Wednesday, December 25, 2024
spot_img

TANZANIA INUNUE PETROLI IWEKE AKIBA

 

NA GEORGINA ROESER

BEI ya Petroli iimeshuka. Iko chini sana karibu duniani kote. Hii ilitokana na uzalishwaji mkubwa wa mafuta huko Urusi na Saudi Arabia.

Mataifa haya mawili yana msuguano wa kibiashara unaohusu bei ya mafuta. Kwa sababu ya msuguano huo, mataifa haya kila moja liliamua kuzalisha mafuta zaidi ya maradufu ya uzalishaji wake wa kawaida. Hapa ndipo neema ya kushuka kwa bei ya mafuta kwa mataifa yasiyozalisha nishati hiyo ilipoanzia. Vita vya panzi, kuku wanapeta.

Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump hakuupenda msuguano huo kwa sababu taifa lake kwa sasa ni miongoni mwa mataifa yenye mafuta mengi duniani.

Historia inaonyesha kuwa Marekani imekuwa ikipigana vita katika mataifa mbalimbali ya Ghuba kwa miaka nenda rudi na kupora mafuta yake.

Uporaji huo wa Marekani ndiyo ulioiwezesha kuwa na hazina kubwa ya mafuta. Hivi sasa Marekani ina jeuri ya kukaa meza moja na wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani kama Urusi na Saudi Arabia baada ya kujilimbikizia bidhaa hiyo kwa njia ya uporaji.

Tukiachana na hilo. Ukweli mwingine ni kwamba Wamarekani wengi waliwekeza katika biashara ya mafuta baada ya biashara zao za vita kuanguka hivyo wana hazina kubwa sana ya Nishati hiyo waliyopora Mashariki ya Kati.

Tangu Urusi na Saudi Arabia wamwage mafuta kedekede duniani, Marekani ilianza kupoteza mapato kutokana na bei ya mafuta kuwa chini sana miezi ya hivi karibuni. Wafanyabiashara wengi wa mafuta Marekani walikuwa wakilalamikia sana hali hiyo mwishoni mwa mwaka jana na mapema Mwaka huu.

Kabla ya kivumbi cha Corona, Rais Trump alitangaza kuwa ataomba ‘poo’ kwa Urusi na Saudi Arabia waache kufanya uzalishaji mkubwa wa mafuta ili bei ipande Wamarekani waweze kuuza mafuta yao kwa bei ya juu.

Urusi na Saudi Arabia walikubali kujadili kilio hicho cha Rais Trump lakini kabla ya kutekeleza hilo Corona ikabisha hodi. Sijui mazungumzo yalipoishia lakini bei ya mafuta sasa IPO chini  kila kona ulimwenguni.

Kufupisha mjadala huu ni kwamba Corona ikishaondoka vichwani vya watu, kuna uwezekano Urusi na Saudi Arabia wakafanya uzalishaji mkubwa ili kujipatia kipato cha kupambana na madhara ya Corona kiuchumi. Hili likifanyika litakuwa neema kubwa duniani kote.

Kwa upande mwingine kuna uwezekano pia Rais Trump akawalipa fedha nzuri sana tu Urusi na Saudi Arabia wasizalishe  kwa  wingi mafuta yao ili bei ipande, Marekani iuze kwa bei kubwa mafuta yake.

Marekani iko tayari kutoa kiasi kikubwa kwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani kwa sababu haiwezi kuuza mafuta yake kwa bei ya chini kama Urusi na Saudi Arabia kwa sababu mafuta yake iliyapata kwa gharama kubwa sana wakati mataifa yanayozalisha yenyewe yanachimba tu. Hii ndiyo sababu Marekani inataka bei ipande wakati wote.

Upo uwezekano Urusi na Saudi Arabia zitampuuza Rais Trump lakini hilo hatupaswi kulizingatia sana kwa sababu lolote lile linawezekana kutokea.

Sasa nini dunia inayoendelea ikiwemo Tanzania, inapaswa kufanya wakati kama huu?

Kati ya mambo ambayo Afrika inapaswa kuiga kutoka Marekani; cha kwanza ni choo na mfumo wa maji taka.

Nikiri kuwa nikiwa mkazi wa hapa, vyoo vyao ni vizuri sana. Tunapaswa  kuanza kuiga hilo siyo ule upuuzi  wao wa uhuru wa vyombo vya habari, haki za binadamu na Demokrasia.

Hapa kwenye mafuta tunapaswa kuiga pia. Tunapaswa kufanya vile vile kama walivyofanya Marekani. Lakini sisi tusiende kupora bali tukanunue na tuweke hazina kubwa.

 Huu ni wakati muafaka kwa nchi yetu kununua mafuta na kuyahifadhi kama ambavyo Marekani ilifanya miaka ya nyuma. Tukanunue kwa bei poa ya sasa na tuyahifadhi kama Marekani walivyofanya.

Hatujui tunakoelekea bei itakuwaje. Kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta ni jambo la kuzingatiwa. Nchi kama yetu ikibidi hata tutakope Urusi au Saudi Arabia mafuta mengi hivi sasa bei ikiwa chini ili baadaye tusije kupoteza fedha nyingi bei itakapopanda.

Kama tuna fedha taslimu ni vema tulipie mzigo wrote tutakaonunua lakini hata kama tumepungukiwa tukakope tu hayo mafuta. Urusi kwa mfano ni marafiki zetu sana, hawatatunyima. Saudi Arabia pia hawatatunyima.

Kuna uwezekano mkubwa bei ya mafuta itapanda siku chache zijazo kwa sababu nilizozieleza hapo juu.

Marekani ina ushawishi mkubwa duniani kibiashara. Urusi na Saudi Arabia watahitaji fedha baada ya Corona. Marekani kwa ninavyowafahamu watawalipa Urusi na Saudia mabilioni wapunguze uzaliahaji.

Wakati ni huu. Binafsi naiona hii ni fursa kubwa sana inayoweza kupaisha uchumi wetu tukichanga karata zetu vema.

 .

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya