NA MWANDISHI WETU
BARABARA za juu zilizopo eneo la Ubungo zinazofahamika zaidi kwa jina la Ubungo Interchange ni picha halisi ya uchapakazi, uwezo wa kiuchumi na utaalamu wa Watanzania.
Kila mtumiaji wa barabara hizo, awe mtanzania au raia wa kigeni licha ya kuvutiwa na uzuri wake anapopita juu yake, picha ya raia wazalendo wa Watanzania wanaoipenda nchi yao, pia humjia akilini.
Ubungo Interchange imejengwa na vijana wa kitanzania waliokuwa asilimia 90 ya wajenzi wote, imesimamiwa na wataalamu wa ndani ya Tanzania ambao ni Wakala wa Barabara (TANROADS) wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Patrick Mfugale huku meneja mradi akiwa Mhandisi Barakaeli Mmari.
Mfugale
Saruji, mchanga, nondo na vifaa vingine vyote vilivyotumika katika ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango kikubwa ama zimetengenezwa na kuzalishwa na viwanda vya ndani vya Tanzania au ni vifaa vilivyo ndani ya Tanzania. Ubungo Interchange ni barabara za Watanzania zilizojengwa na Watanzania kwa kutumia akili, fedha, vifaa na nguvu kazi ya Watanzania wenyewe.
Barabara hizo za kuvutia katika ukanda wote wa Afrika Mashariki zinakutanisha barabara tatu za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro na ujenzi wake ulikamilika Disemba, 2020.
Rais Magufuli
Rais John Pombe Magufuli alipotangaza mpango wa ujenzi wa barabara hizo kulikuwa na mapokeo ya aina mbili, kwanza ni Watanzania waliopokea taarifa za mpango huo kwa furaha kwa imani kwamba zitapunguza au kuondoa kabisa tatizo la msongamano wa magari katika eneo la Ubungo ambalo lilikuwa likidumaza sana uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Furaha hiyo pia ilijengeka katika nyuso za wananchi wengi kwa matumaini ya kupata ajira na zaidi ni tamaa ya maendeleo. Kila Mtanzania alitamani kuiona Tanzania ikiwa na interchange yenye mwonekano wa zile zilizo kwenye mataifa ya dunia ya kwanza
Mapokeo ya pili yalikuwa ya husda kutoka kwa maadui wa taifa ambayo nayo yaligawanyika katika makundi mawili makuu; la kwanza ni lile lililotamani mpango huo usifanikiwe na sababu yao kubwa ni kutotaka kuiona Tanzania ikipiga hatua za kimaendeleo huku kundi jingine ni lile lililotaka lihusike kwenye ujenzi ili kwanza livune pesa na kutoa ajira kwa watu wao ambao haina shaka wangeletwa kwa wingi kufanya kazi kwenye mradi huo na pia kutamani Tanzania iendelee kuwa tegemezi kwa kukosa pesa za ujenzi au kuomba msaada na wataalamu kutoka nje.
Matamanio haya yamekuwa hewa kwa sasa ambapo Watanzania wengi wanayaishi maono na falsafa za Rais Magufuli zinazowafanya watembee kifua mbele kwa sababu wanaamini wanaweza kuijenga nchi yao wenyewe na TANROADS imekuwa mfano bora kabisa katika hili.
Mei 2020, Mhandisi Barakaeli Mmari alipoutangzia umma kuwa kwa mara ya kwanza barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro itafunguliwa kwa majaribio ifikapo Mei 30, 2020 kwa kuruhusu magari kupita na Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma itafunguliwa kwa majaribio pia, Watanzania na raia wa nchi jirani wanaotumia barabara ya Morogoro kama lango kuu la kuingilia jijini Dar es Salaam walianza kushuhudia picha halisi ya Tanzania mpya.
Mhandisi Mmari ambaye alitoa darasa la matumizi ya barabara hizo alisema kuna barabara ngazi tatu, ya chini, ya kati na ya juu. Ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda mjini. Vile vile, itatumiwa na magari yote yatakayokuwa yanapinda kushoto kwenye maungio hayo.
Alisema ngazi ya kati itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara.
Ngazi ya juu itatumiwa na magari yatokayo Mwenge kwenda Buguruni na yatokayo Buguruni kwenda Mwenge.
Mhandisi Mmari alisema barabara za juu zimejumuisha njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi.
Hivi sasa, Watanzania wakiwa wamezama katika ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa, picha halisi ya ubora wa miradi hiyo inaonekana kwa kutazama na kupita juu ya barabara za ghorofa za Ubungo Interchange.