa TANROADS.

Watanzania ambao sasa si taifa masikini tena wanaota mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo uliosainiwa Oktoba 15, 2015 kati ya Tanzania National Roads Agency (TANROADS) na Sumitomo Mitsui Construction Co.,Ltd. (SMCC), lengo likiwa kuboresha makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela. Lengo ambalo limefikiwa.

Awali wengi walikuwa wakiota kuwa ujenzi  wa barabara za aina hiyo hautawezekana Tanzania kwa sababu unagharimu matrilioni ya Dolla za Marekani ambayo Tanzania haina hivyo ili kuwa na barabara ya aina hiyo ni sharti kuomba mkopo kwa wazungu.


Sasa ndoto hizo hazipo, Watanzania wanaota shilingi bilioni 100 za kodi zao zinazokusanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuwa zinaweza kujenga barabara ya juu ya kisasa kama zile zilizoko Chicago na California nchini Marekani na wakiamka wanapita kwenye barabara ya aina hiyo.



Ni ndoto iliyosubiriwa tangu Aprili 16, 2016, siku ambayo Rais Magufuli alizindua ujenzi wa barabara hiyo ya juu.

Ndoto ya tatu inamuhusu Injinia Patrick Mfugale ambaye mchango wake katika ujenzi wa daraja hilo utabaki kuwa kielelezo cha Mtanzania mzalendo aliyetumia vema elimu yake kulinufaisha taifa lake.

Mhandisi Mfugale


Watu walio karibu pamoja na wasaidizi wake wanaeleza kuwa Injinia Mfugale ni mkali kwa watu wanaomsifia yeye binafsi hata kama anastahili kusifiwa. Anapenda sifa zinazomstahili zielekezwe kwa serikali anayoitumikia, taifa na Watanzania.

Kwa sababu ya ukali wake huo, Watanzania wamebaki kuuota uzalendo, utaalamu na uadilifu wake ndotoni. Haina shaka sifa zake nyingi zitatolewa hadharani na bila kuogopa katazo lake atakapokuwa hayupo.


Lakini kwa sababu katazo lake hilo siyo sheria hivyo haliifungi Tanzania PANORAMA Blog kumtendea haki, linafuata nyayo za Rais Magufuli ambaye kwa kuutambua mchango wake katika ujenzi wa barabara hiyo na utumishi wake uliotukuka kwa taifa alimpa heshima ya juu kwa kuiita kwa jina lake.


Dunia sasa inapaswa kumtambua Mhandisi Patrick Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi duniani aliyetumia utaalamu wake kujenga sehemu kubwa ya miundombinu ya barabara na madaraja ya taifa lake.

Kumbukumbu za kazi za kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog mpaka sasa zinaonyesha kuwa rekodi ya Mhandisi Mfugale ya kusaidia kujenga madaraja 1400 katika nchi ya baba na mama zake haijafikiwa na mhandisi mwingine yeyote duniani.

Rekodi zinamtaja pia Mhandisi Mfugale kuwa mtaalamu wa kwanza wa fani ya uhandisi duniani ambaye baada kupata elimu ya juu ya uhandisi nje ya nchi hakulikimbia taifa lake kwenda kufanya kazi ughaibuni ambako wahandisi hulipwa mishahara minono, bali alirejea kulijenga na mpaka sasa amebuni na kusimamia barabara za Taifa la Tanzania zenye urefu wa zaidi ya kilomita 36,258.

Kwa mujibu wa rekodi za kihandisi zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog, Mhandisi Mfugale ndiye pekee duniani mpaka sasa aliyetoa mchango mkubwa kwa nchi yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Watanzania wanaoota taswira ya Patrick Mfugale kila wanapopita juu ya Mfugale Flyover wanapaswa kukumbuka maneno yake mbele ya Rais Magufuli siku ya ufunguzi wa barabara hiyo ili yawajengee uzalendo, unyenyekevu katika utumishi na uwajibikaji, aliposema;


“Ukiwa waziri wa ujenzi ulinituma Japan kwenda kuweka sahihi mkataba wa kazi hiyo, lakini tulikuwa hatujapata mkandarasi na ulinielekeza kuwa nisirudi huku mpaka niwe nimesaini mkataba.

“Na nilipoiambia Japan nimeambiwa na nchi yangu nisirudi, wakasema viza yako imeisha, kwa hiyo ni lazima urudi, nikasema ninaweza nikakaa hata railway stesheni, ili mradi kama mkimbizi lakini tenda hii tutafute namna ya kufanya daraja hili lijengwe,”

Mtu huyu Mhandisi Patrick Mfugale alizaliwa mkoani Iringa na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Consolata ya mjini Iringa na 1975 alihitimu elimu yake ya shule ya upili katika shule ya upili mkoani Moshi.


Mwaka 1977, Mfugale aliajiriwa Wizara ya Ujenzi kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Rocky nchini India ambako alihitimu mwaka 1983  na kutunukiwa shahada yake ya kwanza ya uhandisi kisha akarejea nchini kuja kulijenga taifa lake

Mwaka 1991 Mhandisi Mfugale alisajiliwa kama mhandisi mtaalamu na mwaka 1992 aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.

Mwaka 1994 hadi 1995 alikwenda ughaibuni kusoma katika Chuo Kikuu cha  Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza ambako alihitimu ya kutunukiwa shahada yake ya pili ya uhandisi na kisha akarejea tena nchini kuendelea kulijenga taifa lake.

Mwaka 1995  aliteuliwa kuwa mhandisi mkuu wa madaraja nchini Tanzania na wakati huo huo akiwa masomoni nchini Uingereza alitafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini Tanzania.

Mhandisi Mfugale alibuni Daraja la Magarasi lenye mita 178 lililogharimu shilingi za Tanzania milioni 300 na pia, kwa uchache amejenga

Daraja la Mkapa Rufiji, Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbuji, Daraja la Rusumo, Daraja la Kikwete na  Daraja la Nyerere huko Kigamboni

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya