![]() |
Katibu Mkuu, Akwilapo |
NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu wa Wazara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilapo amesema wajibu wa kumtafuta mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St Mary’s, Labna Said Salim aliyepotea akiwa chini ya uangalizi wa shule ni wa Jeshi la Polisi
Ameyasema hayo jana katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilimuuliza mchango wa wizara kumtafuta mwanafunzi huyo aliyepotea Oktoba 4, 2020.
“Hilo jambo wenye wajibu ni polisi na ndiyo maana sisi halijafika kwetu na hata kama lingekuwa limefika tungelipeleka polisi kwa sababu wao ndiyo wenye wajibu wa mambo kama hayo,” alisema Akwilapo.
![]() |
Labna |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramandani Kingai alipoulizwa jana kuhusu hatua waliyofikia katika msako huo alisema mpasa sasa hawafikiwa kumpata mwanafunzi huyo
Alipoulizwa kuhusu vijana saba waliokamatwa wakivuta bangi nyumbani kwa Kamishna Mstaafu wa Jeshi Magereza ambaye jina lake limehifadhiwa, Kamanda Kingai alisema vijana hao ambao ni wanafunzi bado wanafanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne hivyo wanasubiriwa mpaka watakapomaliza ndipo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Taarifa ya uchunguzi wa awali wa kupotea kwa mwanafunzi huyo iliyotolewa na Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kinondoni, Joseph Kapere ambaye ni mjumbe wa timu iliyoundwa na Serikali ya Wilaya ya Kinondoni kuchunguza kupotea kwa mtoto huyo, mahali alipo sasa na mazingira ya kutoweka kwake ilieleza kuwa timu hiyo ilithibitisha pasipo shaka kuwa Shule ya Sekondari ya St Mary’s Mbezi Makonde imepungukiwa sifa zinazostahili kutoa elimu kwa mwanafunzi.
Wajumbe wengine katika timu hiyo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ufisa Usalama na Mdhibiti wa Ubora wa Elimu Kanda.
Kapere alisema tayari Mkuu wa Shule ya St. Mary’s, Recca Ntipoo amehojiwa na kuungama kutenda makosa katika baadhi ya mambo kwenye sakata hilo na kwamba aliipeleka timu hiyo mahali alikodai Labna alikwenda kuishi na mpenzi wake baada ya kutoroka shule.
Alisema timu ilibaini shule hiyo ilifanya makosa kutotoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mtoto na pia kukaa kimya siku nne bila kutoa taarifa kwa wazazi kuhusu kutoweka kwake wala kuwajulisha kuwa amewaeleza walimu hataki shule.
Katika maelezo yake Kapere alisema, Ntipoo aliungama kufahamu vitendo vya mwanafunzi kutoka shule kwa kuruka ukuta usiku na kwenda maeneo hatarishi kwao jambo ambalo Mwalimu huyo aliliona kuwa la kawaida kwa sababu alikuta likifanyika shuleni hapo.
Aidha, Kapere alisema timu ilibaini shule hiyo kuwa na mazingira machafu, kukosa ulinzi wa kutosha na kutokuwa na ukuta imara.
Alisema mambo mengine yaliyogundulika katika uchunguzi wa timu hiyo ni kubainika kwa nyumba ya Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Magereza ambayo ina shamba la bangi ambamo walikutwa wavulana saba, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s waliokuwa wakivuta pamoja.
Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.
Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule lakini taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.
Katika hatua ya kushangaza, uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.