![]() |
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Paschal Shelutete |
NA MWANDISHI MAALUM – ARUSHA
MAMLAKA ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), imeshinda tuzo ya dhahabu ya kimataifa ya utoaji huduma bora kwa mwaka 2020 inayotolewa na Taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR).
Taarifa ya ushindi huo imetolewa leo na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Pascal Shelutete ambaye ameeleza kuwa tuzo hiyo itakabidhiwa kwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jesta Nyamanga, wiki ijayo, jijini Brussels.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kamishna Shelutete ameeleza kuwa TANAPA imeibuka mshindi miongoni mwa washindani 51 kutoka nchi 39 duniani.
“Tuzo za ESQR za huduma bora hutolewa kila mwaka na Shirika la ESQR kwa kutambua taasisi za serikali na zisizokuwa za kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za viwango ya juu. Washindi wa tuzo hii huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa na taasisi zilizoshinda tuzo hizo awali, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.
“Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo hii unajumuisha utafiti wa taarifa mbalimbali kwa umma, machapisho, maoni chanya ya wateja, miradi ya kijamii na vyuo vikuu pamoja na maonyesho,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Kamishna Shelutete.
Anaandika zaidi kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya mikakati madhubuti ya TANAPA katika kuhifadhi rasilimali za hifadhi pamoja na mrejesho chanya kutoka kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.
“Utambuzi huu utakuwa chachu ya kuendelea kuongeza jitihada za uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu na kutangaza vivutio katika masoko mbalimbali na kuendelea kuboresha huduma za utalii,” inasomeka.
Taarifa hiyo inahitimishwa na wito kwa umma, taasisi za kitaifa na kimataifa na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kaktika kuhifadhi rasilimali za hifadhi ya taifa na kuunga mkono juhudi za kukuza utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.