NA GEORGINA ROESER
HISTORIA ya Tanzania ina mashujaa wake. Mtemi Milambo wa Wanyamwezi ni miongoni mwa mashujaa wa Taifa letu ambaye historia yake tumeienzi kwa kuwa na shule za serikali za msingi na sekondari zilizobeba jina lake.
Mtemi Milambo aliishi miaka 44 kuanzia mwaka 1840 hadi mwaka 1884. Kifo chake inategemea na historia utakayoamini.
Kuna historia inayosema aliuawa kwa sumu na ndugu yake. Ipo pia simulizi kuwa alinyongwa na watu wake kulingana na desturi za wakati huo za wanyamwezi kuwaua kwa kuwanyonga watemi wao waliokuwa wagonjwa.
Historia nyingine inaeleza kuwa aliuawa na mwili wake kukatwa na kuzikwa sehemu tofauti tofauti. Historia nyingine inasema Mtemi Milambo alifariki kifo cha kawaida kabisa baada ya kuugua.
Vyovyote kifo chake kilivyotokea, Mtemi Milambo anakumbukwa kuwa ni miongoni mwa wapiganaji walioongoza mapambano dhidi ya maharamia wa kiarabu na kizungu katika karne ya 19, maharamia waliojishughulisha na biashara dhalimu ya utumwa na pembe za ndovu.
Kazi za Mtemi Milambo ziliwaokoa pia mateka wa kirundi na Congo waliokuwa wakisafirishwa kwenda Zanzibar kuuzwa utumwani.
Siandiki hapa leo kuelezea historia ya Mtemi Milambo. Niliyoandika hapo juu ni kwa uchache tu kuonyesha mema aliyoyafanya Mtemi Milambo kwa Taifa letu. Historia yake ni pana na hata upungufu wake uliokuwepo kutokana na utawala wake miaka ile tunapaswa kuenzi mchango wake kwa taifa letu . Vizazi vijavyo vinapaswa kufahamu historia ya Mtemi huyu mashuhuri barani Afrika kwa wakati wake.
Ninaandika kwa masikitiko kushuhudia namna historia na kumbukumbu ya Mtemi Milambo isivyoridhisha.Pichani chini ni kisima cha maji kilichokuwa ndani ya ngome ya Mtemi Milambo. Ngome hiyo ipo Ulyankulu Tabora barabara ya 13. Kama unavyoona kisima hicho kimeachwa tu kama si kitu chochote cha thamani katika historia ya Taifa letu! Tumesikitisha kama Taifa!
Kisima hiki hii leo kina umri zaidi ya miaka 160 kinatoa maji watu wanateka wanatumia. Kimeachwa wazi tu mbuzi, paka, mbwa na wanyama wengine wamewahi kutumbukia na kufa humo kisimani. Haijawahi kushtua uongozi wowote hata wa soko tu la hapo barabara ya 13 kuwa kuachwa wazi kisima hicho ni hatari kwa maisha ya watu pia.
Kisima hicho kwa maoni yangu ni historia ya Mtemi Milambo. Kwanini hatukienzi? Niliwahi kufika Kigoma miaka michache iliyopita. Kuna eneo Kigoma linamuenzi Livingstone. Muite Livingstone vyovyote utakavyopenda. Kwangu Mimi alikuwa mkoloni tu wa kizungu!
Hapo kwa Livingstone pamejengwa kumbukumbu tena unafika kwa kiingilio!Mtemi Milambo kisima alichochimba kinachowapa maji wana Tabora hadi leo hii hakina hata mfuniko au kujengewa kumbukumbu yeyote? Watanzania sisi wakati mwingine tuna matatizo gani?
Inasemekana kuna mti mkubwa aliokuwa akinyongea wahalifu. Mti huo hivi karibuni kuna mtu kaukata kwa matumizi ya kibinadamu.
Mimi si mshabiki wa mauaji ya binadamu lakini mti huo kama ni kweli au si kweli ulitumika kwa kazi ya kunyonga unabaki kuwa historia. Tulipaswa kuenzi historia hiyo jinsi ilivyo.
Ngome ya Mtemi Milambo imebaki tuta tu linalodharauliwa na kutupiwa takataka. Inasikitisha sana. Sikutegemea kazi ya Mtemi Milambo labda iliyokuwa mimicked na majeshi yetu miaka mingi baadaye itekelezwe kiasi hiki! Aibu yetu kama Taifa! Viongozi wote wa Tabora aibu yenu!
Pumzika kwa amani Mtemi Milambo. Shujaa wa Mashujaa.