NA GEORGINA ROOSER
VYOMBO vya habari vya mataifa ya Ulaya na Marekani kwa mfano BBC, VOA, DW ni vyombo vya propaganda vya serikali za mataifa yao.
Hilo si tatizo kwa sababu kwa njia moja au nyingine serikali za nchi hizo ndiyo wamiliki wa vyombo hivyo wanapotutangazia katika Idhaa mbalimbali kama Kiswahili, Chichewa, Ndebele na nyinginezo ni kukidhi matarajio yao ya kueneza propaganda zao.
Ndugu zetu sasa wafanyakazi wageni wanaofanya kazi katika vyombo hivyo vya habari wanapaswa kuchanganya changanya kidogo akili zao na zile za mbayuwayu. Kadhalika serikali za nchi zetu nazo zijiongeze pia!
Vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani vinatangaza kwa lugha mbalimbali ulimwenguni kote. Vina majina makubwa sana na vina nguvu ya ushawishi wa mambo mbalimbali duniani. Hii inatokana na nguvu kubwa za serikali za nchi hizo katika dunia. Kwa maana hiyo hatuwezi kuviepuka vyombo vya habari vya mataifa hayo bali tunapaswa kushughulika navyo kimkakati.
Wenzetu wa nchi za Asia kwa mfano ni wajanja sana. Nchi zao huweka makachero katika vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani na matokeo yake propaganda za hawa mabwana wa magharibi huwa zinakwama.
Sisi waafrika tunashindwa vipi kubuni mbinu kupambana na hivi vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani? Hatuwezi kuwatimua kwani tunahitaji vidola vyao watatunyima na wataturindimishia madebe matupu usiku kucha kuwa tunabana Uhuru wa vyombo vya habari. Hapatakalika.
Miaka ya 2000s nilikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo katika moja ya vyombo hivi huko ulaya. Kulikuwa ni uchaguzi wa Liberia ambapo mwanasoka maarufu, George Weah alikuwa akigombea urais wa Liberia.
Nakumbuka siku moja nikapewa habari ya kizungu niitafsiri ili itangazwe katika Idhaa ya Kiswahili. Maelekezo kutoka kwa wenye nchi yalikuwa “marufuku” kuanza na “Mchezaji maarufu wa soka barani Afrika, bwana George Weah”Nilitakiwa kuanza na George Weah tu au “mgombea …”
Ilikatazwa kumtangaza George Weah kuwa ni “mwanasoka bora au maarufu”. Fikiria habari hiyo ilikuwa inatangazwa kwa Kiswahili huku Afrika Mashariki. Wa Liberia hawakuwa walengwa na wala wasingeisikia na hata kama wangesikia wasingeelewa Kiswahili. Lakini magharibi huwa hawaachi mwanya wowote wakitaka lao!
Serikali ya nchi hiyo ambayo ndiyo wanaomiliki hicho chombo cha Habari walikuwa wanamtaka yule Hellen Johnson aliyekuja kuwa Rais wa Liberia baadaye ashinde uchaguzi ule. Hawakumtaka kabisa George Weah.
Nakumbuka nilihuzunika sana nilipopata yale maelekezo. Nikamfuata mama mmoja, Mtanzania mwandishi mahiri na wa muda mrefu pale. Nikaanza kujadiliana nae.
Nikamuonyesha ile habari na maelekezo yake. Akacheka sana akanambia sasa unataka kufanyaje? Nikamwambia huko Afrika tunamfahamu George Weah kama mchezaji bora na maarufu wa soka kuliko hata hivi anavyogombea urais. Ukimtaja George Weah soka ndiyo kitu cha kwanza kinachokuja kichwani.
Nikamwambia yaani nitasemaje tu “mgombea… au bwana George Weah bila kutaja soka? Mama yule aliendelea kucheka sana akachukua ile karatasi akaandika sentensi kama “mchezaji maarufu wa soka barani Afrika, bwana George Weah…Akanambia haya kaendelee, tukacheka sana baadae akanambia huo ndiyo uhuru wa habari wa jumba hili. kujiongeza ni muhimu. Yule mama alinifunza jambo kubwa sana siku ile.
Ninachotaka kuzungumza leo ni kwa baadhi ya wenzetu wenye vibarua katika haya mashirika. Hivi kuna tatizo gani kuripoti kuhusu habari za Afrika katika mrengo chanya?
Nimeona habari kuhusu Corona katika maeneo mbalimbali barani Afrika. Habari zote za Afrika Mashariki zinaiponda Kenya, Tanzania na namna walivyopambana na kudhibiti Corona. Nikajiuliza sasa Afrika ilipaswa kufanyaje masikini? Magufuli, Kenyatta wote hakuna aliyefanya zuri? Kweli?
Waandishi wa habari wanaofanya kazi katika Idhaa hizi zinazotutangazia moja kwa moja wangepigwa darasa la uzalendo kwa nchi zetu ili wakifika huko wajue namna ya kushughulika na propaganda za nchi wanakofanyia kazi.
Hatuwezi kuwalaumu kwani misimamo ya nchi hizo na vyombo vyao ni kuhakikisha propaganda za mataifa hayo ya magharibi zinafuatwa na kuenezwa barabara.
Kama unaendesha kipindi ukielewa fika lengo ni kutafuta habari hasi tu unaweza kuweka hiyo hasi lakini bado ukaripoti habari itakayokuwa chanya kwa Afrika.
Habari ya leo kwa mfano kuhusu Corona Afrika, ni kama ilikuwa inaonyesha Kenya sasa itapata maambukizi ya Corona kutoka Tanzania (habari hasi kwa Kenya). Bila shaka Tanzania ikajumuishwa vilevile kuelezewa kuwa legelege katika kupambana na Corona (habari hasi kwa Tanzania pia).
Hapa wangeweza kuendeleza ili kuifanya hiyo habari kuwa chanya kiujumla kwa Afrika Mashariki kwa kueleza namna shughuli za malori mpakani mwa Tanzania na Kenya zinavyoweza kupunguza kuyumba kwa uchumi katika eneo hili la Afrika Mashariki baada ya Corona.
Mzungu angepata stori yake hasi lakini na wao waafrika wenzetu wangekuwa wana stori yao chanya kututia moyo huku nyumbani.
Badala yake tukapelekwa Zimbabwe kuelezewa pia namna “LOCKDOWN” inavyoonyesha kuwatesa wazimbabwe. Sasa waafrika tufanyeje jamani?. Waliokaa bila lockdown wamekosea, waliokaa lockdown wamekosa pia.
Ipo haja kwa serikali za Afrika kuwasomesha waandishi wenzetu darasa la propaganda, uzalendo na mengineyo kama hayo au kwenda full force kama mataifa kadhaa ya Asia kwa kuweka majasusi kabisa kuwa ndiyo watangazaji na waandishi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi.